INEC yasisitiza kuzingatia sheria, maadili uandikishaji daftari la kudumu la  wapiga kura 

April 29, 2025 7:46 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Tume imewataka watoa huduma kutumia lugha za staha hata pale mmoja ya wahudumiwa anapokosea.
  • Ni kwanzia Mei 1 mpaka Julai 4 mwaka huu 2025.

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga Kura kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maadili ya uchaguzi wakati wa awamu ya pili ya zoezi hilo, ambalo linaanza Mei 1, 2025 katika mikoa 15 nchini.

Akizungumza leo Aprili 29, 2025 katika mafunzo ya siku moja kwa watendaji wa kata wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, amewataka watendaji hao kuwa wanyenyekevu na kutumia lugha nzuri wakati wa kuwahudumia wananchi.

“Nawakumbusha tena kama nilivyowakumbusha katika zoezi lililopita, kwamba katika utekelezaji wa zoezi hili mzingatie sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, muwe wanyenyekevu kwa wateja mtakao kuwa mnawahudumia,” amesema Jaji Mwambegele.

Tume yawataka watoa huduma kuwahudumia wananchi kwa staha hata yanapotokea makosa. Picha | INEC

Aidha, amebainisha kuwa wengi wa watakaohudumiwa ni wananchi wa kawaida, hivyo ni muhimu kuwahudumia kwa staha hata yanapotokea makosa. 

“Ikiwa kuna ulazima wa kuwarekebisha pale wanapokosea basi wafanye hivyo kwa staha.” amesisitiza Jaji Mwambegele

Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, zoezi la uboreshaji wa daftari linafanyika kwa mujibu wa kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, kinachoipa INEC jukumu la kufanya uboreshaji huo mara mbili kati ya chaguzi kuu.

Awamu ya pili ya uboreshaji itaenda sambamba na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura, kuanzia Mei 1 hadi Julai 4, 2025 huku zoezi hilo likiwa limegawanywa katika mizunguko mitatu.

Mikoa itakayohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji ni pamoja na Iringa, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 1 hadi 7, 2025.

Vituo 7,869 vitahusika kwenye zoezi hili, kati ya hivyo, 7,659 vikiwa Tanzania Bara na 210 visiwani Zanzibar. Picha | INEC.

Mzunguko wa pili utahusisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025.

Mzunguko wa tatu wa zoezi la uboreshaji wa daftari utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye magereza ya Tanzania Bara na vituo 10 vilivyopo katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Juni 28 hadi Julai 04, 2025.

Kwa ujumla, vituo 7,869 vitahusika kwenye zoezi hili, kati ya hivyo, 7,659 vikiwa Tanzania Bara na 210 visiwani Zanzibar.

Takwimu za INEC zinaonyesha kuwa wapiga kura wapya 1,396,609 wanatarajiwa kuandikishwa, huku 1,092,383 wakiboresha taarifa zao na 148,624 wakiondolewa kwa sababu mbalimbali zikiwemo vifo au kukosa sifa za kisheria.

Mwenyekiti wa INEC amefafanua kuwa, mabadiliko mengine ni pamoja na kuhamisha taarifa za wapiga kura waliobadili kata au jimbo walipoandikishwa awali, pamoja na kushughulikia taarifa za wale waliopoteza sifa kwa mujibu wa sheria.

INEC ilikamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kati ya Julai 20, 2024 hadi Machi 25, 2025. Picha | INEC.

Aidha, kwa kuzingatia kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria hiyo, tume pia italiweka wazi daftari la awali la wapiga kura kwa ajili ya wananchi kuangalia, kufanya marekebisho na kuweka pingamizi dhidi ya wapiga kura wasio na sifa.

Daftari hilo litabandikwa kwenye vituo vyote vilivyotumika wakati wa awamu ya kwanza.

INEC ilikamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kati ya Julai 20, 2024 hadi Machi 25, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks