Kilio bei ya petroli, dizeli ikipanda mwezi Februari

February 5, 2020 9:24 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imepanda kwa viwango tofauti ikilinganishwa na bei zilizotumika mwezi Januari 2020.
  • Ewura imetangaza leo bei mpya kikomo za mafuta za mwezi Februari 2020 na kuonyesha kuwa bei za rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 0.96.
  • Ewura yasema mabadiliko ya bei yanatokana na mabadiliko katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.

Dar es Salaam. Watumiaji wa mafuta nchini Tanzania watalazimika kutoboa mifuko yao zaidi baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za rejareja za nishati hiyo ambazo mwezi huu zimepaa ikilinganishwa na Januari kutokana na mabadiliko katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.

Ewura imetangaza leo bei mpya kikomo za mafuta za mwezi Februari 2020 na kuonyesha kuwa bei za rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 0.96.

Kutokana na ongezeko la bei hiyo, watumiaji wa vyombo vya moto watalazimika kutoboa mifuko yao, ambapo watalipia Sh20 kwa lita zaidi ya bei ambayo walikuwa wananunulia Januari. 

Pia bei za rejareja za dizeli imeongeza kwa Sh74 na mafuta ya taa kwa Sh44 kwa lita. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany, mabadiliko haya yanatokana na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.

Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli  zimeongezeka kwa Sh20.01 kwa lita huku dizeli ikiongezeka kwa Sh74.21 na mafuta ya taa (Sh43.96 sawa na asilimia 2.25).


 Soma zaidi: 


Maumivu hayo pia yatawagusa watumiaji wa nishati hiyo wa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara, inayopokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga ambako nako bei imepanda. 

Kwa mwezi Februari 2020, bei za rejareja za petroli zimeongezeka kwa Sh42 na mafuta  ya taa kwa Sh2 huku bei za mafuta ya dizeli zimepungua kwa Sh18 sawa na asilimia 0.82. 

Pia bei za rejareja za mafuta ya petroli katika mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zimeongezeka kwa Sh35 wakati bei za dizeli zimepungua kwa Sh22. 

Ewura imesema kwa kuwa hakuna mafuta ya taa yaliyopokelewa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika.

“Mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani, mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji,” amesema Mchany katika taarifa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW