Lissu kujitetea mahakamani, kesi ikipigwa kalenda
- Asema uamuzi huo umetokana na mawakili wake kutopewa nafasi ya faragha kuzungumza naye.
- Kesi yake ya uhaini yaahisishwa mpaka Julai Mosi, 2025.
Dar es Salaam. Mwenyekiti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu amepewa ruhusa na mahakama kujitetea mwenyewe katika kesi ya uhaini badala ya mawakili wake kwa madai ya kuwa wamenyimwa fursa ya faragha kuongea naye.
Ombi hilo lililokubaliwa na mahakama leo Jumatatu Juni 16, 2025 litamfanya Lissu kuchuana na mawakili wa Serikali katika kesi hiyo inayofuatiliwa kwa karibu na wadau wa haki za binadamu ndani na nje ya nchi.
Baada ya kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo asubuhi, Lissu amesema kuwa kwa siku 68 alizokaa mahabusu mawakili wake wamekosa fursa ya kukaa naye muda hitajika kutokana na kuwepo ulinzi mkali.
Lissu, ambaye ni mwanasheria mzoefu kwa zaidi ya miaka 20, ameiambia mahakama kuwa kwa sasa amewekwa katika eneo la watu waliohukumiwa kifo (death row) kinyume na utaratibu licha ya kuwa yeye bado ni mtuhumiwa tu.
Lissu amesema pamoja na kukosa faragha na mawakili wake amekuwa akinyimwa haki ya kuabudu kwa takribani siku 68 tangu alipokamatwa na kupelekwa gerezani ikiwemo Jumapili ya jana Juni 15, 2025.
“Kwa haya ambayo nimeyasema mawakili wangu nawashukuru, walipambana sana, walipigana kitaalamu, mlifanya majukumu yenu na mliyafanya kwa usahihi.
“Hivyo ninaichukua kesi hii mikononi mwangu tena. Kwa hiyo mheshimiwa ‘from now on’ (kuanzia sasa) mimi ndiye nitakaojibizana na hao mawakili wa Serikali”, ameeleza Lissu.
Mara baada ya ombi hilo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga, alitoa uamuzi mdogo wa kumruhusu Lissu kukabiliana moja kwa moja na mawakili upande wa jamhuri.
Mchuano wa hoja
Mchuano wa hoja kati ya Lissu na mawakili wa Serikali ulianza baada ya uamuzi huo ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi Nassoro Katuga aliiomba mahakama iahirishe shauri hilo kwa kuwa jadala la kesi kwa sasa linapitiwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) kwa ajili ya kupelekwa Mahakama Kuu.
Lissu aliipinga hoja hiyo na badala yake aliiomba Mahakama imuamuru Wakili wa Serikali kueleza upepelezi wa kesi yake ulipofikia kama walivyoagizwa na Mahakama hiyo Juni 2, mwaka huu.
“DPP(Mkurugenzi wa Mashtaka) hajawahi kuja hapa, wenye faili la Mahakama ni hawa (mawakili wa Serikali), wanaojua kitu gani kinaendelea ni hawa, wanatakiwa watupe ripoti waliyoipata kwa wapelelezi, waiweke mahakamani, sio maneno matupu,” amesisitiza Lissu.
Aidha Lissu, aliongeza kuwa kama mawakili wa Serikali watasema hawana ripoti ya upelelezi basi mahakama imuite DPP kueleza ripoti ya uchunguzi.
Shauri lazogezwa mbele
Hata hivyo, mara baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Kiswaga ameahirisha shauri hilo mpaka Julai Mosi mwaka huu ambapo alibainisha kuwa hoja iliyotolewa na jamhuri ina mashiko uamuzi ambao Lissu aliuafiki.
Lissu anarejea tena rumande ikiwa zimepita siku 68 tangu ashtakiwe mahakamani hapo, ambapo upande wa mashtaka umekuwa ukiieleza mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Kuhusiana na Lissu kukosa haki zake gerezani Hakimu Kiswaga amesema kuwa madai hayo yamebainishwa na mshtakiwa kama taarifa hivyo yatafanyiwa kazi kiutawala.
Katika kesi nyingine inayomkabili mwanasiasa huyo machachari, mahakama hiyo imeanza kupokea ushahidi wa Serikali katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha mitandaoni taarifa za uongo, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Latest



