Madhara ya corona: Idadi ya watalii kushuka mara nne Tanzania

Daniel Samson 1123Hrs   Mei 07, 2020 Safari
  • Hiyo ni kutokana na athari za ugonjwa wa Corona hasa kuzuiwa kwa safari za ndege za kimataifa. 
  • Pia ajira na mapato ya sekta hiyo yatapungua zaidi.
  • Wabunge waitaka Serikali kubuni mkakati mbadala wa kuokoa sekta hiyo.

Dar es Salaam. Kutokana na kuenea kwa janga la virusi vya Corona duniani, idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania itashuka zaidi ya mara nne, jambo litakaloathiri ukusanyaji wa mapato na watu watapoteza kabisa ajira zao. 

Matokeo hayo hasi kwa sekta ya utalii Tanzania yatajitokeza ikiwa hali ya ugonjwa huo itatulia ifikapo mwezi Oktoba 2020. 

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Kigwangalla aliyekuwa akizungumza leo (Mei 7, 2020) wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2020/2021 ambapo ameomba kudhinishiwa bajeti ya Sh114.5 bilioni. 

“Kati ya fedha hizo, Sh69.5 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh45.1 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, “ amesema Waziri huyo. 

Hata hivyo bajeti ya mwaka 2020/21 imeshuka kutoka Sh120.2 bilioni ya mwaka huu wa 2019/2020, sawa na upungufu wa Sh6.5 bilioni. 

Kigwangalla ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini amesema kama hali itatulia hadi mwezi Oktoba 2020 idadi ya watalii wanaokuja nchini itashuka kutoka milioni 1.8 waliotarajiwa mwaka huu hadi kufikia watalii 437,000.

Hiyo ni sawa na anguko la zaidi ya mara nne au asilimia 76.5 ya watalii wote waliotarajiwa kuja nchi kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea mbuga za wanyama na fukwe. 

Mlima Kilimanjaro umekuwa ni kivutio kikubwa cha watalii hasa wale wanaopenda kupanda katika milima mirefu. Picha|Mtandao.

Amesema kupungua kwa watalii kumesababishwa hatua zilizochukuliwa za mataifa ambayo ni masoko muhimu ya utalii nchini katika mabara ya Ulaya, Amerika na Asia kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19.

“Hatua hizo zinajumuisha kuzuia raia wake kusafiri na baadhi ya mashirika ya ndege kutofanya safari nje ya nchi, hali iliyosababisha kuathirika kwa sekta hiyo. Ugonjwa huo umeleta madhara makubwa katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii,” amesema Dk Kigwangalla. 

Mashirika yaliyositisha safari zake ni pamoja na Emirates, Swiss, Oman Air, Turkish, Egyptian Air, South African Airways, Rwand Air, Qatar, Kenya Airways, Uganda Airlines, Fly Dubai na Air Tanzania.

Kushuka kwa idadi ya watalii pia kumeathiri ajira za watu walioajiriwa au kujiajiriwa katika sekta hiyo ambapo Waziri huyo amesema idadi ya ajira za moja kwa moja zitashuka kutoka 623,000 zilizotarajiwa hadi kufikia 146,000.

Hiyo ni sawa na kusema ajira hizo zinaweza kupungua kwa asilimia 76.5 mwaka huu. 

Mapato yanayotokana na utalii yatashuka kutoka Sh2.6  trilioni zilizotarajiwa hadi kufikia Sh598 milioni . 

“Upungufu huo wa mapato ni mkubwa kwa sekta na unaweza kusababisha baadhi ya Taasisi za uhifadhi zilizo chini ya Wizara kushindwa kujiendesha ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara,” amesema waziri huyo. . 

Katika kukabiliana na hali hiyo, Wizara inaendelea kuwashirikisha wadau wa sekta ili kuweka mikakati ya namna ya kuisaidia sekta isiathirike zaidi.


Zinazohusiana



Wabunge waonyesha njia kuinua utalii

Mbunge wa Longido, Dk Steven Kiruswa akichangia bajeti hiyo amesema taasisi za wizara hiyo zipunguziwe mzigo wa mapato hasa kipindi hiki cha Corona ili mapato yaliyotakiwa kwenda serikalini yatumike kujikimu.

 “Ningeshauri hebu sasa tuondoe hizo tozo ili kuilimbikizia Wizara ya Maliasili na Utalii fedha kujikimu kipindi hiki kigumu cha mpito,” amesema Dk Kiruswa.

Amesema pia Serikali iangalie iwezekano wa kuongea na wawekezaji waliowekeza katika huduma za utalii na vitalu vya uwindaji ili wasiondoke bali uandaliwe mkakati mzuri utakaosaidia kulinda na kuendeleza maliasili hizo za utalii nchini.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kemilembe Luota amesema kwa sababu idadi ya watalii imeshuka kutokana na janga la Corona kamati yake inashauri kwamba wizara iandae mkakati madhubuti wa makusanyo ya mapato ambao utaakisi halisi ya sasa. 

Mkakati huo uende sambamba na kutoa ahueni kwa wafanyabiashara mbalimbali waliowekeza katika sekta ya utalii ambao wamekuwa msaada kulisaidia Taifa kukusanya mapato yake katika sekta hiyo.

“Serikali ichukue hatua za ziada kuvutia watalii kwa kupunguza tozo mbalimbali zinazoathiri sekta ya utalii kwa mfano “grounding fees” kwa ajili ya mashirika ya ndege yanayotua nchini, tozo za hifadhi, kutoa masharti nafuu ya kuomba viza, kufuta kabisa viza kwa nchi zinazoleta watalii wengi na kuondoa kwa muda kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika sekta hii,” amesema Luota. 

Related Post