Wanawake katikati ya safari ngumu kuongeza ushiriki, maendeleo Kigoma
- Zaidi ya nusu ya washiriki wa mikutano katika baadhi ya mitaa ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ni wanawake.
- Baadhi ya viongozi wa mitaa wanawake wanaona bado kuna watu wanawadharau.
- Kuna hatari iwapo vipaumbele vya wanawake havitatekelezwa wanawake watakata tamaa kushiriki katika maendeleo.
Kigoma. Katika moja ya mikutano ya Serikali ya mtaa wake, Riziki Ngulinzila aliona bora avunje ukimya.
Alikuwa amechoka kuendelea kutaabika katika mtaa wake huku akiishi na changamoto za upatikanaji huduma za kijamii zilizozuia kutimiza sehemu kubwa ya shughuli zake za kiuchumi na kijamii.
Kwa muda mrefu sasa mtaa anaoishi Riziki (52) uliopo katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji mkoani Kigoma, umekuwa ukikabiliwa na changamoto lukuki licha ya kuwa mjini.
“Siku hiyo niliamua bora tu niseme, niliomba viongozi watusaidie kutatua kero ya barabara, mimi ni mlemavu barabara hii ya sasa hainifai,” anasema Riziki akiwa amekaa pembezoni mwa nyumba yake fupi ya bati iliyojengwa kwa udongo.
Riziki anayeishi mtaa wa Busomelo katika kata ya Kasimbu anasema viongozi walimweleza kuwa wangefanyia kazi kero zake, hadi sasa ni miaka miwili imepita sehemu kubwa mambo hayajafanyika.
‘Huu ni mwanzo tu’
“Nitaendelea kusema kwenye mikutano hata kama hawajatekeleza kero zangu,” anasema Riziki mama wa watoto sita na wajukuu wanne.
Katika manispaa hii ya Kigoma/Ujiji, wanawake ndiyo vinara wanaojitokeza zaidi katika mikutano ya serikali za mitaa ambayo huibua na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Viongozi nane kati ya 10 wa serikali za mitaa hiyo waliiambia Nukta Habari kuwa wanawake ndiyo hujitokeza kwa wingi ikilinganishwa na wanaume na baadhi wamekuwa wakipaza zaidi sauti zao na kufuatilia kwa kina masuala yanayowahusu.
Kama ilivyo mikoa mingine ya Tanzania, wanawake wa mkoa huo miaka ya nyuma, kiutamaduni walikuwa nyuma katika kushiriki shughuli za maendeleo zinazowahusu katika ngazi za mashina kwa kuwa wanaume walitawala kila mahali.
Wengi hawaogopi tena kunyanyua vidole katika mikutano na kurusha maswali magumu kwa viongozi kuhusu kero zao ambazo sehemu kubwa zimekuwa ni masuala ya elimu, afya, maji, miundombinu na ulinzi na usalama.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgumile, Pius Saboya akiwa na wajumbe wa mtaa wakifanya maandalizi ya kikao na wananchi Juni 29, 2021. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta.
Mwamko wa wanawake mkubwa mikutanoni
“Kwa sasa mwamko ni mkubwa sana na wanawake wengi tunashiriki mikutano kuliko zamani… siyo vizuri kutohudhuria mikutano kwa kuwa inasaidia kufahamu mambo mengi ya Serikali na ya kijamii,” anasema Siwa Kiza, mkazi wa Mtaa wa Sokoine katika kata ya Buzebazeba.
Ushiriki wao katika mipango inayohusu mitaa yao imezidi kuwapatia fursa ya kutatua kero zao licha ya baadhi kukatishwa tamaa na baadhi ya mamlaka kwa kutotekeleza ipasavyo mahitaji yao.
Siwa anakumbuka kuwa ukosefu wa shule ilikuwa ni changamoto kubwa katika kata yao jambo lililokuwa likimfanya aliseme mara kwa mara katika mikutano ya mtaani kwao hadi lilipofanyiwa kazi.
Kwa sasa, anasema wanaisukuma Serikali ipeleke walimu wa sayansi na hisabati wa kutosha katika Shule ya Sekondari ya Buzebazeba na kuwajengea zahanati au kituo cha afya karibu na makazi yao.
“Ilipojengwa shule nilifurahia sana sasa wanangu wamepata shule na tulichangia kila mtu Sh3,000. Mimi nipo radhi kuchangia maendeleo kwa mawazo na fedha bila ya kuwa na mtoto, mimi ni mzazi wa wote,” anasema Siwa.
Hata wakati wengine kama Riziki na Siwa wakiwa na uthubutu wa kusema hadharani juu ya kero zao bado wapo ambao huona aibu kusema mbele ya hadhara licha ya kuwa na kero lukuki au mawazo ya kuzitatua kama anavyosema Mtendaji wa Serikali ya Buzebazeba, Shaban Ibrahim.
Mmoja wa wanawake ambao wako mstari wa mbele kuchagiza maendeleo mkoani Kigoma. Picha| Gift Mijoe.
Wanawake ‘wawakimbiza’ wanaume mikutanoni
Katika mtaa huo wa Buzebazeba, wastani wa watu 500 huudhuria mkutano wa mtaa na kati yao, kwa mujibu wa Shaban, robo tatu ni wanawake.
“Kuna mwingine huona aibu kusema mbele za watu ila baada ya kikao anakufuata pembeni na kukueleza. Hali hii imebaki hivi kwa muda mrefu sasa. Wengi wao wanakufuata pembeni utakuta watano au sita hivi wanakueleza kero zao na unazisikiliza,” anasema.
Hata wanapoulizwa kwa nini wanafanya hivyo, Shaban anasema walimweleza kuwa huwa wanaona muda wa mkutano ni mdogo licha ya ukweli kuwa huwa hawanyooshi mikono wakaonwa.
Katika kipindi cha miaka minne hivi, uhamasishaji wa ushiriki wa wakazi katika mitaa mbalimbali katika manispaa hii ya Kigoma/Ujiji umekuwa ukichagizwa zaidi na waraghabishi ambao hufanya kazi kwa karibu na viongozi wa ngazi za chini.
Waraghabishi ni sehemu ya wakazi ndani ya mtaa ambao huwa wanahamasisha wananchi kuibua vipaumbele na kutatua kero zao ikiwa ni moja ya njia madhubuti za ushirikishwaji katika maeneo yao.
Kiutaratibu serikali ya mtaa au kijiji inatakiwa kufanya mkutano angalau mmoja katika kila baada ya miezi mitatu ili kuwapa fursa wakazi kuibua vipaumbele vyao na kutatua kero zinazowakabili.
Viongozi wa serikali za mitaa wanawake licha ya kuwa wengi wanatekeleza ipasavyo majukumu yao bado wapo ambao hukutana na vikwazo kutokana na mfumo dume kuendelea kutawala.

Bado kuna dharau kwa viongozi wanawake
Mtendaji wa Mtaa wa Bulega katika kata ya Buzebazeba, Adela Stephano anaeleza kuwa akiitisha mkutano kuna watu wengi huwa wanajitokeza kumsikiliza lakini vijana humdharau.
“Jumamosi moja tulikuwa na kesi moja yule kijana tulimuita hapa lakini alipokuja akasema ‘mimi sikai hapa, niambieni mlichonitia haraka’ alifanya vile labda sababu mimi ni mwanamke,” anasema Adela (42) na kuongeza “hayo mambo yapo sana.”
Adela anasema waraghabishi walimsaidia kuwaelewesha wakazi wake umuhimu wa kushiriki mikutano hiyo na kutii taratibu walizojiwekea.
Viongozi wa mitaa na kata wana wasiwasi kuwa iwapo vipaumbele vya wakazi wao havitapewa vipaumbele kuna hatari ushiriki wa wanawake unaweza ukapungua siku zijazo.
Tayari baadhi ya mitaa licha ya ushiriki wa wanawake kuwa mkubwa, wanaume wameshaanza kupungua kiasi cha viongozi wa mitaa kutumia vivutio kama kuigiza au kuwadanganyishia watu ajenda za Tasaf ndani ya mikutano yao.
Changamoto hiyo inatokea wakati Serikali ikihaha kutimiza vipaumbele lukuki vya maendeleo katika kipindi cha uhaba wa rasilimali watu na fedha.
“Malalamiko hayo yalikuwepo, baadhi hawaoni vipaumbele vyao vikitekelezwa. Tunaendelea kuwaelimisha kuwa mahitaji kwa sasa katika manispaa yetu ni mengi kuliko rasilimali,” anasema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Fredinand Filimbi.
Kwa mujibu wa uongozi wa Manispaa hiyo, wakazi wote wanashiriki kikamilifu katika masuala mbalimbali ya maendeleo kupitia kuibua vipaumbele, kuchangia, kutekeleza, kusimamia na kufanya tathmini waliyotekeleza.
Wanaharakati wa haki za wanawake wanaeleza kuwa ni faraja kuona wanawake wanashiriki ipasavyo katika kuibua na kutatua kero zinazowakabili ikiwa ni hatua kubwa kufikiwa Tanzania.
Mtaalam wa masuala ya uraghabishi, Annagrace Rwehumbiza anasema katika shughuli za kuhamasisha ushiriki wa wanawake ameshuhudia wengi wakibadilika na kupata sauti ya kuweza kusimama na nia thabiti ya kushiriki na kuleta mabadiliko.
“Yule mwanamke ambaye alikuwa haongei leo anasimama kuelezea masuala yanayomhusu ni kitu ambacho huwa kinaniletea msisimko mkubwa wa mwili halafu naweza kulala kwa amani… hii ni ‘transformation’ (mabadiliko makubwa) kubwa sana,” anasema Annagrace.
Latest