Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018
- Zimekuwa mstari wa mbele kutumia teknolojia kutatua changamoto za jamii na kuwa sehemu ya uboreshaji wa maisha ya wananchi.
- Zimewekeza zaidi katika kutumia teknolojia na kujipatia umaarufu ndani na nje ya Tanzania.
- Lakini mwaka 2019 utakuwa wa kukuna vichwa zaidi ili kuziimarisha na kuziendeleza katika ngazi ya juu.
Dar es Salaam. Wakati tukielekea ukingoni mwa mwaka 2018, kuna kila sababu ya kutambua mchango wa kampuni zinazoibukia (Startups) ambazo zimekuwa mstari wa mbele kutumia teknolojia kutatua changamoto za jamii na kuwa sehemu ya uboreshaji wa maisha ya wananchi.
Sekta zilizopata kipaumbele ni pamoja na huduma za fedha, elimu, kilimo, afya na biashara ambapo wabunifu wametumia weledi na uwezo kutengeneza na kuendeleza teknolojia rahisi kuifikia jamii kwa upana zaidi. Nukta imekuletea startups zilizofanya vizuri mwaka huu na kuacha alama kwa watu:
NALA Incorparation Company Limited
NALA ni programu ya simu (Apps) ambayo imepata mafanikio makubwa kwa muda mfupi kwa kuleta mapinduzi katika sekta ya fedha jumuishi ambapo kwa kutumia simu ya mkononi unaweza kupata huduma za miamala na kulipa bili kwa urahisi na uharaka.
Inafanya kazi kama benki ya kijitali bila intaneti jambo linaloitofautisha na Apps zingine ambazo zinahitaji intaneti ili zitoe huduma za fedha. Pia inawawezesha watumiaji kuangalia salio na historia ya miamala yote iliyofanyika kwa wakati muafaka.
App hiyo inayoendeshwa na vijana wa kitanzania wakiongozwa na Benjamin Fernandes; mshindi wa tuzo ya MBA World Summit na Mhitimu wa Shahada ya Umahili katika Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Stanford cha nchini Marekani.
Kutokana na umaarufu wake, Desemba 13, 2018 Kongamano la ujasirimali la Seedstars Africa Summit lililofanyika jijini hapa limeitambua NALA kama App muhimu ilifanikiwa katika kutoa huduma za kifedha Tanzania ambapo imepata fursa ya kushindanishwa na Apps zingine za Afrika mwaka ujao.
Lakini mapema mwaka huu, NALA pia ilishinda tuzo ya benki ya EcoBank ya Afrika ambayo ililenga kutambua startup iliyofanikiwa kutumia teknolojia kurahisisha huduma za fedha kwa wananchi.
Ufanisi wa NALA umeifanya kukubalika zaidi na watu wengi ambapo hivi karibuni ilishika nafasi ya nne katika orodha za Apps za fedha nchini zenye umaarufu katika duka la Google (Play Store) na kukaa katika nafasi hiyo kwa siku 17 mfulululizo.
App ya NINAYO
Ni mtandao wa bure unaotoa huduma za mauzo na ununuzi wa mazao unaotumiwa na wakulima Tanzania. Uzuri wa mtandao huu ni kuwa hakuna gharama za kuweka matangazo ya kununua na kuuza mazao, na ni njia rahisi ya kupata pesa zaidi kutokana na mazao yako.
Licha ya Ninayo kuanzishwa mwaka 2015 na Jack Langworthy imefanikiwa katika kuunganisha wakulima na wanunuzi kwa kutumia njia ya ujumbe mfupi wa maneno (SMS) na kuwaweza kujadili mauzo na kukubaliana bei wenyewe bila kuingiliwa na mtu.
Mapema mwaka huu walipata tuzo za “Entrepreneurial Venture Award” iliyotolewa na Chama cha wahitimuwa masomo ya biashara (AMBA) jiji la London nchini Uingereza. Vilevile mtandao huo uliweza kutambuliwa na Rais Mstaafu wa Marekani Barack Obama katika moja ya hotuba zake mwaka 2016.
Hata hivyo, wanakibarua kigumu cha kuwafikia wakulima wa vijijini ambao bado hawajafikiwa na mifumo ya mawasiliano ikiwemo matumizi ya simu janja na intaneti.
Jinsi Ninayo inavyoonekana unapoingia katika ukurasa wake:Picha| Ninayo
Ni miongoni mwa startups iliyowahi kushinda tuzo ya taasisi ya Seedstars World mwaka 2016 kutokana na mchango wake katika sekta ya afya ambapo imefanikiwa kupunguza gharama za matibabu kwa watanzania maskini kwa kuleta mfumo teknolojia wa bima ya afya.
Jamii Africa iliyoanzishwa na mwanadada Lilian Makoi ina watumiaji zaidi ya 20,000 na imefika katika hospitali 400 ambapo wanaofaidika ni watu wasiokuwa na uwezo wa kulipia bima kubwa kupata matibabu kwa wakati.
Kwa Tanzania imefaniiwa kushirikiana na kampuni ya simu ya Vodacom na Jubilee Insurance ambao kwa pamoja wanamsaidia mtu mtu asiye na bima akatumia huduma hiyo kwa kutumia simu yake ya kiganjani kwa ajili ya kulipia bima.’
Hivyo kwa wale ambao hawana bima za afya kwa sababu moja au nyingine wanaweza kuwa wakapata ahueni iwapo wataijua inavyofanya kazi teknolojia hiyo.
Lilian Makoi mwanzilishi wa Jamii Africa ambaye amewekeza nguvu zake zote kuhakikisha huduma ya afya inakuwa rahisi kwa kutumia simu yako ya kiganjani. Picha| http://africasyouthfirstnetwork.org
App ya Mtabe
Imejipatia umaarufu katika sekta ya elimu kwa mwaka 2018, kwa kuwasaidia wanafunzi wa shule za sekondari kujifunza masomo ya darasani kwenye viganja vyao hata pasipo kuunganishwa na mtandao wa intaneti.
App hiyo iliyoanzishwa na mtanzania Given Edward imefanikiwa kushinda tuzo ya Vijana ya Umoja wa Ulaya (European Youth Awards- 2018) inayowatambua vijana wanaotumia teknolojia kuleta matokeo chanya katika jamii.
Nyota yake iling’aa zaidi mwaka 2015 alipopata tuzo ya Malkia wa Uingereza kwa viongozi vijana (The Queens Young Leaders) ambayo hutolewa kila mwaka kama njia moja ya kuitambua kazi inayofanywa na vijana katika jamii mbalimbali za mataifa ya Jumuiya ya Madola.
Ushindi huo ulitokana na App yake nyingine ya MyELimu kufanya vizuri kama jukwaa la mtandaoni linalowaunganisha walimu na wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari kukutana na kujadili pamoja masomo.
Nini Mtabe itafanya mwaka 2019 katika sekta ya elimu? Hiyo ni changamoto kwao kubuni njia rahisi zaidi kuwafikia wanafunzi wengi kupata maarifa sahihi.
Zinazohusiana:
NALA yaja na teknolojia ya kijanja kutuma, kupokea pesa
Mfahamu Given Edward, mtanzania aliyeshinda tuzo mbili za kimataifa katika sekta ya elimu
Ni kituo cha kijamii kinachopatikana mtandaoni kilichoanzishwa Juni 2018 na na aliyewahi kuwa Miss Tanzania” mwaka 2004, Faraja Kota kwa lengo la kuinua wanawake katika sekta ya uongozi na ujasiriamali, lakini imejipatia umaarufu kwa muda mfupi.
Inawaunganisha wanawake walio chini ya umri wa miaka 35 katika kuhakikisha wanajengewa uwezo kufanikisha mawazo yao ya biashara na ujasiriamali chini ya uangalizi wa walimu “Mentors” wenye uzoefu katika sekta mbalimbali.
Hata hivyo, Starps hizi zitaendelea kutoboa mwaka 2019 na kuwafikia watanzania wengi? Kwa mujibu wa taasisi ya teknolojia ya Information Management inautazamia mwaka 2019 kuwa ni mwaka teknolojia ikiwemo ya Intaneti ya vitu, matumizi ya mtandao wenye kasi zaidi wa 5G, matumizi ya Virtual reality, ndege zisizokuwa na rubani (drone).