Rais Samia: Tanzania kuna wagonjwa wa Corona wimbi la tatu
- Serikali yasema kuna wagonjwa wa Corona ambao wameshaonekana nchini katika wimbi la tatu.
- Awataka Watanzania wachukue tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo.
- Awataka kumuomba Mungu awaepushe na janga hilo
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema tayari kuna wagonjwa wa Corona ambao wameshaonekana nchini katika wimbi la tatu huku akiwataka viongozi wa dini kupaza sauti kwa waumini wao na Watanzania wachukue tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo.
Kauli ya Rais inakuja siku chache baada ya Wizara za Afya za Tanzania Bara na Zanzibar kuwataka Watanzania kujiandaa na kuchukua tahadhari dhidi ujio wa wimbi la tatu la COVID-19.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Juni 25, 2021 katika mkutano wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki jijini Dar es Salaam amesema ugonjwa wa Corona bado uko nchini na tayari wimbi la tatu limeingia tayari.
“Ishara ndani ya nchi sasa zinaonekana, tayari tuna wagonjwa ambao wameonekana kwenye wimbi hili la tatu” amesema Rais Samia.
Amesema hivi karibuni alivyotembelea hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala alikutana na wodi ya wagonjwa wenye matatizo ya kupumua wakiwemo wa COVID-19
Kutokana na kuwepo kwa ugonjwa huo amewataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao na Watanzania kuchukua tahadhari zote zinazopendekezwa na wataalam wa afya ikiwemo kuvaa barakoa na kunawa mikono mara kwa mara.
“Kwa hiyo ni kusema hili jambo bado lipo, tusijiachie, tuchukue adhari zote na tunawaomba sana viongozi wa dini mliseme hili kwa sauti kubwa kwa waumini wetu ili tujiepushe na vile vifo vya makundi,” amesema Rais.
Kwa sasa, Tanzania haitoi takwimu za wagonjwa wa COVID-19 kwa umma na mara ya mwisho ilitoa Mei 2020 ambapo ilirekodi visa 509 na vifo 21.
Hata hivyo, kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema pamoja na kinga zote na njia za kisayansi tunazotumia kujikinga, wasisahau kurudi kwa Mungu na kumuomba awaepushe na janga hilo.
“Pamoja yote hayo, tumuombe Mungu kwa kiasi kikubwa aendelee kutuepusha na kutupa hifadhi yake kutokana na maradhi hasa ya janga hili la Corona kwa kuwa yeye ndiye muweza wa yote,” amesema Rais Samia mbele ya viongozi wa kanisa Katoliki, Kurasini mkoani hapa.
Latest