Bei za petroli, dizeli zashuka Tanzania

September 4, 2024 1:17 am · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya reja reja ya petroli kwa lita yashuka kwa Sh91, dizeli yashuka kwa Sh120 na mafuta ya taa kwa Sh136.
  • Ahueni hiyo inatokakana na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kwa wastani (weighted average).

Dar es Salaam. Maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto nchini yatapungua kidogo mwezi Septemba mara baada ya bei ya mafuta ya petroli na dizeli kushuka kutokana na kupungua kwa gharama za uagizaji na wastani wa gharama ya kubadili viwango vya fedha za kigeni.

Agosti 2024, wamiliki wa vyombo vya moto walilazimika kujifunga mkanda mara baada ya bei ya reja reja ya petroli kuongezeka kwa Sh21 ambapo lita moja iliuzwa Sh3,231 huku dizeli ikiongezeka kwa Sh16 na kuuzwa Sh 3,131 kwa lita moja.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) leo Septemba 4, 2024 inaeleza kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa Sh91 ambapo lita moja sasa inauzwa Sh3,140.

Bei rejareja ya dizeli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam nayo imeshuka kwa Sh120 ambapo sasa lita moja inauzwa Sh3,011.

Mafuta ya taa Dar es Salaam yameshuka kwa Sh156 ambapo sasa yanauzwa Sh3,121 kutoka Sh3,257 iliyorekodiwa mwezi Agosti.

Kwa upande wa mafuta yanayoingizwa kupitia Bandari ya Tanga  lita moja ya petroli itanunuliwa kwa Sh3,141 kutoka Sh3,229 ya mwezi uliopita.

Dizeli inayotumika zaidi kwenye mitambo na vyombo vya moto, sasa itanunuliwa kwa Sh3,020 kwa lita kutoka Sh3,138 na mafuta ya taa kwa Sh3,167 kutoka Sh3,303 iliyokuwepo mwezi Agosti.

Watu wanaotumia mafuta yaliyopitia Bandari ya Mtwara watanunua petroli kwa Sh3,142 kwa lita kutoka Sh3,304 mwezi Agosti 2024, dizeli Sh3,021 kutoka Sh3,140 na mafuta ya taa Sh3,194 kutoka Sh3,329 ya mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa Ewura, kupungua kwa bei za mafuta kwa mwezi Septemba 2024 kunatokana na kushuka kwa bei za mafuta yaliyochakatwa  (FOB) katika soko la dunia kwa wastani (weighted average) kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa.

“Bei kikomo za mafuta zimekokotolewa kwa kuzingatia bei za soko la Uarabuni za mwezi Agosti 2024. Kwa kulinganisha na bei za Julai 2024, bei za Agosti 2024 za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua kwa wastani wa asilimia 7.68, asilimia 6.22 na asilimia 6.20, mtawalia,” imebainisha taarifa ya Ewura.

Hata hivyo, ahueni hiyo katika bei ya mafuta nchini haipunguzi maumivu kwa watumiaji wa nishati hiyo kwa kiasi kikubwa hasa wa kipato kidogo kutokana na kushuka kwa kiwango kidogo. 

Mathalan, mtumiaji aliyekuwa anatumia Sh10,000 kupata lita 3.09 za petroli jijini Dar es Salaam kwa bei mpya iliyotangazwa leo atapata lita 3.18 za mafuta, nafuu ambayo ni kidogo.

Kwa watumiaji wa dizeli hali ni hiyo hiyo kwa bei mpya ya leo ambapo mnunuzi akiwa na  Sh10,000 atapata lita 3.32 kutoka lita 3.18 alizokuwa anapata mwezi Agosti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks