Mwanza kuchanja watu milioni 1.8 ifikapo Desemba?

October 19, 2022 8:05 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa akizungumza na waandishi wa habari namna ya utoaji wa taarifa za Uviko-19 yaliyofanyika jijjni Mwanza Picha | Mariam John.


  • Mpaka sasa imefanikiwa kuchanja watu milioni 1.6.
  • Hiyo ni sawa na asilimia 87 ya lengo.
  • Waandishi wa habari washirikisha kuongeza hamasa ya chanjo.

Mwanza. Huenda Mkoa wa Mwanza ukavuka lengo lake la kuchanja chanjo ya Uviko-19 kwa watu milioni 1.8 ifikapo Desemba 2022 baada ya kuongeza kasi ya utoaji wa kinga ya ugonjwa huo.

Hadi kufikia Oktoba 17, 2022 mkoa huo ulikuwa umechanja watu milioni 1.6 sawa na asilimia 87 ya lengo ambapo imebakiza watu 200,000 kufikia lengo hilo.  

Akizungumza kwenye warsha iliyokutanisha waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza namna ya kuandika kwa weledi habari za Uviko-19, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk Thomas Rutachunzibwa amesema mafanikio hayo yanatokana na taarifa na elimu inayotolewa na vyombo vya habari.

“Tofauti na kapindi ambacho tulianza kutoa chanjo kwa wananchi, hivi sasa kumekuwa na uelewa wa kutosha kwa jamii,  hakuna dhana potofu kuwa chanjo zinapunguza nguvu za kiume, ugumba, kuwa zombi  na mambo mengine hivi sasa wananchi wanaenda kuchanja wenyewe,” amesema Dk Rutachunzibwa. 

Dr Rutachunzibwa amesema kukiwa na jamii iliyochanjwa ni salama si rahisi virusi vya magonjwa kusambaa.

“Udhibiti wa magonjwa ni kama vita, hivyo tunalazimika kutumia silaha mbalimbali za kujikinga na magonjwa ili yasisambae kwenye jamii.

“Hivyo, Serikali pamoja na waandishi wa habari wana wajibu  kuhakikisha jamii inapata uelewa ili kufikia lengo la kuwapata watu laki mbili ambao wamebaki kufikia lengo la kuchanja watu 1.8 milioni,” amesema Dk Rutachunzibwa.

Ametoa rai kwa wananchi kutobweteka kuwa uviko-19 umeisha na kwamba bado upo ingawa umeshuka hivyo ni vyema kuendelea kuchukua tahadhari.

Tanzania inakusudia kuchanja asilimia 70 ya watu wenye sifa ya kupata chanjo hiyo ifikapo Desemba. Hata hivyo, tayari zaidi ya asilimia 60 ya watu wameshachanjwa. 

Wilaya inayoongoza kutoa chanjo mkoani humo ni Ukerewe ambayo imechanja asilimia 89.4 huku wilaya ya mwisho ikiwa ni Misungwi ambayo imechanja kwa asilimia 74.3.

Mafanikio ya kuchanja idadi hiyo ni kutumia vyombo vya habari ikiwemo kutengeneza vipindi maalum vya kuhamasisha utoaji wa chanjo.

“Ushirikishwaji wa viongozi wa serikali za mtaa pia umechangia kusaidia wananchi kujitokeza kwenda kuchanja,” amesema Mratibu wa elimu ya afya kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa  Mwanza, Renard Mlyakado.

Ametaja idadi ya waliojitokeza zaidi kuchanja ni wanawake wakiwemo wajawazito.

Awali Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza (mpc) Edwin Soko amesema lengo la semina hiyo ni kuwaelimisha waandishi waweze kuandika habari kwa weledi hususan habari za takwimu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW