Jessica Mshama: Mwanamuziki, Mjasiriamali anayebadilisha maisha ya Watanzania kwa biashara

Rodgers George 0535Hrs   Agosti 03, 2019 Ripoti Maalum
  • Ana miaka 23 na anamiliki kampuni ya J Sisters inayoendesha miradi ya kiuchumi zaidi ya mitano.
  • Hutumia kipaji cha muziki na elimu ya biashara kuwawezesha wasichana kuinuka kiuchumi. 

Dar es Salaam. Kasi ya vijana kuchangamkia fursa na kuanzisha kampuni ili kukabiliana na ukosefu wa ajira inazidi kuongezeka kila siku Tanzania. 

Siyo tu vijana wameamua kujiajiri na kupata kipato bali ajira hizo zimekuwa sehemu muhimu kwa jamii zinazowazunguka kunufaika na bidhaa na huduma wanazotoa katika miradi wanayoiendesha. 

Jessica Mshama, Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki ni miongoni mwa vijana wa kike Tanzania ambao wako mstari wa mbele kutumia vipaji na elimu zao kutengeneza mustakabali mzuri wa maisha. 

Wakati vijana wengine wakisubiri kuajiriwa, Jessica (23) ameamua kuitumia shahada yake ya kwanza ya usimamizi wa biashara kuanzisha kampuni mama ya J Sisters Enterprises ambayo inaendesha biashara zaidi ya tano. 

Jina la Jessica linaweza lisiwe geni kwa watu wengi ambao wamekuwa wakifuatilia muziki wa Tanzania, kwani amekua muimbaji wa nyimbo za injili kupitia kundi la J Sisters tangu akiwa na miaka tisa. Kundi hilo liliwahi kutamba na vibao vya “Rushwa” na “Tanzania”. 

Licha ya kuwa Jessica ana kipaji cha kuimba, haukuishia tu kuelimisha na kuburudisha kwa kutumia nyimbo, ameenda mbali zaidi na kuigusa jamii kwa kuanzisha miradi mbalimbali inayotoa ajira. 

“Nafanya kazi kwa bidii ili kupunguza ukosefu wa ajira kwenye jamii kwa kutoa ajira na mafunzo kwa vijana ambao wana ndoto za kubadilisha maisha yao,” anasema Jessica. 


Zinazohusiana: 


Licha ya kuwa Jessica ana kipaji cha kuimba, haukuishia tu kuelimisha na kuburudisha kwa kutumia nyimbo, ameenda mbali zaidi na kuigusa jamii kwa kuanzisha miradi mbalimbali inayotoa ajira. 

“Nafanya kazi kwa bidii ili kupunguza ukosefu wa ajira kwenye jamii kwa kutoa ajira na mafunzo kwa vijana ambao wana ndoto za kubadilisha maisha yao,” anasema Jessica. 

Kampuni hiyo, iliyoajiri wafanyakazi zaidi ya 40 katika maeneo mbalimbali nchini, inaendesha kiwanda cha kutengeneza siagi ya karanga na matunda na kufungasha asali kilichopo Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ambapo bidhaa zote za kampuni hiyo zinatumia jina la “Joy”. 

Karanga zote ambazo zinatumika kutengenezea siagi hiyo zinalimwa katika shamba la kampuni hiyo lililopo jijini Dodoma huku matunda yakinunuliwa kwa wakulima wa  hapa nchini. 

Uwekezaji mwingine ambao ameufanya Jessica ni kuanzisha kiwanda cha uokaji mikate pamoja na ufugaji wa kuku wa nyama katika wilaya ya Bagamoyo na saluni ya kike jijini Dar es Salaam.

Jessica (kushoto) akiwa na marafiki zake  katika moja ya maonyesho ya shughuli zake za utengenezaji wa asali Picha|Jessica.

Haikua rahisi kufika hapo 

Jessica ameiambia www.nukta.co.tz kuwa haikua rahisi kuongoza kampuni hiyo katika umri mdogo lakini shauku ya kuondoa dhana ya kuwa wanawake hawawezi ndiyo iliyomsukuma kuanzisha miradi mingi inayoleta matokeo chanya kwenye jamii. 

“Sikukubaliana na dhana hiyo na nikahamasika na kuithibitishia jamii kuwa wasichana wanaweza kuinuka kiuchumi na kuwa viongozi na siyo lazima wasubiri mpaka waletewe kila kitu,” anasema Jessica. 

Anasema anatumia uwezo alionao kuwahamasisha wasichana na wanawake kuingia katika ujasiriamali ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao.

Katika siku za awali wakati kampuni yake inaanza, watu na wafanyakazi waliokuwa chini yake hawakumkubali kuwa anaweza kuwaongoza katika shughuli za uzalishaji na kuiendeleza kampuni hiyo. 

Hivyo ni kusema, umahiri wake kwenye uongozi ulimfanya kuzishinda changamoto zote na jamii inayomzunguka kuamini kuwa yeye ni sehemu ya kuleta mabadiliko Tanzania. 

Caren Hezron (22) ni mmoja kati ya wafanyakazi wa “Wealthy Style” saluni iliyo chini ya Jessica. Yeye amemuelezea Jessica kama mwajiri mzuri anayejali wafanyakazi wake na kuwasimamia kwa haki na uwazi.

“Mara kadha wa kadha Jessica hujumuika pamoja nasi na kufanya kazi, kuna muda hupanga bidhaa kwenye makabati na kusaidiana na wafanyaazi wake,” amesema Caren.

Sasa jamii inamtambua Jessica

Juhudi zake za kufanya kazi kwa bidii na kugusa maisha ya watu wengi kumemfanya binti huyo atambulike kimataifa ambapo aliwahi kupata tuzo ya “Malkia Ajaye” kutoka kampuni ya habari ya Clouds Media Group (CMG) katika kampeni yake ya Malkia wa Nguvu.

Pia jarida la “Business Elites” limemtambua kama kijana anayetumia mitandao ya kijamii kuleta matokeo chanya kwenye jamii. 

Hata hivyo, mafanikio aliyoyapata Jessica yanamuongezea ari ya kuendelea kutafuta fursa zaidi katika sekta ya biashara ili kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayoajiri watu wengi zaidi. 

Related Post