Magufuli awatoa hofu Watanzania, akihimiza maombi kwa siku tatu

February 19, 2021 11:33 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Viongozi mbalimbali wa Serikali na wafiwa wakiwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam wakati wa kuaga mwili wa marehemu Balozi John Kijazi leo Februari 19, 2021. Picha| Daily News.


  • Amewataka Watanzania kutokuwa na hofu na kuendelea kumtegemea Mungu katika changamoto wanazopitia.
  • Aonya wanaowatisha watu kuhusu vifo vinavyotokea nchini. 
  • Awataka kushikamana ili kuzishinda changamoto zinazolikabili Taifa.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka Watanzania kuepuka hofu na kutishana kuhusu vifo vinavyotokea nchini na kuwataka kushikamana na kumtegemea Mungu pale nchi inapopitia changamoto ikiwemo magonjwa ya aina mbalimbali. 

Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza leo Februari 19, 2021 wakati wa kuaga mwili wa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, marehemu Balozi John Kijazi jijini Dar es Salaam amesema kama Watanzania wamepunguza nguvu ya maombi wanapaswa kuamka tena ili kumuomba Mungu awavushe.

“Tunawaomba Watanzania kama tumetetereka kumuomba Mungu tuanze, kwa leo kwa ndugu zetu Waislamu ambao wameanza, kesho ndugu zetu Wasabato na jumapili kwa ndugu zetu wa Wakristo kwa siku tatu kwa kumuomba na kufunga,” amesema Rais.

Amewataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao ili kuhakikisha suala hilo linapewa kipaumbele katika maeneo yao ili Mungu aliepusha Taifa na changamoto mbalimbali.

“Mimi nina uhakika tutashinda, nataka niwape nguvu hiyo. Tutahangaika sana, Mungu ni mwenye uwezo wa kila kitu. Niwaombe viongozi wa dini kama ambavyo mmekuwa mkifanya endeleeni kuhimiza maombi, tutashinda,” amesisitiza Dk Magufuli. 

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesisitiza kuwa kama maombi yalisaidia kuitokomeza Corona mwaka 2020, basi inawezekana pia mwaka huu na hakutakuwa na ‘lockdown’ huku shughuli za uzalishaji zikiendelea kama kawaida.

“Tulishinda mwaka jana, tutashinda mwaka huu, tutashinda miaka yote kwa sababu Mungu hajaweza kuliacha Taifa hili. Tumeshinda mwaka mwaka jana na tukaingia uchumi wa kati na Corona ipo, uchumi ukaendelea kupanda na Corona ipo. Miradi ikaendelea kutekelezwa wala hatukuweka lockdown, hata sasa hatutaweka lockdown kwa sababu tunajua Mungu yupo siku zote,” amesisitiza Rais Magufuli wakati akitoa salamu za Serikali alipowaongoza Watanzani kuaga mwili wa Balozi Kijazi katika viwanja vya Karimjee jijini hapa. 

Ikumbukwe kuwa Tanzania bado haijaridhia matumizi ya chanjo ya Corona iliyoanza kutolewa duniani. Takwimu za Shirika la afya duniani (WHO) zinaonyesha hadi sasa Tanzania iliwahi kurekodi visa 509 vya corona na vifo 21 na mara ya mwisho ya takwimu hizo kutolewa ilikuwa ni mwanzoni mwa Mei 2020.  

Rais Magufuli amewataka Watanzania kutokuogapa wala kujawa na hofu kwa sababu kifo kipo na kinaweza kusababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo magonjwa ya kupumua. 

“Kufa tutakufa tu, unaweza kufa kwa malaria, kansa, kwa magonjwa mengine kwa sababu kufa kupo lakini kamwe tusimuache Mungu. Huo ndio wito wangu,” amesema Dk Magufuli na kuwataka Watanzania kuacha kutishana na kuzushiana vifo kwenye mitandao ya kijamii.  


Soma zaidi: 


Wakati akimalizia salamu zake kwa wafiwa, amewataka Watanzania kuungana na kuwa wamoja pale matatizo yanapoikabili nchini na kuacha utengano ili kupata ushindi wa pamoja. 

Marehemu Balozi Kijazi ambaye pia alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anatarajiwa kuzikwa kesho Wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Mwanadiplomasia na mhandisi huyo mashuhuri alifariki juzi Februari 17, 2021 katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...