Mambo yatakayosaidia kukuza “startups” za Tanzania mwaka 2020
- Baadhi ya mambo hayo ni kujenga timu imara na kuwekeza katika maudhui ya masoko.
- Wachambuzi wengine wamesema mazingira mazuri ya biashara yanaweza kuchangia ukuaji wa kampuni hizo.
Dar es Salaam. Mwaka unakaribia mwisho wake na mwaka 2020 upo karibu na kona. Katika kipindi hiki watu wa kada tofauti wakiwemo wafanyabiashara hufanya tathmini ili kujiandaa vyema kutekeleza majukumu ya mwaka unaofuata.
Huu ni wakati pia kwa wamiliki wa biashara au kampuni zinazochipukia (startups) kutathmini ni mwenendo (trends) gani utakaowasaidia kukuza biashara zao katika mwaka ujao kwa msaada wa wataalamu wa biashara.
Kama bado unawaza ni mambo gani muhimu ya kuzingatia ili kukuza biashara kwa kiwango unachotaka mwaka ujao, basi mambo haya ni muhimu katika tathmini yako:
Utoaji wa huduma na bidhaa endelevu
Kama unalenga kutengeneza au kuboresha bidhaa zako, basi mwaka ujao hakikisha zinakuwa endelevu ikiwa na maana kuwa zitoe faida za mazingira, kijamii na kiuchumi wakati zinalinda afya ya umma na mazingira katika mzunguko wake wote wa maisha.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kampuni ya kimataifa ya Accenture juu ya matumizi ya bidhaa mwaka 2019, watumiaji wa bidhaa wameanza kupata muamko kununua bidhaa zinazotunza na kulinda mazingira, jambo linalotoa changamoto kwa startups kuongeza ubunifu kuendana na mabadiliko hayo.
Mwaka ujao, utakuwa na kazi kwa wajasiriamali kuangalia namna ya kutengeneza bidhaa ambazo ni rafiki kwa mazingira na wakati huo huo zinachangia katika kuboresha afya za watumiaji na kuongeza faida kwa wawekezaji.
Soma zaidi:
- Mambo muhimu yatakayozisaidia kampuni zinazochipukia Tanzania kukua.
- Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018.
- “Startups” za Tanzania zapewa somo la uwazi, uwajibikaji kuvutia mitaji ya uwekezaji.
Utengenezaji wa maudhui bora ya masoko
Licha ya kuwa matangazo ni muhimu katika kuikuza biashara yako, utengenezaji wa maudhui yanayotoa taarifa kwa kina kuhusu bidhaa au huduma unayotoa nayo ni fursa nyingine katika mikakati ya kutafuta soko (Content marketing).
Kuwapatia taarifa za kina wateja wako katika mfumo video, maandishi au sauti kunaongeza thamani ya bidhaa yako kwa sababu wanafahamu bayana faida zitokanazo na matumizi ya bidhaa husika.
Wachambuzi wa uendeshaji biashara mtandaoni, wanaona hii nayo ni fursa kwa biashara zinazochipukia kukuza biashara zao.
Kuunda timu ya watu wenye weledi wa kufanya kazi
Wachambuzi wa masuala ya kampuni zinazotoa huduma na bidhaa kwa njia ya teknolojia, wanatazamia kuona mwaka 2020, startups zikijikita zaidi kuunda timu ya watu wenye vipaji, wabunifu kwenye kampuni zao ili kuongeza ufanisi katika kazi.
Mwanzilishi na Rais wa programu tumishi (App) ya Calender, John Hall anasema katika makala yake iliyochapishwa katika jarida la Forbes kuwa startups zinalenga kuwaibua na kuwatumia vizuri wafanyakazi bora watakaowezesha kuzivusha biashara katika mafanikio makubwa.
“Suluhisho, mimi na wengine tumelipata, ni kuwekeza katika ukuaji binafsi wa wafanyakazi. Hiyo inamaanisha kuweka mazingira bora ya kazi, uhuru na fidia inayotokana na utendaji ikiwemo mgawanyo mzuri wa faida ili kuendeleza ubunifu na uvumbuzi,” amesema Hall katika makala hiyo ya Novemba 24, 2019.
Kuwapatia taarifa za kina wateja wako katika mfumo video, maandishi au sauti kunaongeza thamani ya bidhaa yako kwa sababu wanafahamu bayana faida zitokanazo na matumizi ya bidhaa husika. Picha| Patrick Tomasso/Unsplash.
Hata wakati, startups zitakuwa na kazi ya kukuza biashara zao mwaka ujao lakini kuna kila haja ya kuweka mazingira mazuri hasa ya uwekezaji ili kutimiza malengo yao ikiwemo upatikanaji rahisi wa mitaji.
Utafutaji wa mitaji kukuza biashara
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayotoa ushauri wa uwekezaji ya SSC Capital, Salum Awadh ameiambia nukta.co.tz kuwa juhudi zinahitajika zaidi katika kuziimarisha startups kifedha ili ziweze kuvumbua bidhaa zinazotatua changamoto zilizopo kwenye jamii.
Awadh amesema pia mabadiliko ya sera bora huchagiza ukuaji mzuri wa startups ili kuongeza wigo wa vijana kujiajiri na kuchangamkia fursa za kuboresha maisha ya watu na kupata kipato.
“Mashirika mengi yanapaswa kujitokeza na kushiriki katika kusaidia startups hasa zinazohusika na sekta ya fedha,” amesema Awadh.
Latest
