Mwanahabari Erick Kabendera ashtakiwa kwa utakatishaji fedha, uhujumu uchumi

August 5, 2019 3:01 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ameshtakiwa kwa makosa matatu ikiwemo utakatishaji wa fedha kiasi cha  zaidi ya Sh173.
  • Makosa aliyoshtakiwa hayana dhamana, jambo litakalomfanya aendelee kusota rumande.
  • Atapandishwa tena kizimbani Agosti 19, 2019 akisubiri kukamilika kwa upelelezi. 

Dar es Salaam. Mwandishi wa  habari za  uchunguzi, Erick Kabendera, aliyekuwa akishikiliwa kwa  zaidi ya siku saba na polisi, hatimaye amepandishwa kizimbani akikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kosa la kutakatisha fedha kiasi cha Sh173.24 milioni. 

Kabendera, ambaye anaandikia  vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi alichukuliwa kwa nguvu nyumbani kwake Mbweni Jijini Dar es Salaam Julai 29, 2019 na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi na wakati wote amekuwa akishikiliwa na polisi. 

Kabendera amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo (Agosti 5, 2019) na kusomewa mashataka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustino Rwezire. 

Mashtaka yanayomkabili mwanahabari huyo ni kuongoza kundi la uhalifu kwa lengo la kupata faida au manufaa mengine, kutokulipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya zaidi ya Sh173.24 milioni na utakatishaji wa fedha kiasi cha  zaidi ya Sh173.24 milioni.

Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na amerudishwa rumande na atarudi tena mahakamani Agosti 19, 2019 kesi hiyo itakapotajwa tena baada ya upande wa jamhuri kusema bado haujakamilisha upelelezi. 

Kutokana na mshtaka yanayomkabili Kabendera hasa la utakatishaji fedha hawezi kupata dhamana, ikizingatiwa kuwa wakili wake, Jebra Kambole alifungua kesi wiki iliyopita kwa niaba ya Kabendera akitaka mteja wake apewe dhamana baada ya kuwa mikononi mwa polisi bila kupelekwa mahakamani. 


Soma zaidi: 


Akizungumza leo nje ya Mahakama ya Kisutu, Kambole amesema mteja wake hawezi kupata dhamana kutokana na aina ya mashtaka yanayomkabili lakini wanapitia hati ya mashtaka na kuangalia namna ya kuchukua hatua za kisheria ili Kabendera apate haki yake. 

“Tumejipanga kwamba tutaenda kupitia hati ya mashtaka vizuri na kuangalia ushahidi uliopo na namna alivyohojiwa na namna gani hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa. Kwa namna ambavyo mashataka haya yameenda, sisi tunaamini siyo makosa ambayo yametokana na kutakatisha pesa, ni makosa ya namna alivyokuwa anafanya kazi zake za kiuandishi wa habari ndiyo ambazo zimemfikisha Erick hapa,” amedai Kambole.  

Siku moja baada ya kumkamata Kabendera yaani Julai 30, 2019, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema  Kabendera hakutekwa lakini alikuwa anashikilikiwa na polisi akisubiri kukabidhiwa kwa maofisa wa uhamiaji kwa ajili ya kuhoji uraia wake lakini leo ameshtakiwa kwa makosa mengine ya uhujumu uchumi. 

Enable Notifications OK No thanks