Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili kuanza Mei, 2025

April 14, 2025 6:36 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Zoezi litafanyika mikoa 15 kwa mzunguko wa kwanza wa pili mikoa 16 na wa tatu vituo vya magereza pamoja na vyuo vya mafunzo.
  • Uboreshaji huo unafanyika katika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Tanzania Zanzibar katika vituo 7,869.

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imebainisha kuwa inatarajia kuanza awamu ya pili ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura sambamba na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura kuanzia Mei 1 hadi Julai 4, 2025.

Mwenyekiti wa INEC Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele aliyekuwa akizungumza na wanahabari  leo Aprili 14, 2025 jijini Dodoma amebainisha kuwa kuwa zoezi hilo litafanyika kwa mizunguko mitatu ambapo mzunguko wa kwanza unahusisha mikoa 15 wa pili mikoa 16 na wa tatu vituo vya magereza pamoja na vyuo vya mafunzo.

Katika mzunguko wa kwanza Jaji Mwambegele amesema uboreshaji utafanyika kati ya Mei 1 hadi 7, 2025 katika mikoa ya Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe.

Bosi huyo wa INEC ameongeza kuwa mzunguko wa pili utahusisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba, kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025.

Uandikishaji huo utawapa fursa wananchi waliokosa nafasi za kujiandikisha awali na kuboresha taarifa zao. Picha/ Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Aidha, mzunguko wa tatu utafanyika kati ya Juni 28 hadi Julai 4, 2025 katika vituo 130 vya magereza Tanzania Bara na vituo 10 vya Vyuo vya Mafunzo Zanzibar.

Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, uboreshaji huo unafanyika katika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Tanzania Zanzibar huku ukihusisha jumla ya vituo 7,869 kati ya hivyo 7,659 vipo Tanzania Bara na 210 Zanzibar.

“Tunatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 1,396,609, kuboresha taarifa za wapiga kura 1,092,383, na kufuta wapiga kura 148,624 waliopoteza sifa,” amesema Jaji Mwambegele.

Aidha, amefafanua kuwa kazi hii inatekelezwa kwa mujibu wa kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 kinachoipa Tume mamlaka ya kuboresha daftari hilo mara mbili kati ya chaguzi kuu.

Sanjari na hilo zoezi hili linajumuisha kuandikisha raia wa Tanzania waliofikisha au watakaofikisha umri wa miaka 18 ifikapo siku ya uchaguzi mkuu wa 2025, kutoa kadi mpya kwa waliopoteza au kadi zilizoharibika, na kurekebisha taarifa za wapiga kura waliopo ikiwemo majina na taarifa nyingine.

Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili unatarajiwa kufanyika Mei 1, 2025 na kukamilika Julai 4 2025. Picha/ Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Jaji Mwambegele ameongeza kuwa mchakato mwingine utakaofanyika ni pamoja na kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.

Hata hivyo, Mwambegele amesisitiza kuwa sambamba na hilo, INEC inaandaa daftari la awali la wapiga kura na kuliweka wazi kwa umma kama ilivyoelekezwa na kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria hiyo ya mwaka 2024 ikiwa lengo ni kutoa fursa kwa wananchi kukagua na kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa.

Daftari hilo la awali litabandikwa kwenye vituo vyote vilivyotumika wakati wa awamu ya kwanza ya uboreshaji na linawekwa wazi sambamba na uboreshaji wa awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari ilianza Julai 20, 2024 na kukamilika Machi 25, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks