Morogoro kufanya maboresho daftari la mpiga kura Machi, 2025

February 18, 2025 3:37 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kuanzia Machi Mosi hadi 7, 2025 
  • Jumla ya wapiga kura wapya  302,752 wanatarajiwa kuandikishwa.

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanza kwa mzunguko wa 12 wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Morogoro na sehemu ya mkoa wa Tanga kwa siku saba kuanzia Machi Mosi mpaka 07, 2025.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele aliyekuwa akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Morogoro Februari 17, 2025, amesema uboreshaji huo utafanyika kwenye mkoa huo na mkoani Tanga kwenye halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga.

“Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 12 kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu wa 12 unahusisha Mkoa huu wa Morogoro na Mkoa wa Tanga katika Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga,” amesema Jaji Mwambegele.

Jaji Mwambegele amesema mikoa 27 tayari imekamilisha zoezi hilo ambayo ni pamoja na Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele akizungumza wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoa wa Morogoro. Picha l Mroki

Ameitaja mikoa mingine kuwa ni Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

“Mikoa miwili ya Pwani na sehemu ya mkoa wa Tanga kwenye Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri za Miji ya Handeni na Korogwe na Halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Lushoto na Muheza inatarajia kukamilisha zoezi hilo tarehe 19 Februari, 2025,” amebainisha Jaji Mwambegele.

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Kailima Ramadhani amesema Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 302,752 mkoani Morogoro sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 1,612,952 waliokuwepo kwenye daftari la wapiga kura mwaka 2020.

“Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Morogoro utakuwa na wapiga kura 1,915,704. Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo Watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” amesema.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Morogoro una vituo  2,816 vitakavyotumika kwenye uboreshaji wa daftari ikiwa ni ongezeko la vituo 112 katika vituo  2,704 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV