Rais Samia atoa maagizo matatu kwa mawaziri aliowaapisha
Waziri wa Tamisemi, Angellah Jasmine Kairuki, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Innocent Lugha Bashungwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Dk Stergomena Lawrence Tax wakiapa kiapo cha maadili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo. Picha | Ikulu.
- Awataka kutunza siri za Serikali na kufanya kazi kwa mujibu wa mipaka waliyowekewa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo matatu kwa mawaziri walioapishwa ikiwemo kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutunza siri za Serikali wamapotimiza majukumu yao ya kila siku.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Oktoba 3, 2022 baada ya kuwaapisha mawaziri watatu aliowateua jana akiwemo Innocent Bashungwa aliyehamishiwa Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa akitokea Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Angellah Kairuki ambaye ameteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania na Waziri wa Tamisemi.
Mwingine ni Dk Stergomena Tax aliyehamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitokea Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa.
Dk Tax anachukua nafasi ya Balozi Liberata Mulamula ambaye uteuzi wake ulitenguliwa jana.
Agizo la kwanza kwa mawaziri hao ni kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba na lazima utekelezaji wa majukumu yao uendane na pande mbili za muungano.
“Mnapoapa hapa kile kiapo kinakuwa ni cha kweli na mnaposema mtaheshimu, mtailinda na kuitetea ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muungano wenye pande mbili na mtatumika sehemu zote sawa,”
Amewataka mawaziri hao kuzingatia na kutambua ukomo wa mamlaka waliyopewa pale wanapotimiza majukumu yao hivyo wanapotaka kufanya jambo lililo nje ya ukomo wao ni lazima wapate ruhusa kutoka mamlaka ya juu.
Agizo la tatu alilolitoa Rais Samia ni utunzaji wa siri na namna ya kuwasilisha maamuzi ya Serikali katika utekelezaji na kusisitiza kuwa wao ni sehemu ya maamuzi ya Serikali.
“Linaloamuliwa na Serikali wewe kama waziri ni lako ni lazima ulibebe ukalifanyie kazi kwa misingi uliyoelekezwa huwezi kusema nimeelekezwa hivi, mimi sikutaka hivi lakini imebidi nifanye hivi kwa sababu nimeelekezwa, huwezi kujitoa,” amesema Rais.
Mabadiliko hayo madogo kwenye Baraza la Mawaziri ni ya tatu kwa Rais Samia tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021.