Mwanza ilivyojipanga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel wa kwanza kulia akionyeshwa mchoro wa mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba. Chanzo hicho kitagharimu zaidi ya Sh69 bilioni hadi kukamilika kwake. Picha| Mariam John.
- Inakusudia kujenga mitambo minne ya kuzalisha maji safi.
- Itakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 160 kwa siku.
- Kwa sasa mkoa huo unazalisha lita milioni 70 kwa siku.
Mwanza. Wananchi wanaokaa pembezoni mwa mkoani Mwanza wanatarajia kuondokana na tatizo la upatikanaji wa maji ikiwa chanzo kipya cha maji cha Butimba kinachojengwa sasa kitakamilika kwa wakati.
Chanzo hicho kinagharimu Sh69 bilioni kinatarajiwa kukamilika mwaka 2023.
Kukamilika kwa chanzo hicho kitasaidia kusambaza maji kwenye maeneo yaliyokuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji yakiwemo maeneo ya Usagara, Kisesa na maeneo yenye miinuko.
Akizungumza baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel kutembelea ujenzi wa chanzo hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele amesema hadi kufikia 2023 mkandarasi atakuwa amekamilisha na kukabidhi mradi.
Mhandisi Msenyele amesema hivi sasa wanatoa maji kwa mgao kutokana na chanzo kilichopo cha Capripoint kutotosheleza mahitaji kwa wananchi wa Mwanza.
“Hivi sasa mahitaji kwa wananchi ni milioni 160, uzalishaji ni lita milioni 90, ili kutosheleza mahitaji hayo kwa siku zinapungua lita milioni 70 ndiyo maana tunafanya mgawo ili kila mtu apate,” amesema Mhandisi Msenyele.
Amesema chanzo hicho cha maji cha Butimba kina laini (mitambo) minne ya kuzalisha maji ambapo kila mtambo una uwezo wa kuzalisha lita za maji millioni 40 hivyo kufanya jumla ya kuzalisha lita za maji milioni 160 na kutokana na ufinyu wa fedha wameanza na mtambo mmoja ambao ujenzi wake unaendelea.
Soma zaidi:
Kwa mujibu Mhandisi Msenyele, hivi sasa fedha iliyopo inatosheleza kujenga laini ya kwanza yenye jumla ya lita milioni 40 huku lita zingine milioni 120 zitajengwa baada ya fedha kupatikana.
“Kazi ya kujenga laini hizo imeshaanza toka mwaka 2021 na atatekeleza kwa miezi 24 na katika mradi huo mkandarasi atafanya kazi ya kusanifu na kujenga ambapo kwa upande wa kusanifu ameisha kamilisha asilimia 90 na kinachofanyika hivi sasa tunaweka nguvu zaidi kumsukuma ili aweze kumaliza kwa wakati,” amesema Mhandisi Msenyele.
Wananchi wa mkoa huo wametakiwa kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo la maji.
“Tunabakia na uhitaji wa lita milioni 30 ili kupunguza adha hiyo ya upatikanaji wa maji ni hatua nzuri na kipande kidogo kitakachobakia cha mahitaji na jitihada zinazofanywa na Serikali na wataalamu zitasaidia kukamilisha ili kusaidia uwepo wa upatikanaji wa maji ya uhakika,”amesema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Gabriel.
Latest