Mahakama yamuachia huru Kabendera, atoa neno

February 24, 2020 2:47 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Mwandishi wa habari Erick Kabendera akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuachiwa huru. Picha|Nuzulack Dausen.


  • Mahakama hiyo ilimtia hatiani Kabendera kwa kwa makosa mawili ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha baada ya mshtakiwa kukiri makosa.
  • Ameachiwa huru baada ya kulipa faini ya 100,250,000 huku akiwashukuru wote waliokuwa pamoja naye katika kipindi kigumu akiwa jela.
  • Mahakama imesema Kabendera hana uwezo wa kukata rufaa kupinga hukumu hiyo. 

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru mwandishi wa habari Erick Kabendera baada ya kulipa faini ya 100,250,000 huku akiwashukuru wote waliokuwa pamoja naye katika kipindi kigumu akiwa jela.

Sambamba na hilo, mwandishi huyo anatakiwa kulipa fidia ya Sh173.24 milioni ndani ya miezi sita tangu hukumu hiyo ilipotewa leo Februari 24, 2020 kutokana na kukwepa kodi.

Hiyo ina maana kuwa atatakiwa kulipa takriban Sh29 milioni kila mwezi ili akamilishe kulipa fidia hiyo.

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega ambaye amesema Kabendera hana uwezo wa kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Mapema leo mahakama hiyo ilimtia hatiani Kabendera kwa kwa makosa mawili ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha baada ya mshtakiwa kukiri makosa.

Baada ya Hakimu huyo kueleza hayo, upande wa mashtaka ulimwomba hakimu huyo kutoa hukumu kadri itakavyoona inafaa ila kwa kuzingatia makubaliano kwa kuwa Kabendera ni mkosaji wa mara ya kwanza na hakuna rekodi ya makosa mengine.

Wakili wa Kabendera, Jebra Kambole alimwomba hakimu kuzingatia kuwa mshtakiwa ana familia na ndugu wanaomtegemea.

“Ni zaidi ya miezi sita yupo ndani hili nalo Hakimu lizingatie unapotoa hukumu. Lakini pia mshtakiwa afya yake siyo nzuri,” amesema Kambole.

“Kutokana na mtuhumiwa kukiri makosa yake, namhukumu kama ifuatavyo:

Katika kosa la kwanza kukwepa kodi kulipa faini isiyozidi Sh250,000 au kifungo cha miezi mitatu iwapo atashindwa kulipa faini. Pia, anatakiwa kulipa fidia ya Sh173.25 milioni na kosa la pili la utakatishaji fedha anatakiwa kulipa faini ya Sh100 milioni. Adhabu zote zitakwenda tofauti,” amesema Mtega. 


Soma zaidi: 


Kabendera aliingia makubaliano na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) kukiri makosa yake ambapo upande wa mashtaka umeondoa kosa la kwanza la kuongoza genge la uhalifu.

Kabendera ambaye anaandikia  vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi  alishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam  Agosti 5, 2019 kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi, ukwepaji kodi na utakatishaji fedha. 

Hata hivyo, mwanahabari huyo ambaye amekaa mahabusu kwa takriban miezi saba  amefanikiwa kulipa faini ya Sh250,000 na  Sh100 milioni leo, Wakili Kambole amewaambia wanahabari leo baada ya mteja wake kutoka.

Akizungumza nje ya mahakama baada ya kuachiwa, Kabendera amewashukuru  wanahabari, ndugu na marafiki ambao walikuwa naye bega kwa bega katika kipindi kigumu alichopitia wakati akiwa jela.

“Binafsi napenda niwashukuru wanataaluma wenzangu kwa kusimama na mimi katika maombi, katika faraja, wengi wenu mmefika kunisalimia hapo Segerea (gerezani) na mmeniletea vitabu vya kusoma, mmeniletea magazeti na mmenitia moyo kusimama katika hali niliyokuwa nayo. Kwa hiyo napenda kuwashukuru sana,” amesema Kabendera mbele ya wanahabari.

 #NuktaHanbari
pic.twitter.com/IpEyIjPdfs

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...