Polisi Tanzania yakiri kumshikilia Mwanahabari Kabendera
Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kuwa Mwanahabari, Erick Kabendera aliyedaiwa kutoweka hakutekwa bali alikamatwa na polisi na anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu uraia wake.
Mambosasa aliyekuwa akizungumza na Wanahabari leo (Julai 30, 2019) amesema walimkamata Kabendera jana jumatatu nyumbani kwake Mbweni jijini Dar es Salaam baada ya kukaidi wito wa kufika polisi.
“Aidha mwandishi huyo awali aliandikiwa barua ya wito kufika Polisi kwa ajili ya mahojiano lakini alikaidi wito huo.
“Baada ya kukamatwa mwandishi huyo tumesikia taarifa mbalimbali zikisambaa kuwa mwandishi huyo ametekwa, niseme kuwa mwandishi huyo hajatekwa ila tumemkamata kwa mahojiano,” amesema Mambosasa.
Amesema wanamshikilia na wanaendelea kuwasiliana na maofisa wa Uhamiaji ili Mwanahabari huyo ambaye anafanya kazi na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi ahojiwe kutokana na mashaka kuhusu uraia wake.
“Aidha mtuhumiwa huyo kuna mashaka makubwa kuhusiana na uraia wake tutakapobaini mara moja tutamkabidhi kwenye Idara ya Uhamiaji ili kushughulika naye na ndiyo maana alikuwa akikaidi wito wa polisi na kujihami kuwa ametekwa,” amesema.
Soma zaidi:
Katika hatua nyingine, Mambosasa amewataka wananchi kutii sheria za nchi bila shuruti ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Wakati Kabendera akishikiliwa na Polisi, watumiaji wa mitandao ya kijamii hasa Twitter wameendelea kupaza sauti zao ili kushinikiza kupatikana kwa Mwanahabari Azory Gwanda wa gazeti la Mwananchi ambaye alitoweka tangu Novemba 21, 2017 na hajulikani alipo mpaka leo
Gwanda ni mmoja wa waaandishi waliokuwa wanaripoti juu ya mfululizo wa mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana yaliyowalenga polisi na viongozi wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
Azory Gwanda kama ilivyo kwa Watanzania wengine ana haki ya kuishi, na familia yake ina haki ya kupewa taarifa kuhusu nini kilitokea kwa Azory Gwanda, Pia wanahabari wana haki ya kujua nini kilitokea kwa mwenzao. #ChangeTanzania
#Justice4Azory Sign Here https://t.co/4z7SesgQC5
pic.twitter.com/tItTTS943H— Change Tanzania (@ChangeTanzania) July 29, 2019