Kesi ya Lissu ya uhaini yasogezwa mbele hadi Julai 15

July 1, 2025 5:49 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Mawakili wa Jamhuri waeleza kuwa kwa sasa bado hawajafanya uamuzi wa kumshtaki rasmi Lissu.
  • Lissu ataka kesi hiyo ipelekwe Mahakama Kuu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imehairisha kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu mpaka Julai 15, 2025 kesi hiyo itakaposikilizwa tena.

Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Franco Kiswaga kusikiliza hoja za pande zote mbili kufuatia ombi la upande wa Jamhuri la kuahirisha kwa kesi hiyo.

Mawakili wa jamhuri wameeleza kuwa kwa sasa bado hawajafanya uamuzi wa kumshtaki rasmi Lissu kwa makosa ya uhaini.

Hata hivyo, Lissu alipinga vikali ombi hilo akieleza kuwa hakuna sababu ya msingi ya kuhairishwa kwa kwa kesi hiyo.

Lissu amedai kuwa upande wa Jamhuri kupitia kwa Wakili wa Serikali Mkuu ulikiri kuwa faili la kesi hiyo limeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya uamuzi, lakini bado haijafahamika iwapo litatolewa uamuzi wa kuipeleka Mahakama Kuu au kufutwa kupitia hati ya ‘Nolle Prosequi’.

Mawakili wa jamhuri wameeleza kuwa kwa sasa bado hawajafanya uamuzi wa kumshtaki rasmi Lissu kwa makosa ya uhaini. Picha | Jamhuri Media

“Hii kesi isihailishwe zaidi ya leo, hakuna sababu yeyote ya msingi ya kuipatia hailisho lingine,” amesisitiza Lissu baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza kufuatia maombi ya upande wa Jamhuri kwa mahakama kuairisha kesi hiyo.

‘Nolle Prosequi’ ni hati ya kufuta mashitaka ya Mwendesha Mashtaka (DPP). Hati hii hutolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka kueleza kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi na kuiomba mahakama kufuta mashtaka dhidi ya mtuhumiwa ama watuhumiwa.

Lissu ametoa ombi kwa upande wa mashataka kama wana ushaidi wa kutosha, wasajili taarifa Mahakama Kuu ili kesi hiyo ipelekwe huko, na ikiwa hakuna ushaidi wa kutosha waifute chini ya kifungu 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Baada ya hoja za pande zote mbili, mahakama imeuagiza upande wa Jamhuri kutoa taarifa ya uamuzi wao iliofikiwa ifikapo Julai 15 ambapo kesi hiyo itaendelea kusikilizwa.

Mahakama yasitisha usikilizwaji wa kesi ya uchochezi 

Katika kesi nyingine ya uchochezi inayomkabili Lissu kwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni nayo ilisikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesimamisha kusikilizwa kwa muda usiojulikana. 

Kusimamishwa kwa shauri hilo kumetokana na Lissu kufungua mashauri mawili Mahakama Kuu, moja likiwa la kurejewa kwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kutokutoa uamuzi juu maombi ya Lissu kupinga mashahidi kutoa ushahidi wa kificho na kudai kuwa unahatarisha haki yake ya kusikilizwa kwa haki na ukamilifu.

Kesi nyingine ya uchochezi inayomkabili Lissu kwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni nayo ilisikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesimamisha kusikilizwa kwa muda usiojulikana. Picha | DW

Shauri la pili likiwa ni kupinga mambo ambayo yaliiruhusu upande wa Jamhuri kuleta mashahidi wake kwa kificho kuwa hapakuwepo na ushahidi wa kutosha kumuwezesha hakimu kutolea uamuzi wa kuruhusu ushahidi wa kificho kwa watu ambao sio askari.

Mashauri hayo mawili yalisikilizwa na Jaji Elizabeth Mkwizu Juni 28, 2025 na yanatajiwa kutolewa maamuzi Julai 11, 2025.

Lissu alikamatwa na Jeshi la Polisi Aprili 9, 2025 alipokuwa katika mkutano wa kisiasa wa chama chake mkoani Ruvuma na kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Aprili 10, 2025 ambapo kesi yake inaendelea kusikilizwa.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...