Lissu kuendelea kusota rumande, uchunguzi uhaini ukiendelea
- Hakimu autaka upande wa Jamhuri kukamilisha haraka uchunguzi.
- Atoa onyo kwa Lissu, mawakili, wahudhuriaji kesi kuzingatia sheria za mahakama.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, Tundu Lissu hadi Juni 16, 2025, uamuzi utakaomfanya endelee kusota rumande kwa zaidi ya miezi miwili tangu ashtakiwe kwa kosa hilo la jinai.
Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alishtakiwa Aprili 10 kwa tuhuma za uhaini akidaiwa kuwa Aprili 3 kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Tangu ashtakiwe mahakamani hapo, upande wa mashtaka umekuwa ukiieleza mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja na nusu.
Leo tena mawakili wa jamhuri walieleza kuwa uchunguzi wa shauri hilo, linalofuatiliwa na wengi ndani na nje ya nchi, bado haujakamilika jambo lililowafanya mawakili wa Lissu kuiomba korti kutupilia mbali kesi hiyo na kumwachia huru Lissu.
Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Mpale Mpoki, Dkt. Rugemeleza Nshala, Peter Kibatala na wengineo walieleza kuwa kitendo cha Jamhuri kushindwa kukamilisha upelelezi kwa wakati kunamnyima mtuhumiwa haki zake za msingi ikizingatiwa kuwa kupitia shauri hilo mtuhumiwa hawezi kujibu chochote.
Baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga ameeleza kuwa kwa sasa sheria haziipi mahakama hiyo fursa ya kufuta kesi kutokana na kucheleweshwa kwa uchunguzi kama ilivyokuwa kwa kesi za miaka ya nyuma zilizorejewa mahakamani hapo na upande wa utetezi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Nassoro Katuga aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo upo hatua za mwishoni.
Hakimu Kiswaga ameuagiza upande wa Jamhuri kuhakikisha unakamilisha uchunguzi na kesi hiyo iliyopangwa kuendelea tena Juni 16, 2025.
Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwamo kukamilika kwa upelelezi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndio ina mamlaka ya kuisikiliza.
Mahakama yamuonya Lissu
Mbali na mjadala wa kucheleweshwa uchunguzi, Hakimu Kiswaga amemuonya Lissu, mawakili pamoja na wahudhuriaji wa kesi hiyo kuzingatia sheria baada ya mwanasiasa huyo kutamka maneno “No reforms” na kisha wafuasi wake kuitikia “No elections’ baada tu ya kuingia kortini.
Kiswaga amesema alichofanya Lissu ni kutoiheshimu mahakama
kwa kuwa alitamka maneno hayo wakati hakimu akiwa ameshaketi.
“Kwa hiyo nihitimishe kwamba maneno aliyosema mshtakiwa hayakuwa sahihi na hawa walioitikia hawakuwa sahihi kwa hiyo kilichofanyika sio sahihi na natoa ovyo sio tu Mshtakiwa na yoyote aliyekuwa mahakamani kutotamka neno lolote bila ruhusa ya mahakama,” amesema Hakimu Kiswaga.
Awali mawakili wa Lissu wameeleza kuwa mtuhumiwa alicheleweshwa kuingizwa kwenye chumba cha Mahakama jambo lililomkosesha uhuru wa kusalimiana na ndugu, jamaa na marafiki zake waliofika kumuunga mkono, utetezi uliokataliwa na hakimu Kiswaga.
Aidha, mahakama hiyo inatarajiwa kupokea ushahidi wa Serikali katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.
Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha mitandaoni taarifa za uongo, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Latest



