Mambo yatakayosaidia kuongeza ufanisi utoaji mirabaha ya wasanii Tanzania

February 19, 2022 10:22 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuongeza uwazi katika makusanyo na mgao mirabaha.
  • Cosota yashauriwa kufuata sheria ikiwemo kuendesha mkutano mkuu wa mwaka.
  • Mirabaha isiishie kwa wanamuziki peke yake, iwafikie wasanii wengine.

Dar es Salaam. Wadau wa sanaa Tanzania wameshauri mambo mbalimbali yatakayosaidia kuongeza ufanisi na uwazi wa ukusanyaji na utoaji wa mirabaha kwa wabunifu nchini ikiwemo kuwafikia wabunifu wengine na siyo wabunifu wa muziki pekee.

Kauli hiyo imeuja baada ya Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota) kutoa mirabaha yenye thamani ya Sh312 milioni kwa wasanii wa muziki ikiwemo Kwaya ya Mtakatifu Cecilia ya Arusha iliyopata Sh8.7 milioni na msanii Alikiba aliyepata Sh7.5 milioni.

Hata baada ya Cosota kutoa mirabaha hiyo kumekuwa na maoni tofauti ambapo baadhi wamepongeza hatua hiyo ya kuwatambua wasanii huku wengine wakisema haikutolewa kwa usawa.

Mtandao wa Tasnia ya Ubunifu Tanzania (CINT) umetoa maoni yake ambao unaamini yakiwafanyiwa kazi yataongeza ufanisi na uwazi wa mirabaha hiyo, hivyo kupunguza malalamiko kwa baadhi ya wasanii.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 19, 2022, Mkurugenzi Mtendaji wa CINT, Robert Mwampembwa amesema ugawaji wa mirabaha hiyo ulikiuka utashi na matakwa ya sheria kwenye maeneo muhimu ikiwemo kugawa mirabaha kwa kutumia sampuli badala ya kuigawa kwa wabunifu wote wanaostahili.

“Sheria ya Hakimiliki na Ushirikishaji inaitaka Cosota kugawa mirabaha kwa kuzingatia leja ya kumbukumbu. Leja hizi zinapaswa kukusanywa kutoka nchini nzima kwa watumiaji mbalimbali wa kazi za ubunifu.

“Hata hivyo, Cosota ilitangaza kuwa wametumia kumbukumbu za redio kwa baadhi ya wanamuziki kama sampuli ya kugawa mirabaha. Huu ni ubaguzi, kinyume na matakwa ya sheria, “ amesema Mwampembwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa CINT Robert Mwampembwa (kushoto) akiwa na Mwanachama wa CINT, John Kitime (Kulia). Picha| Rodgers George.

Mirabaha iwafikie wabunifu wengine pia

Inapozungumziwa mirabaha, baadhi ya watu wanadhani ni kwa ajili ya wanamuziki tu, jambo ambalo siyo la kweli. Mirabaha ni stahiki ya wabunifu ikiwemo watunzi wa muziki, waandishi wa vitabu, waandishi wa filamu na hata wachoraji.

Kwa mirabaha iliyotolewa na Cosota mara mbili mfululizo (2019 na 2022) imekuwa ikiwafikia wabunifu wa muziki pekee na kuwasahau wengine ikiwemo waandishi wa filamu ambao pia kazi zao zinatumika sehemu mbalimbali nchini.

“Cosota inafanya kazi kwa ajili ya wasanii wote na watunzi/wabunifu wa kazi zenye hakimiliki zikiwemo filamu, programu (maunzilaini), sanaa za uchongaji, usanifu, waandishi na makundi mengine. 

“Utaratibu huu siyo mzuri na hautendi haki kwa wasanii wengine wote wasio wanamuziki na inaleta mgawanyiko ndani ya sekta,” amesisitiza Mwampembwa.


Soma zaidi:


Uwazi na siyo mafichoficho

Wadau hao wa sanaa wameshauri uwepo wa uwazi katika chama hicho cha hakimiliki ili kuimarisha utendaji kwani tangu mwaka 2008, wanadai Cosota haijawahi kuwa na bodi ya wakurugenzi,  jambo linalofanya chama hicho kufanya maamuzi ambayo yanaibua maswali.

“Ugawaji wa mrabaha unatakiwa kutanguliwa na mkutano mkuu, jambo ambalo halikufanyika. Mara ya mwisho kufanyika mkutano mkuu ni mwaka 2007” amesema Mtendaji huyo wa CINT akiongeza kuwa mkutano huo husaidia kujua hali za wasanii, waliopo hai, waliopo nje ya nchi ili stahiki zao ziwafikie warithi au kokote waliko.

CINT inaishauri Cosota kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mirabaha kwani kwa fedha zilizotolewa Januari ni kutoka kwenye redio saba kati ya redio 172 zilizosajiliwa nchini Tanzania.

“Kuna sehemu nyingi za kukusanya mirabaha, kuna televisheni, redio, majukwaa ya mtandaoni kama Spotify, sehemu za kuchapisha na kampuni za mawasiliano,” amesema Mtendaji huyo wa CINT.

Pamoja na hayo, CINT imeshauri Serikali kuunda ofisi ya haki miliki pamoja na kuisasisha sheria ya hakimiliki nchini ili kuwanufaisha wasanii wa pale kazi zao zinapotumia kote nchini na hata kimataifa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW