“Injili kwa flash”: Biashara haramu inayohujumu mapato ya wasanii, Serikali Tanzania

January 2, 2021 7:37 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wafanyabiashara wasema biashara hiyo ni daraja kati ya wasanii wa muziki wa injili na kuisambaza injili kwa watu.
  • Hata hivyo, biashara hiyo haifanyiki kwa utimilifu kwani muziki unaowekwa, ni tofauti na matangazo yanayotolewa.
  • Baadhi ya flashi huharibika ndani ya muda mfupi licha ya kuuzwa kwa bei ya juu.

Dar es Salaam. Nje ya geti la kutokea magari katika kituo cha daladala cha Makumbusho jijini Dar es Salaam, gari dogo aina ya Toyota Caldina limepaki pembeni likiwa na spika mbili juu zinazorusha matangazo kwa sauti ya juu. 

“Jipatie nyimbo mbalimbali za parokia zote za ‘Roman catholic’ (Kanisa Katoliki). Nyimbo zote hizi nzuri utazipata kwenye flash kwa bei rahisi,” anasema mtangazaji mwenye sauti ya kiume aliyepo kwenye gari hilo. 

“Sasa nahama kutoka kwenye nyimbo za romani na kuhamia kwenye kuabudu…tenzi zote za rohoni nimezipanga, utazikuta kwenye flash,” anaongeza. 

Nje ya gari hilo yupo binti aliyesuka nywele kiustadi anayechukua flashi kwenye gari hilo na kuwauzia wateja wawili walionekana kuvutiwa na nyimbo hizo. 

Kundi la watu linalosubiria usafiri katika kituo hiki cha daladala majira ya Saa 12 jioni linaendelea kupata burudani ya nyimbo za injili huku wachache wakishawishika kununua kazi hizo za uinjilishaji katika kifaa kidogo cha kielektroniki cha kutunzia taarifa maarufu kwa kimombo kama ‘flash disk’. 

Ni kawaida kwa wakazi wa jiji hili katika siku za hivi karibuni kukutana na magari au baiskeli zenye matangazo ya kuuza kazi za wasanii kwenye flash kwa bei tofauti kuanzia Sh5, 000 hadi Sh20, 000 ikitegemea na nafasi ya kifaa hicho. 

Jambo ambalo wauzaji na wanunuzi hawajui ni kwamba kitendo hicho ni kinyume na sheria na kanuni za nchi zinazoiua uuzaji wa kazi za sanaa za watu bila idhini ya wahusika. Kinawanyonya wasanii na kudidimiza hatua za kusaidia kuzalisha kazi nyingine ambazo zingesaidia kuendelea kuinjilisha au kutoa burudani kwa Watanzania na kuiingiza Serikali mapato.

Moja ya gari linalouza flash za njimbo za injili (lenye spika juu) katika kituo cha daladala jijini Dar es Salaam ambacho ni mwa maeneo maarufu ambayo nyimbo hizo huuzwa. Picha| Nukta Habari. 

Mwanzo wa safari ya “upigaji”

Uchunguzi uliofanywa na Nukta Tanzania kwa miezi minne umebaini kuwa watu hao wanaouza flash huziuza bila idhini ya wahusika licha ya kuwa nyimbo hizo huwa na “malengo ya kuinjilisha watu” kama baadhi wanavyodai. 

Kuanzia katikati ya jiji vituo vya daladala vya Posta, Mnazi Mmoja, Stesheni, Buguruni, Makumbusho hadi Segerea na maeneo mengi, biashara hii imeenea. 

Maeneo mengine maarufu kwa biashara hiyo haramu ni Kariakoo, Mbagala, Mbezi Mwisho Stendi, Kinyerezi, Gongo la Mboto, na Tegeta Mwisho. 

Mara nyingi biashara hiyo hufanyika jioni kuanzia tisa alasiri wakati wakazi wa jiji wakiwa wanatoka kazini. 

“Nyimbo zipo nyingi, unaweza kuzipakua kwenye kompyuta na kuhamishia kwenye flashi tayari unauza. Siyo wote wanaweza kufanya hivyo au wote wanaujuzi huo,” anaeleza Athumani Mbemba, muuza nyimbo za injili kwenye flash. 

Kijana huyo huzipata nyimbo hizo kwa kuzipakua kwenye intaneti na kisha kuzipakia kwenye flash anazozinunua kwa bei ya jumla kwenye maduka ya vifaa vya kielektroniki Kariakoo.

Licha ya kuwa anachofanya ni uvunjifu wa sheria, Mbemba ameiambia Nukta Habari kuwa kazi yake “ni daraja kati yake na wasanii hasa wa injili kwa kuwa mara nyingi kazi zao hupatikana kwa nadra na sio watu wote wanaweza kuzitafuta mtandaoni.” 

Mfanyabiashara huyo ameeleza kuwa kuna nyimbo usiponunua CD, utazikuta YouTube. 

“Sasa kwani wote wanajua ‘kudanilodi’ (kudownload ama kupakua) nyimbo kwenye YouTube, mimi nawasaidia, tena nawachanganyia nyimbo nyingi, nawauzia. Ninafanya kazi ya bwana,” anasema Mbemba.

Anachokifanya mbemba ni kudhurumu kazi za wasanii wa injili kwa kuingilia mauzo ya CD, VCD, DVD na uwezo wa mtu kusikiliza ama kutazama wimbo mtandaoni,  kitu ambacho walau kinaweza kumsaidia msanii kuingiza kipato fulani tofauti na flash zisizomrudishia msanii kitu chochote zaidi ya kufahamika kwa wimbo wake.

Pia, katika mauzo ya CD, VCD, DVD au kanda ya kaseti, Serikali hupata kiasi cha fedha kwenye kila nakala kama ushuru lakini kwenye mziki unaouzwa kwenye flash Serikali nayo inaambulia patupu. 

Kwa nyakati tofauti katika uchunguzi huu waandishi wetu walinunua flash zenye muziki wa injili katika maeneo matano tofauti jijini Dar es Salaam zenye ukubwa kuanzia GB4 hadi  GB16 bila ya kuwa na stampu wala kupewa risiti licha ya kuzidai. 

Katika kituo cha Kariakoo, mmoja ya waandishi alinunua flash aina ya Transcend GB16 yenye nyimbo za dini mchanganyiko ambayo baada ya kufanyiwa majaribio ya kusikiliza kwenye muziki wa kwenye gari na kompyuta ilibainika kuwa sauti za nyimbo zipo chini na zinatofautina ubora kati ya wimbo mmoja na mwingine. 

Flash hiyo pia ilibainika pia kuwa na virusi baada ya kuwekwa kwenye kompyuta jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wake iwapo watazitumia tu bila kuzisafisha na viua virusi kwa kuwa wadudu hao wa kielektroniki huvuruga nyaraka au kufuta kabisa taarifa. 

Licha ya kuwa flash bora yenye ukubwa wa GB16 kuuzwa sokoni kwa kati ya Sh10,000 na 20,000 flash nyingi za ukubwa huo zilinunuliwa na waandishi wetu kwa kati ya Sh6,000 na Sh7,000.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akiangalia baadhi ya DVD feki zilizokuwepo katika moja ya maduka ya Kariakoo, Jijini Dar es salaam Julai, 2016. Picha|Mtandao. 

Mmoja ya wauzaji wa flash ambayo aliomba kutotajwaa jina kulinda kibarua chake anasema ili msanii aweke wimbo katika flash zao, wimbo wake sharti uwe “umehit” (umebamba) na unapatikana mtandaoni lakini hakuna makubaliano yeyote ya kifedha. 

“Ukitaka wimbo wako uwe kwenye flashi, unakuja kuongea na “Boss” na wimbo wako unawekwa,” anasema binti huyo baada ya kuulizwa iwapo kuna kiwango chochote chaa mapato anacholipwa msanii au kwaya husika baada ya kazi zao kuuzwa kwenye flashi. 

“Tunakulipaje sasa,” anasema binti huyo aliyemuuzia mwandishi wetu flashi ya GB16 kwa Sh6,000 ikiwa na nyimbo za injili 35 tu zikiwemo za wasanii maarufu kama Joel Lwaga, Martha Mwaipaja, Paul Clement na Angel Benard.

“Kama utahitaji kulipwa, unaongea na Boss. Kama flashi yenye wimbo wa wako itauzwa sana, utapewa asilimia yako,” alielezea binti huyo huku akiwa hana uhakika na uwepo wa malipo. 

Baadhi ya watu walionunua flash hizo wanasema kuwa zimekosa ubora na nyingi huaribika ndani ya mwezi mmoja ikiwemo kukataa kusoma kwenye redio au kompyuta. Tatizo hilo husababisha wanunuzi nao kupoteza mapato yao kwa kununua bidhaa haramu iliyochini ya ubora. 

Wanunuaji wanalalama

Mkazi wa Morogoro Kennedy William anasema kuwa sehemu kubwa ya flash hizo hazidumu licha ya kuwa mwanzoni hufanya kazi vizuri jambo ambalo awali alidhani vifaa vyake kama redio au kompyuta ni vibovu. 

“Jamaa wengine wapigaji, ilikua nikinunua flash inakaa wiki tu imeharibika, nimeamua ‘kujidownloadia’ (kupakua) kwenye kompyuta yangu. Sihangaiki na watu siku hizi,” anasema William aliye na flash mbovu zenye muziki wa injili zaidi ya tatu.

Wakati wengine wakilia na ubora, baadhi ya wanunuzi hujikuta wamenunua flashi zenye nyimbo tofauti na zile ambazo hutangazwa na wauzaji. 

Mashauri Ndekeja mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam anasema kuwa mara nyingi wauzaji hao huuza flash hizo zikiwa na nyimbo nyingi zisizovutia kusikiliza tofauti na matarajio. 

“Nilinunua flashi ya nyimbo za kuabudu na kati ya nyimbo zaidi ya 50,  nilipenda nyimbo mbili tu. Wanapokuwa wanauza, wanapiga nyimbo maarufu na ukivutiwa ukinunua unakuta matarajio siyo uliyoyahitaji,” Ndekeja anayefanya biashara katika soko la Kariakoo jijini hapa aliiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) hivi karibuni. 


Zinazohusiana:


Waimbaji hawapati chochote

Wakati wanunuzi wa flash za nyimbo za injili wakilalamikia ubora vifaa hivyo vinavyowafaidisha baadhi ya watu isivyo halali, baadhi ya wanamuziki wa nyimbo za injili wanasema wizi wa nyimbo zao ni mkubwa kuliko inavyodhaniwa. 

Mwanamuziki Joel Lwaga anayetamba na wimbo wa ‘Umejua Kunifurahisha’ anasema kuwa hawana makubaliano yoyote na watu wanaouza nyimbo hizo kwenye flash na wamefanya juhudi mbalimbali kulifuatilia suala hilo lakini bado hawajaweza kuwadhibiti. 

“Wameamua tu kufanya hakuna makubaliano yoyote,  inatukwaza, inatuumiza utawafanya nini? mfumo wenyewe wa nchi ulivyokaa ni kama jambo hilo limeruhusiwa hata tulivyojaribu kupiga kelele hakuna mafanikio,” anasema Lwaga. 

Lwaga anasema changamoto za utekelezaji wa sheria pia zinafanya watu hao waendelee kuuza miziki yao isivyo halali kwa sababu ili haki ipatikane inachukua mlolongo mrefu ambao haumalizi tatizo. 

“Kimsingi kumpata yule aliyeanzisha siyo rahisi, wana connection (mtandao) kubwa na watu ambao wanahusika kwenye tasnia hii,” anadai mwanamuziki huyo ambaye nyimbo zake zimekua zikiwavutia vijana ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha. 

Wapo baadhi ya wanamuziki wa injili wamechukua hatua kulinda kazi zao kwa kuwakamata wanaouza nyimbo hizo bila makubaliano, licha ya kuwa wanakumbana na upinzani mkubwa. 

Mwenyekiti wa kikundi cha nyimbo za injili cha Zabron Singers, Marko Joseph anasema kuna wakati waliendesha msako mtaani kuwakamata wauza flash za nyimbo zao bila kibali na kuwafikisha polisi lakini hawakupata matokeo mazuri waliyotarajia.

“Ingawa kuna mfumo huo wa Cosota lakini bado kuna loophole (pengo) ya kisheria, kuna kipindi tuliwahi kuwafuatilia sana lakini hatukufanikiwa,”  anasema Joseph ambaye wimbo wao wa ‘Mkono wa Bwana’ ni miongoni mwa zinazouzwa kwa wingi kwenye flash jijini Dar es Salaam. 

Baadhi ya waimbaji wa injili wanaona uuzaji wa nyimbo hizo kwenye flash hauna tatizo lolote kwa kuwa unasaidia kusambaza injili kwa watu mbalimbali. 

Mwimbaji Florance Mayala maarufu kama Madam Flora anasema unauchukulia muziki anaofanya kama huduma ya kiroho na siyo sehemu ya kujiingizia kipato na angependa wenzake wawe na mtazamo huo ili kuepuka changamoto zisizo za lazima. 

“Mimi naona sawa (wauze nyimbo kwenye flash) tu kwa sababu wanatafuta riziki. Kwa upande wangu mimi sitegemei sana muziki wa injili kwa sababu nafanya biashara zingine na muziki nafanya kama huduma ili kutangaza injili kwa watu ambao haijawafikia,” anasema Madam Flora.  

Hata hivyo, muimbaji huyo anasema ili kuifanya biashara hiyo kuwa na ufanisi na matokeo mazuri kwenye jamii uwepo utaratibu mzuri utakaowezesha viwango vya ubora na sheria zinazingatiwa. 

“Mimi nafikiri kungekuwa na utaratibu wa namna yao wao kuzichukua zile nyimbo kwenye flashi kwa sababu zina wamiliki. Ni vizuri wakafuata utaratibu kuhakikisha hizo nyimbo zinakua na ubora mzuri,” anasema mwimbaji huyo. 

Sheria na jinsi Serikali inavyokosa mapato

Wauzaji hao wa kazi za wasanii wa nyimbo za injili  wamekua wakikiuka Sheria ya Hakimiliki na Hakishirikishi namba 7 ya mwaka 1999 inayosimamiwa na Cosota na Sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura ya 147 chini ya Kanuni za Stampu kwa Bidhaa za Filamu na Muziki ya mwaka 2013.

Sheria hizo zinamtaka mfanyabiashara wa bidhaa za muziki kuhakikisha vifaa vinavyotumika kuhifadhia muziki ikiwemo ‘CD’ na ‘DVD’ zinawekewa stampu za ushuru wa bidhaa zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kabla ya kusambazwa. 

Flash hizi haziwekwi stampu wala wauzaji wake hawatoi risiti yeyote ya mauzo kwa wanunuzi kuonyesha kuwa wanalipa kodi za kazi za muziki na filamu na nyinginezo kama kodi ya mapato. 


TRA na Cosota waingilia kati sakata hilo

Licha ya kuwa nyimbo hizo zinazouzwa kwenye flash na CD zimekuwa njia rahisi ya kufikisha injili kwa watu, TRA inaeleza kuwa wauzaji wafanye kulingana na taratibu za kikodi zilizowekwa na si vinginevyo. 

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo anasema flash hizo zinatakiwa kubandikwa chapa ya mlipa kodi (revenue stamps) kama ilivyo kwa kazi zote za wasanii wa muziki. 

“Lengo lake ni kuwalinda wazalishaji wa hiyo miziki, vile vile kuepuka miziki ambayo ni feki. Hata wale wanaoagiza nje wanajua, ziwe zimefuata compliance (taratibu) na hivyo ziwe zimebandikwa stampu ya mapato,” Kayombo aliiambia  Nukta Habari alipoulizwa iwapo kuna udhibiti wowote wa kimapato kwenye biashara ya muziki wa kwenye flash. 

Anabainisha kuwa iwapo taratibu hizo hazijafutwa, wahusika wanakiuka sheria za kodi na wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria. 

“Kuna taasisi mbalimbali zinazohusika, Cosota (Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki), Polisi na TRA kuhakikisha kwamba hao watu wanakamatwa na wanachukuliwa hatua za kisheria,” anaeleza. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura ya 147, mtu atakayefanya kosa la kuuza vifaa vyenye kazi ya muziki bila stampu anakuwa amefanya kosa na anaweza kuhukumiwa kulipa faini ya Sh2 milioni au kifungo cha miaka miwili jela au vyote kwa pamoja. 

Cosota katika kuwasaidia wanamuziki Tanzania, imesema inashughulikia changamoto hizo kwa wanamuziki ambao ni wanachama wake na ambao wamesajili kazi zao za uimbaji ili kulinda hatimiliki na si vinginevyo. 

“Hawaruhusiwi kuuza nyimbo mpaka wapate kibali cha muhusika. Yawezekana hao wanaouza wanachukua nyimbo za msanii ambaye hajawa mwanachama wa Cosota,” anasema Afisa Usajili na Nyaraka wa Cosota, Magreth Ngasa. 

Ngasa anasema kama kuna mwanamuziki wa nyimbo za injili ambaye amethibitisha nyimbo zake zinauzwa kwenye flash’ bila ridhaa yake anapaswa kuwalisha malalamiko kwenye chama hicho ili hatua za kisheria zichukuliwe. 

“Cosota itapitia hilo andiko lako na kuhakikisha malalamiko yako yana mashiko na baada ya hapo watawaita. Adhabu inategemeana na Cosota watakavyoangalia uzito wa hilo lalamiko, kama ni malipo au fidia,” anasema Ngasa.  

Baraza la usuluhishi la Cosota litatoa maamuzi ya kesi iliyowasilishwa na kama mhusika hajaridhishwa na maamuzi yaliyotolewa, kesi inapelekwa mahakamani kwa hatua zinazofuata. 

Hata hivyo, Cosota inasisitiza wanamuziki kusajili kazi zao kwa mamlaka husika ili kuepuka usumbufu au changamoto pale kazi zao zinapotumiwa vibaya na wasio na nia njema. 

Ili kujihakikishia kipato, wasanii hasa wa nyimbo za injili Tanzania wanapaswa kuwekeza katika masoko ya mtandaoni yatakayowasaidia kuepuka kazi zao kuibiwa. Picha| Bandzoogle. 

Waamua kugeukia masoko ya mtandaoni

Kutokana na kukua kwa wizi wa kazi za wasanii, wanamuziki wa injili wameamua kugeukia masoko ya mtandaoni wanayoweza kuwafikia watu wengi  ili kukwepa wizi wa kazi zao unaofanya na vifaa hivyo.

“Tulishaamua kughairi na utagundua kwa sehemu kubwa mimi sitoi tena CD. Tunachokifanya sasa hivi ni kutoa kazi zetu mtandaoni lakini mambo ya CD tulishaachana nayo,” anasema Lwaga. 

Wanamuziki hao wanasema kuwa siyo rahisi kwa mwanamuziki kufanikiwa katika zama hizi ikiwa atategemea kuuza kazi zake kwenye flash au CD kwa sababu ni teknolojia inayopitwa na wakati na watu wengi wanageukia mifumo ya mauzo ya kidijitali. 

Mbali na mtandao wa Youtube unaotumiwa na wanamuziki wengi, programu zingine zinazotumiwa kimauzo na wanamuziki hao ni pamoja na Spotify, Napster, Apple Music na Tidal.

Nyongeza na Nuzulack Dausen. 

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks