Mashindano ya baiskeli yanavyowainua wanawake kiuchumi Mwanza
- Ni kupitia fedha wanazopata baada ya kushinda mashindano hayo.
- waiomba Serikali kuboresha miundombinu ili kuvutia washiriki wengi zaidi.
Mwanza. Ni nadra sana kukutana na mwanamke akiendesha baiskeli kuelekea katika shughuli zake za kila siku hususani katika maeneo ya mijini ambako nyenzo za usafiri zimerahisishwa.
Stori ni tofauti katika baadhi ya maeneo ya vijijini, huko mwanamke kuendesha baiskeli si jambo la anasa, bali huchangiwa zaidi na kutokuwepo kwa miundombinu rafiki kuwezesha aina nyingine za usafiri kama magari na pikipiki.
Restuta Nicolaus (44) mkazi wa Kijiji cha Malya Machinjioni wilayani Kwimba mkoani Mwanza, daima hutumia usafiri wa baiskeli kufanya shughuli zake ikiwemo kwenda shambani au kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Umaarufu wake katika matumizi ya baiskeli akiwa amepakia mzigo wa kilogramu 20 unawavuta waandaji wa mashindano ya baiskeli wilayani Malya kumualika mama huyo wa watoto saba kushiriki mbio hizo.
Ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki mbio hizo zilizoandaliwa na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo wilayani Kwimba, Restuta anaibuka mshindi wa pili katika mashindano hayo akipishana kwa sekunde chache na mpinzani wake.
Pamoja na kuwa na ndoto ya kushiriki mashindano hayo ili kuonesha kipaji chake Restuta alihitaji nafasi hiyo ili kupata fedha itakayomsaidia yeye pamoja na familia yake.
“Lengo langu ilikuwa nije kushiriki ili nikishinda nipate hata Sh30,000 kwa ajili ya matumizi ya familia, lakini nimeshika nafasi ya pili na kupata kiwango zaidi ya nilichokitarajia,” amesema Restuta
Kupitia mashindano yaliyofanyika mwishoni mwa juma hili, Restuta na wanawake wengine watano walijitokeza kushiriki mashindano hayo ambapo yeye alifanikiwa kushika nafasi ya pili kwa kutumia muda wa saa 1 na dakika 15 akikimbia umbali wa kilomita 20 na kujinyakulia kitita cha Sh50, 000 pamoja na medali.
Mshindi wa kwanza katika mbio hizo alikuwa ni Veronika Simon mkazi wa Kijiji cha Maswa ambaye alitumia saa 1 na dakika 9 na kujinyakulia kitita cha Sh100, 000 pamoja na medali.
Matarajio yake mbeleni
Restuta anakiri kuitazama fursa ya kukuza uchumi wake kupitia mbio hizo ambapo anasema kuwa iwapo mashindano yatakuwa mengi ana uhakika wa kujikusanyia kipato kitakachotosha kupata mtaji wa biashara ndogo.
Hata hivyo, Umri wake huenda ukawa kikwazo kutimiza hilo kwa kuwa tayari watoto pamoja na mumewe wanadai hawezi kuendelea kutokana na umri wake kuwa mkubwa.
Washiriki wengine wanavyoyatazama mashindano
Veronica Simoni ambaye ni mshindi wa kwanza kwenye mashindano hayo ameiambia Nukta Habari kuwa mashindano hayo ni mazuri ingawa changamoto ya miundombinu ya barabara inatakiwa kufanyiwa kazi ili yawe bora zaidi.
Veronika ameiomba Serikali na wadau wa michezo kuwasaidia kuboresha mchezo wa baiskeli hususan kwenye vifaa bora ikiwemo baiskeli maalum kwa mashindano ili waweze kushiriki vyema mpaka ngazi ya kimataifa.
Asemavyo katibu wa Mbio za baiskeli Mwanza
Fikiri Chuchuli ni Katibu wa Mbio za Baiskeli mkoani Mwanza, amebainisha kuwa mwitikio wa wanawake katika mashindano ya mbio za baiskeli bado uko chini kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo, mila na tamaduni, gharama za kiingilio na miundombinu.
Chukuli amebainisha kuwa endapo Serikali itatengeneza mazingira rafiki ya kwa washiriki huenda ingesaidia idadi ya wanawake kuwa wengi kuliko ilivyo sasa.
“Mwitikio ni mdogo huenda ni kutokana na sababu ya mila na tamaduni zetu kuwa mwanamke bado yuko chini ya mamlaka ya mwanaume, lakini pia sababu nyingine ni hizi njia ni mbovu zinasababisha washiriki washindwe kuhimili,” amesema Chuchuli
Latest