Namna ya kupambana na habari za uzushi TikTok
- Ni pamoja na kuepuka kusambaza video kwa watu wengine kabla ya kuzithibitisha.
- Pia angalia kama chanzo kilichotoa ujumbe ni cha kweli na kina dhamira njema kuhusu wagonjwa wa Corona.
Dar es salaam. Huenda wewe ni mtumiaji wa mtandao wa TikTok ambao unahusika zaidi na maudhui ya video, fahamu kuwa unahitaji kuongeza umakini ili kukabiliana na uzushi wa baadhi ya watu wanaotumia mtandao huo.
Uzushi huo ni ule wa kutengeneza video zisizo za kweli hasa zinazohusu ugonjwa wa Corona.
Kutokana na umuhimu wa mtandao huo ambao una watumiaji zaidi ya milioni 700, baadhi ya taasisi zinazohusika na afya likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) zina akaunti kwa ajili ya kutoa taarifa sahihi.
Licha ya kuwa TikTok kuwa na sera na sheria za kudhibiti habari za uzushi kuhusu Corona kama ilivyo kwa mitandao mingine kama Facebook na Twitter, bado watu wenye nia ovu wanautumia video kupotosha watu .
Ufanye nini kubaini habari au video inayopotosha wakati unatumia mtandao huo wa kijamii? Dondoo hizi zitakusaidia kukuweka salama wewe na jamii inayokuzunguka:
Jambo la kwanza la msingi ni kuangalia chanzo cha habari husika. Katika hatua hiyo mtazamaji anatakiwa kufamu aliyeweka ujumbe ni mtu wa kuaminika na ujumbe uliowekwa hauna mashaka yoyote?
Hii itakusaidia kuepuka kutumia habari isiyo sahihi hasa hizi ambazo hazitolewi na taasisi za afya au zile zilizoidhinishwa kwa ajili ya kusimamia janga la Corona.
Sehemu nyingine ya kutilia mashaka ni kwenye tarehe ambapo jambo la msingi ni kuangalia tarehe ambayo video ilipotengezwa au kuchapishwa kwa mara ya kwanza halafu linganisha na tarehe ambayo muhusika ametumia kwenye Tiktok.
Dondoo nyingine muhimu ni kuangalia baadhi ya alama zilizopo kwenye video husika kama zinashabiana na eneo au tukio halisi linalozungumziwa. Kuna alama yoyote inayotambulisha eneo husika?
Zinazohusiana
Mfano, video inaonyesha watu wakipata chanjo kwenye moja ya viwanja vya mpira wa miguu nchini Kenya lakini, mtengeneza maudhui anasema ni Tanzania.
Kama una mashaka na tukio au eneo husika, ni vema kutumia zana za kidijitali ikiwemo Google Map kupata matokeo ya eneo linalozungumziwa. Hii itakusaidia kung’amua kama habari ni ya kweli au uongo.
Pia jambo lingine la msingi na ambalo ni gumu zaidi kuligundua ni dhamira ya aliyetengeneza habari ya uzushi. Kila video inayowekwa kwenye mtandao huo inakua na dhamira fulani.
Kabla ya kusambaza kwa wengine au kufanya maamuzi ya video husika, jaribu kung’amua aliyechapisha anakusudia nini? Baadhi ya video zinamtaka mtu kuisambaza kwa watu wengi tena kwa amri na kwamba usipofanya hivyo utapata madhara. Video za namna hii siyo za kuziwekea uzito kwa sababu kila mtu ana uhuru wake.
Hivyo wakati huu wa janga la corona watumiaji wote wa TikTok wanatakiwa kuwa makini na kila habari wanayoipokea kabla yakuisambaza kwa wengine.
Latest
