Kamati yataka chanzo cha maji Butimba kikamilike kwa wakati
- Yaridhishwa na ujenzi wake.
- Mradi huo utakuwa mkombozi kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza.
Mwanza. Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji imewataka watu wote wanaohusika katika kufanya kazi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba watimize wajibu wao ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Kamati imetoa maagizo hayo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 za maji kwa siku.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Almas Maige amesema kuwa maendeleo ya mradi huo ni mazuri na kazi imefanyika na fedha imetumika kama zilivyotakiwa.
“Tumekagua na tumeridhishwa na kazi inayofanyika hapa fedha zinatumika kama vile ambavyo zimekusudiwa. Nataka kusema wote wanaofanya kazi hapa watimize wajibu wao kwani kilio cha Rais Samia ni kumtua mama ndoo kichwani,” ameeleza Maige.
Mwenyekiti huyo amewataka wakandarasi wanaochelewesha miradi kuwa hawana nafasi ya kufanya kazi nchini kwani kuna sheria nzuri inayowabana wanaochelewesha miradi.
“Lakini kama mradi umechelewa zipo sababu ambazo siyo za wakandarasi nasi tumefuatilia na tunajua jambo linalotokea ambalo halihusu pande mbili ambazo zimekubaliana kwenye mkataba mradi huu unaenda vizuri,” amesema Maige.
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Mary Prisca Mahundi ameeleza kuwa mradi huo ni muhimu kwa Mkoa wa Mwanza hivyo wizara imepokea maagizo yote yaliyotolewa na kamati hiyo.
Amesema mradi huo watausimamia kwa ukaribu zaidi tofauti na awali ili kuhakikisha unakamilika mapema lengo lao ni kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa uharaka.
“Kamati hii imekuwa ikitushauri na kufanikiwa sana na hapa Mwanza kwenye huu mradi ni mradi ambao tunautegemea uongeze tija katika kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo haya na tunaendelea kufuatilia kuhakikisha vifaa vinafika ndani ya muda ambao tumekubaliana na hatuwi kikwazo kuona mradi huu unakamilika,” amesema Mahundi.
Ujenzi wa mradi wa maji wa Butimba ukiendelea kujengwa mkoani Mwanza. Picha | Mariam John.
Akitoa taarifa ya Mradi huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele, ameeleza kuwa mradi mzima una njia nne zenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 160 kwa siku.
Amesema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo wameanza na njia moja ambao ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku na umegharimu kiasi cha Sh69 bilioni na kunufaisha wananchi takriban 500,000.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu na mjumbe wa kamati hiyo Emmanuel Cherehani, ameeleza kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wananchi wa Mwanza na ukanda wa Ziwa Victoria hivyo Wizara ya Maji inapaswa kuzingatia ipasavyo mikataba iliyowekwa.
“Mkandarasi asimamiwe fedha za umma ambazo Rais amezitoa ziweze kuwanufaisha wananchi kwa wakati kwa sababu wanauhitaji mkubwa wa huduma ya maji,” ameeleza Cherehani.
Cherehani ameishauri serikali kuwaangalia na kuwapa kipaumbele wakandarasi wa ndani waweze kupewa mikataba ya kandarasi ya miradi mikubwa ya maji, barabara na mingine ili kuendelea kuwajengea uwezo mkubwa badala ya kuendelea kuwapa nafasi wakandarasi kutoka nje ya nchi pekee.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza na upungufu wa maji lita million 70 japokuwa wa miradi ya maji yenye thamani ya Sh300 billioni ikiwemo iliyokamilika pamoja na inayoendelea na utekelezaji malengo yao ni kuhakikisha wanamaliza tatizo la maji.
Latest