Dk Mpango: Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 4 mwaka 2020

May 16, 2020 5:50 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Kasi hiyo ya uchumi itashuka kutokana na janga la ugonjwa wa Corona. 
  • Kwa miaka miwili mfululizo uchumi ulikuwa ukikua kwa kiwango cha asilimia 7. 

Dar es Salaam. Kasi ya ukuaji wa uchumi Tanzania inatarajiwa kukua kwa asilimia nne (4) mwaka 2020 kutokana na athari za ugonjwa wa Corona (COVID-19) kwenye sekta mbalimbali nchini, ikiwa ni matarajio ya chini ndani ya miaka ya hivi karibuni. 

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango ameliambia Bunge leo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2020/2021 leo (Mei 15, 2020) kuwa uchambuzi wa awali unaonyesha kuwa pato halisi la Taifa litakua kwa asilimia nne (4) mwaka 2020. 

Awali kabla ya COVID-19 haijalikumba Taifa, Serikali ilitarajia uchumi ungekua kwa asilimia 6.9 mwaka 2020, kwa mujibu wa Msemaji wa Wiazra ya Fedha Ben Mwaipaja. Matarajio hayo yalikuwa yakienda sanjari na wastani wa ukuaji wa uchumi wa asilimia 7 ambao umeshuhudiwa kwa muongo mmoja sasa. 

Hata hivyo, waziri huyo amesema kuwa uchumi ulikua kwa asilimia saba (7) mwaka 2019 ikiwa ni sawa na ilivyokuwa mwaka 2018. 

“Kutokana na uchambuzi wa awali, shabaha za uchumi jumla katika mwaka 2020/21 ni kama ifuatavyo: Pato halisi la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 4 mwaka 2020; mfumuko wa bei kubaki katika wigo wa tarakimu moja; nakisi ya bajeti ya Serikali kufikia asilimia 2.8; mapato ya ndani asilimia 14.5 ya Pato la Taifa; na mapato ya kodi asilimia 12.5 ya Pato la Taifa,” amesema Dk Mpango.

“Matarajio hayo yameshuka kutokana na athari za mlipuko wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona katika sekta mbalimbali,” ameongeza Dk Mpango.


Soma zaidi:


Aidha, amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) itachukua hatua madhubuti kuhakikisha takwimu za mwenendo wa uchumi zinapatikana kwa wakati ili kuiwezesha Serikali na wadau wengine kufanya maamuzi sahihi.

Kwa mwaka jana, sekta zilizoongoza katika ukuaji ni pamoja na uchimbaji wa madini na mawe asilimia 17.7, Ujenzi (asilimia 14.1), sanaa na burudani (asilimia 11.2); na usafirishaji na uhifadhi wa mizigo kwa asilimia 8.7.

Kwa sasa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa reli ya kisasa, mji wa Serikali Jijini Dodoma na barabara ambazo zimechangia kutekeneza kipato na ajira za muda mfupi na mrefu.

Amesema  wizara yake ilichukua hatua mbalimbali za kisera na kiutawala zilizochangia ukuaji wa uchumi kwa kiwango hicho  ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Kufanya Biashara nchini (Blueprint) ili kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Enable Notifications OK No thanks