Mifuko kutoboka zaidi kwa wamiliki wa magari, petroli ikipanda

March 1, 2022 1:23 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Mafuta yameongezeka kwa Sh60 kwa upande wa bandari ya Dar es Salaam.
  • Kama Serikali isingefuta kodi, bei ingeongezeka kwa Sh160.

Dar es Salaam. Watumiaji wa mafuta nchini Tanzania watalazimika kutoboa mifuko yao zaidi baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za rejareja za nishati hiyo ambazo mwezi huu zimepaa ikilinganishwa na Februari 2022.

Ewura imetangaza leo Machi, bei mpya kikomo za mafuta za mwezi Machi 2022 na kuonyesha kuwa bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Taarifa iliyotolewa na Ewura kuhusu bei za mafuta zitakzoanza kutumika kesho, imeainisha kuwa huenda gharama za mafuta zingekuwa juu zaidi kama Serikali isingeahirisha kodi ya Sh100 kwa kila lita moja ya mafuta.

Kwa maana hiyo, mafuta yatakayopitia bandari ya Dar es Salaam, yatauzwa kwa bei pungufu ya Sh100 kwa miezi mitatu mfululizo.

Petroli itauzwa kwa  Sh2,540 ikiwa imepanda kwa Sh60 kutoka Sh2,480 mwezi Februari, dizeli Sh2403 ikipanda kutoka Sh2,338.

Hata hivyo, mafuta ya taa yameshuka hadi kufikia Sh2,208 kutoka Sh2,291. 

Maumivu hayo pia yatawagusa watumiaji wa nishati hiyo wa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara, inayopokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga ambako nako bei imepanda. 

Kwa ukanda huo, petroli itauzwa kwa Sh2,563, dizeli Sh2,484 na mafuta ya taa kwa Sh2,254.


Soma zaidi:


Pia bei za rejareja za mafuta ya petroli katika mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zimeongezeka ambapo petroli itauzwa kwa Sh2,577, dizeli Sh2,530 na mafuta ya taa kwa Sh2,280.

Waziri wa Nishati, Januari Makamba jana alitangaza kuahirisha ukusanyaji wa tozo ya Sh100 kwa kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa kipindi cha miezi mitatu tangu jana alipotoa tangazo hilo.

Tozo hiyo ilipaswa kulipwa na watumiaji wa mafuta nchini humo kuanzia mwezi Machi mpaka Mei, mwaka huu huku taifa likiendelea kutathmini mwenendo wa soko la dunia katika mafuta.

Hatua hiyo, itaifanya Serikali kukosa Sh30 bilioni kila mwezi.  Uamuzi huo umekuja kutokana na kupanda bei za mafuta katika soko la dunia kunakosababishwa na vita kati ya Urusi na Ukraine.

Enable Notifications OK No thanks