Ashikiliwa na polisi kwa kumtorosha mtoto kunusuru ndoa yake
- Ni Rise Joshua mkazi wa Mwanza aliyemtorosha mtoto wa mwenzake hadi Kigoma.
- Amefanya hivyo baada kukosa mtoto kwa muda mrefu katika ndoa yake.
- Anashikiliwa na Jeshi la Polisi na atafikishwa mahakamani.
Dar es Salaam. Jeshi la polisi mkoani Mwanza linamshikilia Rise Joshua (27) mkazi wa Buhongwa kwa kosa la kumuiba mtoto wa miaka miwili na kumtorosha hadi mkoani Kigoma ili kunusuru ndoa yake.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadan Ng’anzi amesema tukio hilo limetokea Desemba 19 mwaka huu maeneo ya soko la Machinga, Kata ya Buhongwa jijini Mwanza baada ya mtuhumiwa kutengeneza mazoea ya karibu na mama wa Stella Damas (22) mfanyabiashara mdogo anayefanya shughuli zake eneo la Buhongwa.
Kamanda Ng’anzi amesema mtuhumiwa alimuomba Stella amsaidie kumbeba mtoto wakati akiendelea na shughuli zake za biashara kisha kutoweka na mtoto kusikojulikana.
“Baada ya kitendo hicho, mama wa mtoto alitoa taarifa polisi ndipo ufuatiliaji wa haraka ulifanyika kwa kushirikiana na polisi Mkoa wa Kigoma na baadaye mtuhumiwa alikamatwa mkoani Kigoma na kumuokoa mtoto akiwa hai na afya njema,” amesema Ng ‘anzi.
Uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa alifanya uhalifu huo ili kunusuru ndoa yake baada ya kukosa mtoto kwa muda mrefu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa wazazi/walezi kuacha tabia ya kuwa na mazoea na watu wasiowafahamu ili kuepusha uhalifu wa aina hiyo.
Pia linaendelea kuwasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi lao ili liendelee kudhibiti uhalifu na wahalifu katika maeneo yote.
Soma zaidi
- Zawadi zinazowafaa wanawake sikukuu ya wapendanao
- Zawadi za kielektroniki unazoweza kumpatia umpendae msimu wa sikukuu
- Zawadi unazoweza kuwanunulia wazazi msimu wa sikukuu
Wakati huo huo katika kuelekea sikukuu ya mwaka mpya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa wito kwa wananchi kusheherekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu katika maeneo yao na kuwasihi wasije wakajihusisha na vitendo vya kiuhalifu na kwa yeyote atakayethubutu atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Sambamba na hilo askari wataendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya Jiji na Mkoa wa Mwanza kwa kufanya doria za miguu, magari, pikipiki na mbwa.
Pia kwenye fukwe za Ziwa Victoria, askari wa kikosi cha Polisi wanamaji wataendelea kufanya doria maeneo yote na kutoa elimu ya ulinzi shirikishi na askari wa usalama barabarani wataendelea kupangwa maeneo muhimu na kuhakikisha ajali hazitokei.
Jeshi la polisi limepiga marufuku wananchi kuchoma matairi barabarani, kurusha mawe na kupiga fataki bila kibali na kwa yeyote anayetaka kupiga fataki aombe kibali kwa Mkuu wa Polisi Wilaya husika (OCD) na kwa yeyote atakaekwenda kinyume, hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Hata hivyo, jeshi hilo limewashukuru wananchi wote wa Jiji na Mkoa wa Mwanza kwa kusheherekea sikukuu za Krismasi na Boxing Day (siku ya kupeana zawadi) katika hali ya utulivu na amani.
“Katika kipindi chote hicho kwa ujumla hali ilikua shwari wananchi walikwenda kwenye Mkesha na Ibada ya Krismas bila kupata tukio lolote la kihalifu, makanisa yote yalipewa ulinzi,” amesema Kamanda Ng’azi.
Latest
