Necta yatangaza matokeo ya darasa la saba 2022, ufaulu ukishuka kidogo

December 1, 2022 8:53 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ufaulu wa jumla umepungua kwa asilimia 2.3 ukilinganisha na mwaka jana.
  • Idadi ya watahiniwa waliofaulu imeongezeka kwa asilimia 18.24.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2022  huku ufaulu wa jumla ukipungua kwa asilimia 2.3 ikilinganishwa na mwaka jana.

Watahiniwa milioni 1.07  kati ya milioni 1.34 waliofanya mtihani huo wamefaulu sawa na asilimia 79.6.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi akitangaza matokeo hayo leo Desemba 1, 2022 Jijini Dar es Salaam amesema kati ya watahiniwa waliofaulu, wasichana ni 558,825 sawa na asilimia 79.9 ya wasichana waliofanya mtihani huo huku wavulana wakiwa ni 514,577.

“Kitakwimu kuna punguzo la ufaulu kwa asilimia 2.35 japokuwa kwa idadi ya watahiniwa waliofaulu imeongezeka kwa asilimia 18.24,” amesema Dk Amasi. 


Zinazohusiana


Watahiniwa milioni 1.38 wa shule za msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo wakiwemo wasichana 723,027 sawa na asilimia 52.23 ya watahiniwa wote. 

Kati ya watahiniwa waliosajiliwa, watahiniwa wenye mahitaji maalum walikuwa 4,221.

“Watahiniwa milioni 1.35 sawa na asilimia 97.57 ya waliosajiliwa walifanya mtihani. Kati yao wasichana walikuwa 709,556 sawa na asilimia 98.14 na wavulana walikuwa 641,325 sawa na asilimia 97 ya waliosajiliwa” amesema Amasi wakati akitangaza matokeo hayo. 

Watahiniwa 33,305 sawa na asilimia 2.42  hawakufanya mtihani huo uliofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu nchi nzima kutokana na sababu mbalimbal zikiwemo utoro na ugonjwa.

Enable Notifications OK No thanks