Wanawake wanavyotumia huduma za kibenki kujikwamua kiuchumi Mwanza

October 19, 2021 7:51 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mikopo na akiba ambazo wanatumia kama mitaji.
  • Benki, Serikali kuendelea kuwashika mkono.

Mwanza. “Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari ndoto yangu ilikuwa ni kuendelea na masomo ya elimu ya juu lakini hali ilikuwa tofauti baada ya kushindwa kuendelea na masomo hayo,” anasema Editha Leonard. mkazi wa jijini Mwanza.

Baada ya ndoto zake kutokutimia aliamua kujifunza udereva wa pikipiki (bodaboda) na sasa anafanya kazi ya kusafirisha abiria jijini hapa.

“Uthubutu katika maisha ndio mafanikio ya kukuza uchumi, baada ya matokeo ya kidato cha nne kutokuwa mazuri sikukata tamaa niliamini katika uthubutu sikufikiria mara mbili kwani kwa sasa maisha ni popote na hauwezi kuchagua kazi,” amesema Editha.

Editha  hakupenda kuendelea kuwa tegemezi kwa wazazi wake, alitamani kuwa na kipato chake mwenyewe na pia kujitofautisha na wasichana wengine ambao wameshindwa kupata fursa ya kusoma elimu ya juu.

Hata hivyo, ndoto ya binti huyo ni kuwa dereva wa malori makubwa. Tayari ameanza kujiwekea akiba kidogo kidogo ili apate ada ya kwenda kusomea kozi ya kuendesha magari katika Chuo Cha Elimu ya Ufundi Stadi cha jijini Mwanza.

Wakati akiendelea na shughuli zake anajiwekea akiba hiyo katika Benki ya Biashara Tanzania (TCB), jambo linalompa dhamana ya kupata mkopo kwa ajili ya kuanza masomo.

Editha kwa sasa anafanya shughuli hizo huku akiweka faida yake kwenye benki ya TCB ili kupata faida itakayomwezesha kupata mafunzo kwenye chuo cha Veta ili kutimiza malengo yake.

Akizungumza kwenye kongamano la kuwajengea uelewa wanawake ili waweze kuchangia kwenye uchumi wa nchi Oktoba 18, 2021 jijini hapa, Kaimu Mkurugenzi  wa TCB, Moses Manyatta amesema benki hiyo imejikita kuwawezesha wanawake waweze kukua kiuchumi.

Anasema katika uchunguzi wao walibaini wanawake wengi hususan wajasirimali wadogo hawapewi mikopo kwenye taasisi nyingi za kifedha na katika kuwasaidia benki inawapa mikopo yenye riba nafuu.

“Kongamano hili lilianza toka mwaka 2019 na katika kipindi hicho benki hiyo nchini ilitoa mikopo yenye thamani ya Sh600 bilioni, mwaka huu benki ilitoa mikopo ya Sh700 bilioni, ”amesema Manyatta.

Akiba na mikopo hiyo wamewasaidia wanawake wengi jijini hapa kujikwamua kiuchumi kupitia biashara na miradi ya kiuchumi inayowaingia kipato kuendesha maisha yao.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula ameitaka benki hiyo kuwafikia wanawake wa vijijini ili nao waweze kunufainika na fursa hizo za mikopo.

Waziri huyo pia ameiomba benki hiyo kutoa mikopo yenye riba nafuu itakayowasaidia wanawake wengi kupata mikopo na kuweza kurejesha kwa wakati.

“Kongamano hili limeanzishwa kwa wakati mwafaka wakati nchi ikiwa kwenye mikakati mbalimbali ya kuwainua wanawake kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi, ni vema sasa makongamano haya yafanyike kila mkoa hususan maeneo ya vijijini ili wanawake waliopo kwenye maeneo hayo nao waweze kukuza uchumi wao,” amesema Mabula.

Mbali na benki hiyo, pia Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuwasaidia wanawake ambapo imetenga asilimia 10 kwenye kila pato la halmashauri kwa ajili ya mikopo ya wanawake.

“Niwaombe wanawake waendelee kuchangamkia fursa na kutangaza bidhaa wanazofanya kupitia makongamano na warsha mbalimbali  ili waweze kukuza mitaji yao,” amesema Mabula.

Enable Notifications OK No thanks