Maumivu: Bei ya mafuta ikiongezeka Tanzania
- Petroli imeongezeka kwa Sh149, Dizeli Sh25 na mafuta ya taa kwa Sh37.
- Ewura yatahadharisha kuongezeka kwa bei zaidi kutokana na umbali wa mikoa na bandari za mafuta
Dar es Salaam. Kwa mara nyingine tena watumiaji wa vyombo vya moto nchini wanaingia kwenye maumivu mara baada ya bei ya mafuta ya petroli kuongezeka kwa Sh149 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Kwa mujibu wa bei mpya za rejereja zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na kuanza kutumika leo Machi 1, 2023, bei ya petroli jijini Dar es Salaam imepanda hadi kufikia Sh2,968 kwa lita kutoka Sh2,819 iliyokuwa ikitumika Februari mwaka huu.
Pia bei ya mafuta ya taa na dizeli yanayoingia kupitia bandari ya Dar es Salaam nayo imepanda, jambo linalozidisha maumivu kwa wamiliki wa vyombo vya moto.
Dizeli inauzwa kwa Sh3130 kutoka Sh3,105 iliyokuwa inatumika mwezi uliopita ikiwa ni sawa na ongezeko la Sh25 kwa lita, huku mafuta ya taa yakipaa kutoka Sh3,061 hadi Sh3,098.
“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji (BPS Premium) na thamani ya shilingi ukilinganisha na dola ya kimarekani,” imeeleza taarifa ya Ewura.
Kwa mafuta yanaoingia kupitia bandari ya Tanga bei ya mafuta imepungua kulinganisha na mwezi Februari.
Soma zaidi
Kwenye bandari hiyo petroli inauzwa kwa Sh2,783 ukilinganisha na Sh2,848 iliyokuwa ikitumika mwezi uliopita, mafuta ya dizeli yanauzwa Sh2,998 kuanzia leo yamepungua kutoka Sh3,207 iliyotumika mwezi uliopita.
Wakati bei ya mafuta ikishuka kwenye bandari ya Tanga, bandari ya Mtwara imeendelea kupitia maumivu zaidi mara baada ya bei ya mafuta kuendelea kupanda, Mathalani petroli inauzwa Sh2,882 ukilinganisha na Sh2,744 iliyotumika mwezi Februari huku dizeli iliyouzwa Sh3,043 sasa inauzwa Sh3,111.
Kwa mujibu wa Ewura baadhi ya mikoa nchini ikiwemo mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma itapata maumivu zaidi ya bei hizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama za usafirishaji kutoka bandarini.
Wakazi wa Kyerwa mkoani Kagera ndiyo wananunua mafuta hayo muhimu kwa vyombo vya moto kwa bei ya juu kuliko wote nchini baada ya Ewura kubainisha kuwa bei kikomo ya petroli itakuwa 3,220.
Kwa wakazi wa mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma nao watanunua mafuta hayo kwa ongezeko la bei la Sh138 kwa lita wakati bei ya mafuta ya dizeli zinapungua kwa shilingi 68 kwa lita ukilinganisha bei za Februari