Matumaini mapya: Wateja benki ya FBME waanza kulipwa
- Walipwa malipo ya awali ya Sh2.43 bilioni.
- Benki hiyo ilifilisiwa Mei 2017 kutokana na tuhuma za utakatishaji fedha.
Dar es Salaam. Serikali imewalipa baadhi ya wateja wa iliyokuwa benki ya FBME jumla ya Sh2.43 bilioni ikiwa ni malipo ya awali ya fidia ya bima ya amana, tangu ifilisiwe takriban miaka sita iliyopita.
Malipo hayo yamefanyika kwa wateja 3,446 hadi Machi, 2023.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande amesema kuwa malipo hayo yamefanyika kupitia Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kwa wateja wa benki hiyo waliojitokeza kudai malipo hayo.
Chande alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Chwaka, Makame Mlenge Haji, aliyetaka kujua ni lini Serikali itawalipa waathirika wa benki ya FBME iliyofilisiwa tangu Mei 2017.
“Malipo ya fedha za ufilisi (liquidation proceeds) kwa wateja wenye amana zaidi ya shilingi milioni 1.5 yanayotokana na uuzaji wa mali, makusanyo ya madeni, mikopo na fedha nyingine za benki hiyo yatafanyika ndani ya mwaka huu wa fedha 2022/23,” amesema Chande.
Fedha za ufilisi zitalipwa baada ya mahakama ya nchi ya Cyprus kutoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowekwa na Benki Kuu ya Cyprus la kuitambua DIB kama mfilisi wa benki yote ikijumuisha makao makuu pamoja na tawi la Cyprus (Global liquidator), uamuzi unatarajiwa kutolewa ndani ya mwaka wa fedha 2022/23.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 kifungu cha 39, kifungu kidogo cha II na III, amana au akiba ya wateja katika benki au taasisi ya fedha zina kinga ya bima ya amana kiasi kisichozidi Sh1.5 milioni tu na endapo mteja ana salio la amana isyozidi Sh1.5 milioni atapata fidia ya asilimia 100.
Wateja walio na amana zaidi ya Sh1.5 milioni wanalipwa Sh1.5 milioni kama fidia ya bima ya amana na kiasi kilichobakia kinalipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi.
Zinazohusiana:
- M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni
- Wawekezaji wa Acacia soko la hisa Dar tabasamu tupu
- Maumivu kwa wawekezaji wa kampuni ya bia soko la hisa Dar
Namna FBME ilivyofilisika
Uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuifungia benki hiyo ulitokana na notisi iliyotolewa Julai 15, 2014 na taasisi ya Marekani inayopambana na uhalifu wa kifedha (the US Financial Crimes Enforcement Network(FinCEN)), kuhituhumu FBME kuwa ni taasisi inayojihusisha na biashara ya utakatishaji wa fedha na hatua ya Benki Kuu ya Cyprus kuliweka tawi la FBME lililopo nchini Cyprus chini ya uangalizi maalumu.
FBME walifungua kesi huko Marekani (US District Court for the District of Columbia) wakiiomba mahakama kutengua uamuzi wa FinCEN ambapo April 14 2017 mahakama ilitoa uamuzi ambao uliiruhusu FinCEN kuendelea na utekelezaji wa uamuzi wake wa mwisho (Final Rule) ambao uliifungia benki ya FBME kutumia mfumo wa kibenki wa Marekani.
Uamuzi huo wa mahakama uliongeza athari kwa kiwango kikubwa katika uendeshaji wa FBME kwa kuwa haikuweza tena kufanya miamala ya kibenki ya kimataifa na kupata huduma za mifumo ya kibenki na hivyo kushindwa kutoa huduma muhimu kwa wateja wake kwa mujibu wa leseni waliyopewa.
Hatua hiyo ndiyo iliwezesha BoT kusimamisha shughuli zote za FBME na kufuta leseni yake ya kufanya shughuli za kibenki, kuiweka chini ya ufilisi na kuiteua DIB.
Kabla ya kufungwa, FBME ilikuwa na matawi manne nchini Tanzania huku makao makuu yakiwa jijini Dar es Salaam. Matawi mengine yalikuwa Kiswandui visiwani Zanzibar, barabara ya 47 Old Moshi/Haile Selassie mkoani Arusha na tawi la Mwanza.
Licha ya kuwa na matawi machache benki hiyo ilikuwa inajiweza kimtaji. Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia Septemba 2013, FMBE ilikuwa na mali zenye thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 2.7 sawa na Sh4.4 trilioni.