Uaminifu wawabeba wanawake kazi za utingo, ukatishaji tiketi za mabasi

March 5, 2022 6:01 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Idadi ya wanaofanya kazi hizo inaongezeka kila siku.
  • Ukosefu wa ajira wachangia wanawake kufanya kazi hizo.
  • Uaminifu, uwezo wa kufanya kazi wawapaisha.

Mwanza. Ni stendi ya mabasi ya mikoani ya Nyegezi mkoani Mwanza, pilika pilika za hapa na pale zinaendelea. Katika eneo hili utapokelewa na kundi la watu, kila mmoja ana kazi yake, wapo watakaokuvuta huku na huko, wapo watakaokukatia tiketi na wengine ni makondakta.

Hapo utawakuta wanawake na wanaume wakiendelea na majukumu ya kuwasaidia watu wanaofika katika stendi hiyo kukata tiketi, kusafiri na kusafirisha mizigo kwenda katika mikoa mbalimbali Tanzania.

Tofauti na miaka ya nyuma, ilikuwa siyo rahisi kuwakuta wanawake wakifanya shughuli hizo. Lakini kwa sasa hali imebadilika, wanawake nao wameingi kati kupambania fursa za ajira kila zinapojitokeza.

Wanawake wanaofanya kazi ya utingo (ukondakta) katika stendi hiyo wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa “kazi popote maadamu mkono unaenda kinywani na watoto wanaenda shule.”

Mmoja wa wanawake hao, Elizabeth John ambaye ni kondakta katika moja ya basi linalofanya safari za mikoani anasema haikua rahisi kuingia katika kazi hiyo kwa sababu ya mfumo dume uliokuwa umetawala.

Shughuli mbalimbali zikiendelea katika stendi ya mabasi Buzuruga. Picha na Mariam John

Elizabeth, mama wa watoto wawili anasema licha ya changamoto alizokutana nazo hakuacha kuipambania kazi ya kuhudumia abiria katika mabasi, ambayo alikuwa anaipenda kwa muda mrefu.

Mama huyo aliingia katika kazi ya ukondakta mwaka 2016 baada ya kukosa kazi ya ualimu aliyosomea katika Chuo Cha Ualimu cha Butimba Mwanza.

Kukosa kwake kazi ya ualimu, ilikuwa ni fursa ya kuangalia vyanzo vingine vya mapato ili kuboresha maisha yake. 

“Naifurahia kazi yangu naweza kuhudumia familia yangu na watoto wanasoma kwa kweli siyo tegemi tena,” anasema Elizabeth ambaye awali  alikuwa anaona aibu akihofia kukutana na marafiki zake ambao watapanda kwenye basi ambalo anafanyia kazi kuwa watamafikiria tofauti.

Elizabeth ni miongoni mwa wanawake wengi ambao wamevunja mnyororo wa utegemezi na kuamua kufanya kazi kama wanaume katika sekta ya usafirishaji.

 “Tunafanya kazi kwa zamu tupo wawili tunabadilishana napata muda wa kupumzika,” anasema Elizabeth akiwa ofisini kwake stendi ya mabasi Nyegezi.


Soma zaidi:


Uamifu, kujituma kwawabeba wanawake

Wakizungumzia mwitikio wa wanawake kujitokeza kwa wingi kufanya shughuli za ukondakta baadhi ya wakazi jijini Mwanza wanasema hali ya uchumi imekuwa sababu ya wao kutobagua kazi.

“Maisha ya sasa ni tofauti na zamani wanaume walikuwa wanafanya wake zao kuwa tegemezi, kwa sasa wanaona mmoja akitoka na mwingine akitoka jioni wakileta kitu na kukiunganisha pamoja wanafanya jambo la maana,” amesema Judith Ferdinard, mkazi wa Kilimahewa jijini Mwanza.

Anasema sababu nyingine ni ukosefu wa ajira ambapo wanakaa muda mrefu nyumbani bila kazi ya kufanya, hivyo kujishughulisha na kazi yoyote.

Katibu wa Chama Cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) Mkoa wa Mwanza, Anwar Seif ametaja sababu kuu tatu zinazosababisha wanawake waaminiwe kwenye kazi zao mojawapo ikiwa ni pamoja na uaminifu.

“Wanawake wamekuwa wakijitambua, wametambua majukumu yao. Ni waaminifu wapo tayari kushaurika na wanaweza kurudisha fedha tofauti na wanaume ambao wanaweza kudaganya,” anasema Seif.

Anasema kitu kingine ni waangwana, si wajeuri na niwatiifu na kwamba wanafanya kazi kwa maadili makubwa wakiamini kazi hiyo ndiyo inasababisha maisha ya familia zao yanaenda.

“Wamiliki wengi wamekuwa wakiwaamini wanawake kwa kuwa fedha wanazozipata kwenye kazi hiyo asilimia 100 zinarudi kutimiza majukumu ya nyumbani, wao wamekuwa walezi wakubwa wa familia tofauti na wanaume ambapo wanawaza kulewa na kucheza kamali,” anasema katibu huyo.

Wanawake wamesema “Kazi popote maadamu mkono unaenda kinywani na watoto wanaenda shule.” Picha| Mariam John.

Sifa nyingine ya wanawake kuaminiwa ni kutokana na hivi sasa vyombo vingi vya moto vinaendeshwa kidigitali hivyo wanaweza kuhimili kufanya kazi hiyo ambayo haitumii nguvu nyingi kama kunyanyua vyuma au kwenda shamba.

Hata hivyo, Mwenyekiti  wa TABOA mkoa wa Mwanza,  Ernest Gutomwanza ambaye amesema pamoja na suala la kuaminiwa lakini pia zipo kazi ambazo wanawake hawawezi kuzifanya maisha yao yote.

Anatambua kuwa mwamko wa wanawake kufanya shughuli hizo umekuwa ukiongezeka siku hadi siku na kwamba asilimia 20 ya wamiliki wa mabasi hivi sasa wamewaajiri wanawake.

“Ni asilimia 80 tu ya wamiliki ndiyo wamewaajiri wanaume kutokana na kazi nyingine kama za ufundi na zingine ambazo wanawake hawawezi kuzifanya, lakini pia kisababishi kingine cha wanawake kuaminiwa ni kutokana na ushawishi wao kwa wateja uko kiwango cha juu,” anasema Gutomwanza.

Amewashauri wanawake waendelee kuchapa kazi ili kujiletea maendeleo na kuzitunza familia zao kwa kushirikiana na wanaume zao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW