NMB yapunguza hewa chafu kwa 7.3% mwaka 2025
- Uzalishaji huo ulipungua kutoka tani 23,822 mwaka 2024 hadi tani 22,075 mwaka 2025, sawa na upungufu wa tani 1,747 za hewa ya ukaa.
Dar es Salaam. Benki ya biashara ya NMB imepunguza uzalishaji wa hewa chafu unaotokana na shughuli zake za ndani kwa asilimia 7.3 mwaka 2025, hatua inayotokana na juhudi za kuboresha matumizi ya nishati na kupunguza athari za kimazingira za uendeshaji wake.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Uendelevu (ESG) ya benki hiyo ya mwaka 2025 iliyozinduliwa leo Novemba 26, 2026 uzalishaji wa hewa chafu ulipungua kutoka tani 23,822 mwaka 2024 hadi tani 22,075 mwaka 2025, sawa na upungufu wa tani 1,747 za hewa ya ukaa.
“Uzalishaji wa moja kwa moja ulipungua kwa asilimia 34, kutoka tani 5,638 hadi tani 3,719, huku ule unaotokana na matumizi ya umeme ukishuka kwa asilimia tatu hadi tani 7,371, imeeleza ripoti hiyo.
Hewa chafu ni gesi zinazotolewa angani kutokana na michakato ya asili au shughuli za kibinadamu kama vile viwanda, matumizi ya nishati isiyo rafiki kwa mazingira kama vile kuni, jenereta au hata vyombo vya usafiri kama vile moshi wa magari na pikipiki.

Kwa NMB kupungua kwa uzalishaji wa hewa chafu kumetokana na kupungua kwa matumizi ya mafuta katika jenereta, magari, pamoja na uzalishaji usio wa moja kwa moja unaotokana na matumizi ya umeme katika matawi, ofisi na vituo vya huduma vya benki hiyo.
Mafanikio hayo yamechangwa na kuweka mifumo ya nishati ya jua yenye uwezo wa kuzalisha Kilowati 229.08 katika makao makuu, pamoja na kuboresha mifumo ya taa katika matawi 248 nchini.
Hewa ukaa yaongezeka duniani
Jitihada za NMB kupunguza uzalishaji wa hewa chafu zinakuja wakati dunia ikiendelea kukabiliwa na ongezeko la gesi chafu katika angahewa, ambazo zinachangia ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi.
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) linaripoti kuwa wastani wa kiwango cha hewa ya ukaa (CO₂) katika angahewa ulifikia sehemu 426.8 kwa kila milioni (ppm) mwaka 2025, kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa.
Kiwango hicho kilichorekodiwa mwaka 2025 ni asilimia 53 zaidi ya kiwango cha kiulichorekodiwa kabla ya mapinduzi ya viwanda.
Hali hii imekuwa ikichangia athari mbalimbali za kimazingira kwa sasa ikiwemo kuongezeka kwa joto duniani, pamoja na mabadiliko ya tabia nchi kama vile ukame na mvua kubwa zisizotabirika.
Ufadhili endelevu waongezeka
Afisa Mkuu wa Fedha na Mkurugenzi Mtendaji wa Fedha wa benki hiyo, Juma Kimori amesema NMB inaongoza uwajibikaji wa kimazingira kwa kujumuisha ufadhili endelevu katika mkakati wake mkuu wa biashara ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa muda mrefu.
“Kupitia nyenzo bunifu za kifedha, ikiwemo hati fungani za uendelevu ambazo NMB imekuwa miongoni mwa taasisi za kwanza kuziorodhesha katika masoko ya London na Luxembourg, tumefanikiwa kukusanya mabilioni ya shilingi kutoka kwa wawekezaji,” amesema Kimori leo Novemba 26, 2026 jijini Dar es Salaam.

Tangu mwaka 2022 benki hiyo imekusanya Sh621 bilioni kupitia ufadhili endelevu, zilizotumika kufadhili miradi ya nishati mbadala, kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, usafiri unaotumia nishati safi, mipango ya kuimarisha usalama wa chakula pamoja na biashara zinazoongozwa na wanawake.
Ripoti inaonesha mikopo ya kijani ilifikia Sh328 bilioni, huku benki ikifadhili miradi ya nishati jadidifu yenye uwezo wa kuzalisha megawati 26.4.
Hata hivyo, uzalishaji wa hewa chafu unaotokana na shughuli za wateja na miradi inayofadhiliwa na benki hiyo ulifikia tani 1.44 milioni za hewa ya ukaa kutoka tani 1.12 milioni mwaka uliotangulia.
Uzalishaji huo hutokana na shughuli za kiuchumi za kampuni na miradi inayofadhiliwa na benki, tofauti na hewa chafu zinazotokana na shughuli zake za ndani.