Mahakama yakataa ombi la dhamana ya Lissu, kesi yake kuendelea Novemba 3, 2025
- Mahakama imeeleza kuwa kosa la uhaini ni miongoni mwa makosa yasiyo na dhamana kwa mujibu wa sheria
Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imekataa ombi la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, la kutaka apewe dhamana katika kesi ya uhaini inayomkabili, huku ikipanga kuendelea na usikilizaji wa kesi hiyo Novemba 3, 2025.
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa, Oktoba 24, 2025, na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, wakisaidiwa na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, baada ya Lissu kuwasilisha maombi ya dhamana kufuatia ombi la upande wa Jamhuri la kuahirisha kesi hiyo.
Awali, upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa madai kuwa shahidi wa nne ambaye alitarajiwa kutoa ushahidi leo hakuweza kufikishwa mahakamani kutokana na changamoto za usafiri, kwa kuwa baadhi ya mashahidi wapo nje ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, Lissu alipinga ombi hilo akidai kuwa Jamhuri inatumia kisingizio cha mashahidi kuchelewesha mwenendo wa kesi kwa lengo la kumweka gerezani hadi kipindi cha Uchaguzi Mkuu kimalizike.

Alidai kuwa Mahakama inapaswa kuilazimisha Jamhuri kuendelea na kesi au kumpa dhamana ili arejee nyumbani akisubiri mwenendo wa kesi hiyo.
Katika uamuzi wake, jopo la majaji limekubaliana na hoja za upande wa Jamhuri likibainisha kuwa sababu zilizotolewa ni za msingi na zinakubalika kisheria, hasa ikizingatiwa kuwa tangu kesi hiyo ianze, Jamhuri haijawahi kushindwa kuleta mashahidi.
Aidha, Mahakama imeeleza wazi kuwa kosa la uhaini ni miongoni mwa makosa yasiyo na dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo ombi la Lissu la kupewa dhamana halikukubalika.
Kwa mujibu wa Mahakama, usikilizaji wa kesi hiyo utaendelea Novemba 3, 2025, ambapo shahidi wa nne wa upande wa Jamhuri anatarajiwa kuanza kutoa ushahidi wake.
Latest