Polisi mbaroni kumvunja raia mguu kisa mapenzi

January 10, 2023 7:10 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Anadaiwa kuwa mkuu wa kituo kidogo cha polisi Kiseke mkoani Mwanza.
  • Wivu wa mapenzi wasababisha miguu ya Mohamed Khatibu kuvunjwa.
  • Viongozi wa dini, wananchi wakemea kitendo hicho. 

Mwanza. Januari 3 mwaka huu majira ya saa 5:00 asubuhi ni siku ambayo haitasahaulika kwa Mohamed Khatibu, mkazi wa Mtaa wa Kirumba jijini Mwanza baada ya kushambuliwa kwa kipigo na mkuu wa kituo kidogo cha polisi Kiseke kwa madai ya kutoka kimapenzi na mzazi mwenzie.

Ni tukio lililomfanya akatishe mwendo kwa kuvunjwa miguu na kusababisha majeraha kwenye uti wa mgongo kama ilivyothibitishwa na vipimo alivyofanyiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.

Khatibu (29) anasema alichukuliwa nyumbani kwao na watu wanadaiwa kuwa ni polisi wakamfunga pingu kisha kumpeleka kwenye gari wakimtaka kwenda kituo cha polisi.

“Cha kushangaza sikupelekwa kwenye kituo cha polisi Kirumba badala yake walinipeleka kituo kidogo cha polisi Kiseke, nikiwa njiani mmoja kati ya hao akaanza kunipiga na virungu kwenye vifundo vya miguu na magoti hadi wakavunja vikombe vya magoti,” anasema Khatibu.

Mbali na kumpatia kipigo hicho pia anadai walimfunga kitambaa chekundu usoni kisha wakamhamishia kwenye kituo kingine cha polisi cha Buswelu.

Sababu ya kupatiwa vipigo hivyo

Mwanzoni mwa Disemba mwaka jana, safari ya mapenzi kati ya Khatibu na Dorine ilianza. Wakiwa katikati ya huba zito, Khatibu alimhoji iwapo mwanamke huyo kaolewa na kupatiwa jibu la kuwa alizaa na askari mmoja kisha wakaachana.

Penzi lao kabla hata ya kumaliza mwezi, tayari Khatibu yupo kitandani akiuguza majeraha baada ya kupatiwa kipigo alichodai kilitoka kwa askari huyo ambaye ni mzazi mwenzie na rafiki yake huyo mpya.

Khatibu ambaye ni baba wa mtoto moja kwa sasa hawezi kusimama wala kufanya shughuli zake za udalali wa magari kwa kuwa miguu yake miwili imevunjwa kabisa.

Anasema pamoja na kuwa na mawasiliano na mwanamke huyo, wamewahi kukutana mara mbili lakini kwa kipindi hicho cha wiki tatu walikuwa wakitumiana ujumbe na kuzungumza kwa kirefu zaidi hadi saa saba usiku.

Mohamed Khatibu akiwa akiwa kindani baada ya kudai kupigwa na polisi na kusababisha kuvunjwa miguu kwa wivu wa mapenzi. Picha | Mariam John.

“Siku ya Disemba 25 nilikutana na mwanamke huyo na kunieleza kuwa Disemba 31 ni siku yake ya kuzaliwa baada ya mazungumzo waliachana na kuahidiana kukutana siku hiyo, hata hivyo haikuwezekana kutokana na shughuli zake hivyo kulazimika kumpigia simu kumtakia heri kwenye siku yake hiyo mpya,” amesema Khatibu

Baada ya kumpigia simu Dorine ilipokelewa na mwanaume kisha ikakatika na siku mbili baada ya tukio hilo hawakuweza kuwasiliana hadi alipokuja kukamatwa akiwa amelala nyumbani kwao kisha kupelekwa kituoni kupatiwa vipigo hivyo.

“Hawakunikamata kama mtuhumiwa na sikuweza kuona namba za gari na hata waliponifikisha kituoni sikuandikishwa kwenye daftari la watuhumiwa nilipelekwa moja kwa moja selo na kuanza kushushiwa virungu hadi nikashindwa kusimama,” anasema Khatibu.

Kwa sasa haelewi nini hatma ya maisha yake kwa kuwa majibu ya hospitali hawezi kufanyiwa upasuaji miguu ikiwa imevimba badala yake wanasubiri uvimbe upungue na kwamba gharama ya matibabu ya miguu yote ni Sh640,000.

Nini anachojutia

Siyo tu amewachukia wanawake, Khatibu pia anajutia kwanini alichukua mawasiliano ya mwanamke huyo. 

“Sikuwahi kupafahamu nyumbani kwa huyo mwanamke na hata kutana yetu haikuwa ya mara kwa mara ingawa yeye nahisi alikuwaga anapajua nyumbani,” anasema Khatibu.

Hata hivyo, anaomba sheria ichukue mkondo wake hasa kwa askari wanaotumia vibaya vyeo walivyonavyo.


Soma zaidi:


Mama mzazi azungumza

Akizungumza na Nukta habari (www.nukta.co.tz), mama mzazi wa Khatibu, Hidaya Somba amesema kijana ambaye ni mtoto wa pili kati ya nane alionao anakumbuka siku hiyo aliondoka mapema nyumbani kuelekea kwenye shughuli zake na kumwachia hela ya kujaza umeme.

“Nikiwa kazini nilipigiwa simu na binti yangu Saida kuwa kuna watu wamefika nyumbani kwa fujo na kumkamata Mohamed baada ya taarifa hizo nilianza ufuatiliaji nikianza na kituo cha polisi Kirumba ambapo sijamkuta kisha nikaelekea Kiseke,” anasema Hidaya.

Wakiwa Kiseke waliomba daftari la kuandikisha watuhumiwa lakini hakukuwa na mtuhumiwa mpya ndipo wakaelekea Buswelu ambapo pia hakuwa ameandikishwa kwenye kitabu.

“Ilinilazimu kuwaomba wale watu wa mapokezi wanisaidie kumwangalia lakini hawakutaka kunipa ushirikiano hadi pale nilipoanzisha vurugu ndipo wakakubali kuwa yuko hapo na alipelekwa na mkuu wa kituo kidogo cha polisi anayejulikana kwa jina la Paulo,” anasema Hidaya.

Kwa mujibu wa Hidaya, baada ya kuelezwa yuko hapo alipiga simu kituo cha polisi Ilemela kueleza shida hiyo ambapo alitakiwa kuwa mpole na aende kituoni hapo kwa kuwa suala hilo wanalishughulikia.

Aliongozana na watu aliokuwa nao kwenda kituoni na majira ya saa 3 usiku waliona gari likija kituoni hapo kisha wakamshusha kijana huyo akiwa amepigwa na hawezi kutembea.

Anasema walipouliza kuhusu suala la matibabu, mkuu huyo wa polisi alisema kwa kuwa wamempata mtoto wao wamchukue kwenda kumtibia.

Anasema msaada waliopewa kituoni hapo ni kupewa gari la kumpeleka hospitali ambapo baada ya vipimo ilibainika kuwa amepigwa na kusababisha vikombe vya miguu kuvunjika na kutakiwa kwenda Bugando kwa ajili ya matibabu.

Wananchi nao watoa ya moyoni

Baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza, wamelaani tukio hilo na kuomba haki ipatikane kwa mtu aliyetendewa kitendo hicho.

Zabron Mhoja ni mkazi wa eneo la Kirumba amesema kitendo kilichofanywa askari huyo ni kinyume cha haki za binadamu kwa sababu amejichukulia sheria mkononi.

“Ni Jirani yangu hakupaswa kutendewa kitendo hicho, kama suala lilikua ni kutoka kimapenzi na mzazi mwenzie wangesuluhisha kwa namna nyingine lakini si kumsababishia ulemevu.

Amesema wanaamini polisi ni walinzi wa raia ana mali zao lakini cha kushangaza wao ndiyo wa kwanza kuvunja sheria.

“Kwa kweli jambo hili halikubaliki litasababisha kuleta uhasama kati ya raia na polisi, hivyo ni vyema hatua zikachukuliwa ili kuepusha sintofahamu hiyo,” anasema Lucia Kaloli.


Tangazo: 


Kauli za viongozi wa dini

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke analaani kitendo kilichofanywa na askari huyo na kueleza kuwa linaweza kuvunja amani na kusababisha makundi kwenye jamii.

Anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakipambana kurejesha amani ndani ya nchi na kuondoa uwoga uliokuwepo kati ya polisi na wananchi.

“Zamani polisi na wananchi hawakuwa wanapatana kila mmoja alimuona mwenzake kama adui jambo lililosababisha wananchi kuficha siri nyingi za uhalifu kwa kuwa waliamini hata kama polisi wakipewa habari hizo hakuna atakayezifuatilia na kwa kitendo hiki kinaweza kurudisha hiyo sintofahamu,” anasisitiza Sheikh Kabeke.

Shekh Kabeke ameliomba Jeshi la Polisi kuwawajibisha askari wao wanaoenda kinyume cha sheria ili kurejesha amani iliyokuwepo.

 

Zege halilali

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia anayedaiwa kuwa Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Kiseke aliyefahamika kwa jina moja la Paulo baada ya kudaiwa kumpiga na kumvunja miguu Khatibu kwa ajili ya uchunguzi. 

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya anasema wanaendelea kufanya uchunguzi ambapo kwa taarifa zilizowasilishwa ni kuwa Khatibu alipigwa kwa madai ya kutoka kimaenzi na mzazi mwenzie na mkuu huyo wa polisi.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV