Usafiri mabasi ya mikoani warejea kawaida

December 29, 2021 11:44 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kupita sikukuu ya Krismasi.
  • Kupata kwa nauli na wingi wa abiria ilikuwa ni miongoni mwa changamoto.
  • Taboa yasema hali ni shwari sasa hakuna usumbufu.

Mwanza. Hali ya usafiri wa mabasi yaendayo mikoani imeanza kurejea kawaida baada ya usafiri huo kukumbwa na changamoto kadhaa katika baadhi ya mikoa zilizosababisha na ongezeko kubwa la abiria msimu wa sikukuu ya Krismasi.

Katika baadhi ya mikoa hasa abiria waliokuwa wakisafiri kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kupandishiwa nauli na wengine kukosa safari kutokana na wingi wa watu waliokuwa wanasafiri katika mikoa hiyo.

Changamoto hizo pia zilijitokeza katika Mkoa wa Mwanza ambao ni kiungo cha shughuli za usafirishaji katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. 

Hata hivyo, hali ya usafiri katika maeneo mengi imerejea kama ilivyokuwa awali tofauti na ilivyokuwa wiki moja iliyopita.

Wakizungumza na Nukta habari (www.nukta.co.tz) baadhi ya abiria waliokutwa katika stendi ya mabasi ya Nyegezi  mkoani hapa wamesema hawapati usumbufu kama walivyokuwa wanaona kwenye taarifa habari katika maeneo mengine.

“Hapa ukikata tiketi unapata siti yako, hatujauziwa tiketi moja zaidi ya watu wawili, nauli iko sawa ni kama ya siku zote,” amesema Neema Paul msafiri kwenda Kahama mkoani Shinyanga.

Abel Juma yeye alikuwa anasafiri kwenda mkoani Singinda amesema wiki moja iliyopita alishindwa kusafiri kwa kuwa kila gari aliloenda kukata tiketi alikuta nafasi zimejaa.

“Niliamua kuacha kupisha huo msululu lakini sasa nimekata na nimepata nafasi kawaida na si za kugombania kama ilivyokuwa,” amesema Juma.

Wakati mwingine, baadhi ya wakatishaji tiketi walitumia kisingizio cha kuwaambia watu kuwa magari yamejaa ili kujipatia fedha zaidi ya kiwango kinachopaswa kutozwa kwa kila safari.

Hali hiyo ilisababisha usumbufu kwa abiria na katika baadhi ya maeneo madereva na wamiliki wa mabasi wamechukulia hatua za kisheria kwa kupandisha nauli msimu wa sikukuu za Kristmas.


Zinazohusiana: 


Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Yohana John ambaye amereja kutoka mkoani Kilimanjaro jana amesema hajapata usumbufu wowote wa kukosa basi kwa sababu idadi ya watu wanaosafiri imepungua.

“Wiki iliyopita hali ilikuwa siyo nzuri, watu walikuwa wengi mpaka nikakosa basi kwenda Moshi. Nikalazimika kupanda gari binafsi ili nisikose kujumuika na ndugu zangu nyumbani,” amesema John. 

Dalali wa ukatishaji tiketi kwa magari yanayoenda mikoa ya kaskazini katika kituo cha Bunju B jijini hapa, Juma Nkwabi amesema hali sasa ni shwari ikilinganishwa na wiki iliyopita licha ya kuwa hali hiyo ilimsaidia kuingiza kipato.

“Wiki iliyopita hapakutosha hapa, tulifanya kazi ya ziada kuwatafutia watu magari ya binafsi kwa sababu mabasi yalikuwa hayatoshi lakini sasa hali imerejea kama kawaida,” amesema Nkwabi.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi nchini (Taboa) Mkoa wa Mwanza, Anwar Said, amesema hali ya usafiri kwa sasa iko salama na ajali zimepungua msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

Kuhusu suala la kupandishwa kwa nauli amesema mara nyingi suala hilo hufanywa na wakatisha tiketi ambao kwa tamaa zao hulazimika kupandisha na kwa upande wao suala hilo wamelidhibiti kwa kiasi kikubwa.

“Tunakushukuru kwa mwaka huu hali imekuwa nzuri na usimamizi umekuwa mzuri pia mamlaka husika ikiwemo Serikali na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) kwa pamoja wamekuwa wakishirikiana kuhakikisha nauli haziondishwi na magari yanasafirisha abiria yale yaliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Said.

Katibu huyo amesema wamekuwa wakichukua hatua ya wao kwa wao kujionya kuhusiana na kupandisha nauli lakini pia watu waliowapa dhamana ya kukatisha tiketi kuhakikisha hawapandishi nauli.

“Kwa pamoja tumeshirikiana na ndiyo maana katika kipindi hiki hatujasikia taarifa za ajali na hadi kwenye maeneo mengine kama Tanga mabasi yalionekana kukosa abiria,” amesema Said.

Enable Notifications OK No thanks