Umeme unavyompaisha kimaisha binti wa miaka 21 Njombe

March 10, 2022 8:18 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kupitia umeme, ameweza kufungua biashara ya vifaa vya umeme kijijini kwake.
  • Kama binti mdogo, amefanikiwa kuwa msaada kwa wazazi na ndugu zake.
  • Wito wake kwa wanawake wengine ni wasibweteke kwani hamna uzuri katika hilo.

Dar es Salaam/Njombe. Wapo mabinti ambao licha ya kuzungukwa na nishati ya umeme, bado hawajaweza kutambua fursa zinazoweza kuwatoa kimaisha endapo watatumia nishati vizuri.

Kazi kama kuanzisha saluni, kuuza duka la bidhaa mchanganyiko, uokaji wa mikate, kuuza barafu na hata kusaga juisi, ni miongoni mwa kazi zinazohitaji nishati kuzifanya.

Ni tofauti kwa Restuta Mswata, mkazi wa kijiji cha Lusitu mkoani Njombe ambaye umeme wa gridi ndogo ya umefanikisha ndoto yake ya kuwa mfanyabiashara huku ikimuacha kama kioo cha mabinti na wanawake wengi katika kijiji chake.

Mwanzo wa safari

Restuta (21), ambaye alikuwa na ndoto kubwa ya kuendesha biashara lakini hakuifanikishwa kwa muda mrefu kwa sababu kijiji chake hakikua na umeme.

Ndoto yake ilianza kutimia mwaka 2019 baada ya mradi wa umeme wa gridi ndogo (mini grid) unaozalishwa na maji wa kampuni ya Rift Valley kuanzishwa kijijini hapo.  

“Biashara yangu ni duka la vifaa vya umeme na simu. Pia nina mlango mwingine ni duka la nguo, viatu na mabegi,” amesema Mswata ambaye amesoma hadi ngazi ya cheti (certificate) katika fani ya kompyuta.

Restuta akiwa dukani kwake. Picha| Thabit Mikidadi

Umeme huo wa maji ni miongoni mwa nishati safi na salama ambazo zimekuwa zikipendekezwa na wadau wa nishati kwa sababu zinapunguza uharibifu wa mazingira na kulinda afya za watu.

Kwa mujibu wa Restuta, umeme huo inamsaidia kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi kwani hata usiku unapoingia, yeye anawasha taa na kuendelea na kazi.

Kuwa na uzoefu wa bidhaa za umeme kumemsaidia kuwa na ushawishi kwa watu wengine kuona uhitaji wa bidhaa za umeme anazouza ikiwemo pasi na majagi ya kuchemshia maji.

Mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri

Mafanikio ya Restuta yalianza na imani aliyoipata kutoka kwa wazazi wake, akiwa binti wa mwisho kati ya watoto nane wa mzee Mswata.

Restuta ameiambia Nukta habari (www.nukta.co.tz) kuwa, baada ya kuhitimu masomo yake ya kompyuta, wazazi wake walimpatia mtaji ambao ulimsaidia kufungua biashara yake mwaka 2020.

“Baba alikuwa mwalimu, alipostafu, alinipatia pesa kidogo. Kipindi hicho nilikuwa sijaolewa lakini nilikuwa na mtoto,” anasema mwanamke huyo ambaye kwa mwezi biashara ikichanganya na uhakika wa kupata hadi Sh500,000.

Katika miezi iliyochangamka, faida yake huigawa nusu kwa kuongezea mtaji huku nusu nyingine ikienda kwenye kaunti ya benki kwa ajili ya kuweka akiba.


Soma zaidi:


Nuru angavu gizani

Kutokana na mafanikio yake, unaweza kuhisi Restuta ni mama anayejisikia na asiyependa kuchangamana na wanawake wenzake. Lakini hayupo hivyo. 

Restuta amekuwa mwalimu kwa wanawake wengine kijijini hapo namna ya kutumia nishati kujiletea maendeleo kwa kwa kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi ili kupunguza utegemezi kwa waume zao.

“Kuna wenzangu wengine wameshaanza kuniuliza ninafanyaje biashara, mabinti wadogo wadogo, kuna baadhi wananifuata wanafanikiwa,” anasema.

Ndoto yake ni kuwaona wanawake wengi zaidi katika kijiji cha Lusitu wakifanikiwa kibiashara na kutimizia ndoto zao.

Kupitia biashara yake, Restuta anaweza kuwasaidia wazazi na familia yake. Picha| Thabit Mikidadi.

Shujaa asiyesahaulika

Kupitia duka lake, Restuta amekuwa msaada kwa watu wanaomtegemea ikiwemo familia, ndugu na zaidi wazazi.

Kwa upande wa wazazi wake, huenda walichokifanya kwa binti yao ni uwekezaji ambao unawalipa kwa sasa kutokana na biashara hiyo kuwa sehemu ya wao kusaidika na mtoto wao.

“Umri wangu ndiyo ni mdogo lakini nini majukumu mengi. Nina “wa-care” (ninawahudumia) wazazi wangu maana mimi ndiyo msaada pia ndugu zangu ambao hawana uwezo mimi ndiyo ninawasaidia,” anasema Restuta.

Kama mfanyabiashara, changamoto ni sehemu ya safari ya ujasiriamali. Kwa Restuta, changamoto kubwa ni majukumu makubwa kwani anategemewa hasa na familia yake.

Hata hivyo, kinachomsaidia kuvuka milima na bahari zake ni kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wake huku maji yanapozidi unga akiruhusu ndugu zake wengine wamsaidie.

“Changamoto nazitatua kulingana na uwezo wangu. Nikipata changamoto, wapo ndugu zangu wanaonisaidia. Tunaishi kwa kusaidiana,”

Ujumbe wa Restuta kwa wanawake wengine ambao bado hawana muamko wa kutumia rasilimali zinazowazunguka ikiwemo nishati jadidifu, ni kutoka usingizini na kuzisaka fursa hizo.

Anasema hakuna uzuri wowote katika kuwa tegemezi kwenye jamii ikiwa una nguvu ya kufanya kazi na ari unayo.

Licha ya kuwa umemejua umekuwa ukiboresha maisha ya wanawake kiuchumi, lakini ni njia ya rahisi ya kutunza mazingira hasa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na shughuli za kibinadamu.

Umemejua unasaidia kupunguza uchafuzi wa hewa kwa sababu inapunguza matumizi ya kuni na mkaa, nishati ambazo zinazochochea ukataji wa miti.

Hupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati visivyoweza urejeshwa kama vile nishati ya  mafuta na kuni.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Upatikanaji na Matumizi ya Nishati Tanzania Bara ya mwaka 2019/20 ya Wakala wa Niashati Vijijini (REA), asilimia 90.2 ya viongozi wa jamii wanasema asilimia kubwa ya watu vijijini wanatumia umemejua kama mbadala wa ukosefu wa umeme wa gridi ya Taifa.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la WAN-IFRA-Press Freedom. WAN-IFRA haihusiki kwa namna yeyote na maudhui haya. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW