INEC kuandikisha wapiga kura wapya 400,000 Mwanza, Shinyanga
- Wadau wakosoa kuwa muda uliowekwa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura ni mdogo ikilinganishwa na jiografia ya mikoa hiyo hususan Mwanza.
Mwanza. Wakati Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikipanga kuandikisha zaidi ya watu 400,000 ndani ya siku saba katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga katika zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura, baadhi ya wadau wa demokrasia na wasiasa wamekosoa kuwa muda uliopangwa hautoshelezi kutoa haki kwa kila mtu kujiandikisha.
Katika hatua za uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, INEC inatarajia kuandisha wapiga kura wapya kuanzia tarehe 21 hadi 27 Agosti, 2024 ikiwa ni moja hatua muhimu katika mchakato wa uchaguzi kuhakikisha kila mtu mwenye umri stahiki wa kupiga anapata haki hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya INEC iliyotolewa leo Agosti 9 2024, tume hiyo inatarajia kuandisha jumla ya wapiga kura wapya 400,082 katika mikoa hiyo miwili ya kanda ya ziwa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Kailima Ramadhani amebainisha kuwa wapiga kura wapya 209,951 wataandikishwa mkoani Shinyanga huku Mwanza ikitarajiwa kuwa na wapiga wapya 190,131.
Kwa mujibu wa Kailima, wapiga kura hao wapya mkoani Mwanza ni sawa na ongezeko la asilimia 10.3 ya wapiga kura 1,845,816 waliopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kufanya mkoa huo kuwa na jumla ya wapiga kura 2,035,947.

Baadhi ya wadau jijini Mwanza wakishiriki uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura mkoani Mwanza. Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika katika kipindi cha siku saba kuanzia Agosti 21-27 2024. Picha na Mariam John/Nukta.
“Kwa mkoa wa Shinyanga tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 209,951. Hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 ya wapiga kura 995,918 waliopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,” amesema Kailima.
INEC ilifanya mikutano na wadau wa uchaguzi leo Mwanza na Shinyanga ili kuhamasisha wapiga kura kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili zoezi lifanyike kwa ufanisi.
Mkoani Mwanza mkutano wa wadau umefunguliwa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele na mkoani Shinyanga mkutano umefunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa tume Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk.
Siku ziongezwe
Hata hivyo, baadhi ya wadau wamekosoa muda uliopangwa kufanya uboreshaji wa daftari hilo katika mikoa hiyo miwili wakieleza hautatosha kuwapatia fursa watu wengi kujikiandikisha kupiga kura hasa waishio visiwani kama Mwanza hivyo ni vema tume ikaongeza siku.
Mwanaharaki wa kutetea wanawake katika wilaya ya Ukerewe Sophia Dolnad amesema kutokana na wilaya hiyo kuwa na idadi kubwa ya visiwa vinavyokaliwa na watu ni dhahiri kuwa uboreshaji hautawafikia watu wote hususani wanawake wajasiriamali.
“Kama tunavyofahamu ukerewe ina zaidi ya visiwa 30 na vinavyokaliwa na watu ni 15 hivyo kutoka kisiwa kimoja na kingine ni zaidi ya masaa saba changamoto ni namna ya kuwapata hao watu hususani wanawake ambao wengine ni wajasiriamali,” amesema Sophia
Amesema wasiwasi mwingine ni kwamba wapo watu ambao ni wa kuhama hama na hii ni kutokana na biashara inayofanyika visiwani ambapo mtu hakai kwenye kisiwa kimoja.
Abas Mayalla, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) amesema mbali na kutoridhishwa na idadi ya siku zilizotolewa lakini pia bado kuna changamoto ya upungufu wa vitendea kazi.
Latest