Ni ahueni Tanzania kushusha gharama za kupima Uviko-19?

August 19, 2021 12:27 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya Watanzania wasema zitawapunguzia gharama za maisha.
  • Wengine wasema zitafungua zaidi fursa za kibiashara na masomo nje ya nchini.
  • Waiomba Serikali ielekeze nguvu zaidi katika utoaji wa chanjo. 

Dar es Salaam. Kufuatia serikali ya Tanzania kushusha gharama za upimaji wa ugonjwa virusi vya Corona (Uviko-19), baadhi ya Watanzania wamesema ni ahueni kwa sababu itapunguza gharama za maisha na kuinua biashara huku wakitaka zishushwe zaidi.

Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kupambana na Uviko-19 ikiwemo kutoa chanjo na kupima wananchi na wageni wanaoingia na kutoka nchini ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima katika taarifa yake  ya Agosti 11, 2021 amesema Serikali imepunguza gharama za upimaji wa Uviko-19 kutoka Dola za Marekani 100 (Sh230,000) hadi Dola 50 (Sh115,000) kwa kipimo kikubwa aina ya “RT PCR” ambacho kinatumika kuwapima wasafiri wanaoingia na kutoka nchini.

Pia kwa kipimo cha haraka (Antigen Rapid test), gharama zake zimepungua kutoka Dola za Marekani 25 (Sh57,500) hadi Dola 10 (Sh23,189) ambapo watalipia wasafiri katika viwanja vya ndege. 

Kwa watu wanaopita mipakani hawatalipa gharama zozote kupata kipimo hicho ambacho hufanyika kwa wasafiri wote.

“Sababu za kushusha gharama za upimaji Uviko-19 inatokana na gharama za uendeshaji kutengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2021/22,” amesema Dk Gwajima katika taarifa hiyo.

Ni ahueni kwa Watanzania, wasafiri? 

Baadhi ya Watanzania, wafanyabiashara na wachambuzi wa masuala ya uchumi wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa uamuzi huo wa Serikali wa kupunguza gharama za vipimo vya Uviko-19 ni ahueni kwao na utatoa fursa zaidi ya wao kusafiri nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali za kibiashara na kimasomo.

Mtanzania ambaye anasomea shahada ya Uzamiri katika Chuo Kikuu cha Wasabato cha Fridensau, Ujerumani amesema gharama ya kupima Corona nchini Tanzania zilikuwa juu ikilinganishwa na baadhi ya nchi duniani, hivyo kuzishusha kutapunguza maumivu kwa wasafiri. 

Amesema awali alilazimika kulipia Dola 100 kupima Uviko-19 wakati anatoka Tanzania na akifika Ujerumani pia alitakiwa kulipia Euro 90 ambayo ni sawa na Sh244,900.

Hata hivyo, Serikali imeombwa kutokuwapima mara mbili watu ambao tayari wamepata vyeti vya Uviko-19 nje ya nchi ili kuwapunguzia gharama. 

“Naona si sahihi kwamba nikifika uwanja wa ndege Tanzania nipime tena Corona wakati tayari nilishapima huku na ni daktari  amethibitisha kuwa nipo sawa. Bora ingebaki kupima nikiwa nahitaji kusafiri,” amesema Gibbe wakati akiongea na Nukta Habari kutoka Ujerumani. 

Hata wakati Gibbe akishauri Serikali kuendelea kupunguza gharama hizo, mfanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo, Mashauri Mathias amesema hatua hiyo itawasaidia wafanyabiashara kutumia fedha hiyo katika mambo mengine.

“Wamekata kama nusu hivi ya gharama ya awali, hiyo walau tutaiacha hata nyumbani wanunue mboga. Zamani zilikua juu sana kwa kweli,” amesema Mathias.

Katika baadhi ya nchi, kipimo cha haraka ni bure. Picha| Quartz.

‘Gharama bado zipo juu’

Licha ya Serikali kushusha gharama za kupima Uviko-19, baadhi ya Watanzania wamesema bado zipo juu na kwa mwananchi wa kawaida kuzimudu itakuwa ni vigumu hasa wanaosafiri mara kwa mara.

Mkazi wa Mabibo mkoani Dar es Salaam, Magreth Shoni amesema ni wazi kuwa Serikali imetambua watu wengi wanashindwa kufanya kipimo cha Uviko-19 kutokana na hali ngumu ya kimaisha hata pale wanapohisi wanaumwa.

“Hatua hiyo itasaidia watu wengi hadi wale waliokuwa wanashindwa kwenda kupima. Kwa upande wangu bado hizo gharama siwezi kuzimudu,” amesema Shoni.

Kwa takwimu rasmi zilizotolewa mara ya mwisho na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hadi kufikia Julai 23, 2021, Tanzania ilikuwa na wagonjwa 858 wa ugonjwa wa Corona huku vifo vikiwa ni 29.

Naye Mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam, Omari Mikoma ameiomba Serikali ipunguze zaidi gharama hizo ili kupima iwe ni jambo ambalo hata wananchi wa kawaida wanaweza kufanya.

“Katika hali ya kawaida bado gharama ni kubwa ikibidi wapunguze zaidi,” ameshauri Mikoma.

‘Gharama siyo tatizo’

Wananchi wengine wamesema tatizo siyo gharama, elimu inatakiwa itolewe kwa watu kujitokeza kwa wingi kupima ugonjwa huo ili kujua hali zao. 

Msusi wa nywele kutoka Mikocheni mkoani hapa, Rayah Mpate amesema licha ya kuwa Serikali imepunguza gharama za kupima Corona, anaishauri ielekeze nguvu zake katika kutoa elimu ya kupambana na ugonjwa huo.

“Kupungua kwa gharama siyo ushawishi mkubwa kwa wananchi kwenda kupima Corona, unaweza kupunguza gharama na bado watu wasiende kupima, elimu iende kwanza kwa wananchi alafu vipimo viendelee,” amesema Mpate.

Kupungua kwa gharama za kupima Uviko-19 kunaweza kusaidia kufungua fursa za kibiashara na usafirishaji wa mizigo nje ya nchi na hivyo kuiongezea Serikali mapato. Picha| JamiiForums.

Kupungua kwa gharama za vipimo ni kicheko kwa wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi kwa sababu wataongeza kasi ya biashara na hivyo kuiongezea Serikali mapato.

“Huenda ikawasaidia wafanyabiashara zaidi kwa sababu wao ndiyo wanahitaji safari za mara kwa mara. Hata hivyo, bado gharama ziko juu ikilinganishwa na nchi nyingine ikiwemo Dubai ambayo kupima kipimo cha haraka ni bure,” amesema Redemptha Nsanzugwanko, mtaalamu wa masuala ya mawasiliano na masoko.

Naye Mshauri wa sekta binafsi na Msaidizi wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga amesema ni jambo jema kuwa Serikali imetambua gharama kubwa za kupima Uviko-19 na kuzipunguza kwa nusu ya gharama ya awali. 

Mzigo mkubwa ulikuwa umebebwa na wafanyabiashara kwa kuongeza gharama za usafirishaji baina ya nchi mbili, amesema Maganga. 

“Hivyo tunatarajia kuwa kushuka kwa gharama hizi zitaleta unafuu mkubwa kwa msafirishaji mizigo na mtumiaji wa mwisho hivyo kushusha gharama za huduma na bidhaa,” anasema Maganga. 

Habari hii imeandikwa na Rodgers George na Herimina Mkude.

Makala hii imeandaliwa kwa ushirika na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).  

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW