Ndugu wa aliyechomwa moto na mwajiri wake Mwanza, washinikiza hatua zaidi za kisheria
- Wasema kitendo alichofanyiwa ni kinyume na sheria.
- Jeshi la Polisi latoa rai kwa wananchi kutojichukulia sheria mkononi.
Mwanza. Siku moja baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kutangaza kumshikilia Christina Shiriri mkazi wa Usagara kwa tuhuma za kumchoma moto mfanyakazi wake wa nyumbani, baadhi ya ndugu na jamaa wa mfanyakazi huyo wameiomba Serikali kumchukulia hatua kali, kutokana na kitendo hicho cha kikatili.
Kaka wa majeruhi, Joseph Semando ameiambia Nukta Habari kuwa alipata taarifa ya kuunguzwa kwa mdogo wake kwa njia ya simu usiku wa kuamkia Juni 2, 2024 ambapo alifanikiwa kumfikisha katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi anakoendelea na matibabu.
“Nilipigiwa simu usiku muda wa saa sita nikaambiwa niende nyumbani alipokuwa anafanya kazi mdogo wangu kuwa ameunguzwa na moto, nilipofika nikamkuta kweli ameunguzwa nikamchukua na kumpeleka kwenye zahanati ya Nyanza kutokana na majeraha aliyokuwa nayo walishindwa kumtibu wakatupa rufaa ya kwenda hospitali ya Wilaya ya Misungwi,” amesema Semando.
Semando ameongeza kuwa aliambiwa mdogo wake ameunguzwa baada ya kubainika kuiba Sh160, 000, fedha za mwajiri wake.
Hata hivyo, Felister Semando ambaye ni shangazi wa majeruhi amesema licha ya binti yake kubainika kufanya kosa la wizi hakutakiwa kuunguzwa bali kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria na kuwa kitendo alichofanyiwa ni unyanyasaji ambao mtuhumiwa anatakiwa kuadhibiwa.
Soma zaidi:Makamba: Safari za Rais Samia zina uhusiano na ustawi wa wananchi
“Baada ya kufika hospitali nilikuta kweli ameunguzwa sehemu za mikono, matiti, tumboni na kwenye mapaja…Kitendo alichofanyiwa binti yangu ni cha kikatili tunaomba sheria ifuate mkondo wake,” amesema Semando.
Kwa mujibu wa Semando binti huyo yupo chini ya uangalizi wa madaktari akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake bado haijaimarika.
Juni 5, 2024 Jeshi la Polisi mkoani Mwanza lilitoa taarifa kwa vyombo kwa habari kuwa linamshikilia mtu mmoja Christina Shiriri maarufu kwa jina la Manka mwenye umri wa miaka 43 kwa kosa la kumfanyia ukatili mfanyakazi wake wa ndani Grace Joseph (17) kwa kumwagia mafuta ya taa mwilini kisha kumchoma moto akimtuhumu kuiba kiasi cha Sh161,000.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, Mtuhumiwa alidai kuibiwa fedha zake alizokuwa amehifadhi chumbani kwake na baada ya kumuuliza msichana wake wa kazi alikiri kuzichukua lakini alizirejesha.
“Baada ya kurejeshewa fedha hizo, Christina aliamua kumfanyia ukatili msichana huyo kwa kumchoma moto sehemu za mikono, tumbo na kwenye mapaja yote mawili,” amesema Mutafungwa.
Kwa mujibu wa Mutafungwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea ambapo ametoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi pindi wanapowatuhumu watu wanaofanya makosa badala yake wawafikishe kwenye vyombo vya sheria.
Latest