Maumivu, ahueni Ewura ikitangaza bei kikomo za petroli, dizeli Mei
-
Bei ya petroli, dizeli inayopitia bandari ya Dar es Salaam yapanda.
- Wakazi wa mikoa ya Kaskazini na Kusini kutumia bei za April 2023.
Dar es Salaam. Kwa mara nyingine tena watumiaji wa vyombo vya moto katika jiji la Dar es Salaam wanaingia kwenye maumivu mara baada ya bei ya mafuta ya petroli na dizeli kuongezeka kwa viwango tofauti ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Kwa mujibu wa bei mpya za rejereja zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na kuanza kutumika leo Mei 3, 2023, bei ya petroli jijini Dar es Salaam imepanda kwa Sh90 hadi kufikia Sh2,871 kwa lita.Pia bei ya dizeli yanayoingia kupitia bandari ya Dar es Salaam nayo imepanda kwa Sh24 hadi kufikia 2,871, jambo linalozidisha maumivu kwa wamiliki wa vyombo vya moto kwa sababu watatoboa mifuko yao zaidi kupata nishati hiyo.
Mathalan, mtu mwenye Sh10,000 atapata lita 3.4 za petroli.
Wakati bei ya petroli na dizeli ikipanda, bei ya mafuta ya taa imepungua kwa Sh99 kwa lita na sasa mafuta hayo yanauzwa kwa Sh2,830 kwa lita.
“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji (BPS Premium) na thamani ya shilingi ukilinganisha na dola ya kimarekani,” imeeleza taarifa ya Ewura.
Wakazi wa Ruberwa katika Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ndiyo wananunua mafuta hayo muhimu kwa vyombo vya moto kwa bei ya juu kuliko wote nchini baada ya Ewura kubainisha kuwa bei kikomo ya petroli na dizeli ni Sh3,109 kwa lita kila moja.
Kwa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara), bei za rejareja za Mei 2023 kwa mafuta ya petroli na dizeli zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Aprili 5 2023 kwa kuwa, kwa mwezi Aprili 2023, hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga.
Kwa mafuta ya taa, waendeshaji wa vituo kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta hayo kutokea bandari ya Dar es Salaam.
“Hivyo, bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo italingana na gharama za kupokelea mafuta hayo kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika,” imeeleza Ewura.
Wananchi wa mikoa Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma), bei za rejareja za Mei 2023 kwa mafuta ya petroli na dizeli zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Aprili 5, 2023 kwa kuwa, kwa mwezi Aprili 2023, hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara.
Aidha, kwa kuwa hakuna matanki ya kuhifadhia mafuta ya taa katika bandari ya Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya kusini wanashauriwa kuchukua mafuta hayo kutoka katika bandari ya Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta hayo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
“Tofauti ya bei kutoka sehemu moja kwenda nyingine inatokana na tofauti ya bandari mafuta yanapochukuliwa na gharama ya usafirishaji,” ameeleza taarifa ya mamlaka hiyo.
Latest