Rais Samia aongoza mamia kuaga mwili wa Mafuru Dar es Salaam

November 14, 2024 6:08 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Aeleza mchango wake katika kutatua changamoto ya uhaba wa dola na maandalizi ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Lawrence Mafuru huku akieleza kuwa kifo cha kiongozi huyo ni pigo kwa Taifa kutokana na sifa zake za ubunifu na uchapakazi. 

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika shughuli ya kuaga mwili wa Mafuru katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam leo Novemba 14, 2024 amesema kiongozi huyo alikuwa zawadi kwa familia, jamii na Taifa.

“Nataka niseme kwamba Lawrence alikuwa ni zawadi nzuri kwa Taifa letu kwa ujumla…Lawrence alikuwa mshauri mwema mwenye uwezo na hekima ya kushauri hata katika jambo ambalo alifahamu hawezi kuafikiana nalo,”amesema Rais Samia.

Rais Samia pia amemuelezea kiongozi huyo kuwa miongoni wa watumishi mashujaa, waadilifu walioishauri Serikali katika kutatua baadhi ya changamoto zilizokuwa zinalikumba Taifa.

“Ushujaa unaweza kujitokeza katika namna mbalimbali, katika kufanya kazi kwa bidii na kujitoa kwa Taifa lako bila shaka ni namna iliyo dhahiri ya ushujaaa hivyo basi nitakuwa sijakosea nikisema Lawrence Mafuru ni moja wa mashujaa wa Taifa letu,”amebainisha Rais Samia.

Mbali na Rais Samia shughuli hiyo ya kuuaga mwili wa Mafuru imehunduriwa na viongozi wengine wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge Mussa  Zungu, viongozi wa awamu zilizopita akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Mizengo pinda, wenza wa marais pamoja na familia.

Mchango wa Lawrence Mafuru kwa Taifa

Rais Samia amewaambia waombolezaji wa shughuli hiyo kuwa Mafuru ni miongoni mwa viongozi watakaokumbukwa katika mchango wake kwa sekta binafsi, Serikali na kwa Taifa huku akiacha alama chanya katika changamoto mbalimbali zilizolikumba Taifa.

Miongoni mwa maeneno aliyoacha alama Mafuru ni katika changangamoto ya uhaba wa Dola za Marekani zinazohitajika katika kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma nje ya nchi.

Marehemu Mafuru kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu na watendaji wengine wa Serikali walichaguliwa kuunda kamati maalum iliyoibua mapendekezo yaliyomaliza tatizo hilo nchini.

Si hayo tu Mafuru akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya  Mipango alikuwa miongoni mwa watumishi waliokasimishwa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 baada ya ile ya awali inayoishia mwaka 2025 kufikia mwisho wake.

Chini ya uongozi wa Prof Kitila Mkumbo Waziri wa Wizara ya Mipango na Uwekezaji waliandaa midahalo na kukusanya maoni kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali hatimaye kufanikisha rasimu ya kwanza ya dira hiyo iliyowasilishwa kwa Rais Samia hivi karibuni.

Sanjari na hayo Rais Samia ameeleza kuwa yote aliyoyapokea katika rasimu hiyo yote ni mema kwa taifa na kwa upande wake amefanya marekebisho katika sehemu chache.

Hata hivyo, Rais Samia amesisitiza kuwa ni vyema kutumia nafasi ya uhai kufanya kazi kadri iwezekanavyo ili siku ukifa ukumbukwe kwa utendaji kazi wenye manufaa.

Mafuru atazikwa kesho Novemba 15, 2024 katika makaburi ya Kondo, Ununio mkoani Dar es Salaam.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiongoza waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Marehemu Lawrence Mafuru katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam. Picha/ Ikulu Mawasiliano.

Enable Notifications OK No thanks