Kero za walimu zamuibua Waziri Bashungwa
- Atoa maagizo mazito kwa wakurugenzi, wadhibiti ubora wa elimu.
- Awataka kuwafuata walimu mashuleni kutatua kero zao.
- Tume ya Utumishi wa Walimu yapewa mtihani mzito kupandisha madaraja ya walimu.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa amewaagiza wakurugenzi, wadhibiti ubora na maofisa elimu kutofumbia macho kero za walimu ikiwemo ikiwemo kutolipwa stahiki za uhamisho wa vituo vya kazi.
Bashungwa aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 8, 2022 amesema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko ya kutolipwa na kucheleweshwa kwa stahiki za uhamisho, matibabu, likizo na mazishi.
Pia walimu wamekuwa wakinyimwa vibali vya kwenda mafunzoni na kutolipiwa ada kwa wanaopata vibali.Bashungwa amebaini uwepo wa mawasiliano hafifu baina ya viongozi wanaoshughulikia utoaji wa huduma na walimu, kutopandishwa vyeo kwa wakati sambamba na ukosefu wa nyumba za walimu.
Ili kutatua changamoto hizo, waziri huyo ameagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuwasimamia viongozi wa elimu kwenda mashuleni badala ya kukaa maofisini pekee ili kufuatilia kero na mikakati ya usimamizi na uboreshaji wa elimu na kuwasilisha taarifa zao Tamisemi.
“Ni marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya halmashauri kutafuta huduma. Mwalimu apelekewe huduma shuleni badala ya watoa huduma kukaa ofisini,” amesema Bashungwa.
Zinazohusiana:
- Apps za elimu zitakazowasaidia wanafunzi 2019
- Mfahamu GIven Edward, mtanzania aliyeshinda tuzo mbili za kimataifa katika sekta ya elimu
- Apps za elimu zinazoweza kuwaelimisha watoto wadogo kabla ya kwenda shule
Wakurugenzi na maafisa wa Tume ya Huduma za Walimu wametakiwa kuhamasisha walimu kuingia kwenye mpango wa mafunzo uliopo kwenye kila halmashauri, sambamba na kutoa huduma ipasavyo kwa kuzingatia mwongozo wa waajiri ili kuhakikisha upatikanaji wa vibali vya masomo kwa urahisi na uwazi.
“Naelekeza kuandaa mpango wa mafunzo kulingana na mahitaji…Wakurugenzi wa Serikali za mitaa wawalipie mafunzo wanaopata nafasi,” amesema Bashungwa akiahidi kuboresha vituo vya mafunzo hayo ili walimu wajifunze katika mazingira bora.
Amemuagiza Katibu Mtendaji Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), “kupitia na kuchambua upandaji daraja wa kila mwalimu kwa lengo la kubaini stahiki halali ya daraja la mwalimu na kuchukua hatua stahiki za kuwapandisha madaraja watakaothibitika kucheleweshewa stahiki zao za madaraja.”
Kuhusu uboreshaji wa mawasiliano kati ya walimu na viongozi wao amesema “mwalimu akiandika barua kwa mamlaka ya serikali ya mtaa anapaswa kujibiwa kwa maandishi ndani ya siku saba baada ya kupokelewa.”
Kuhusu nyumba za walimu, amesema “kwa mara ya kwanza Serikali imetenga kiasi cha Sh55.57 bilioni kwa ajili ya ujenzi huo ambapo nyumba 1,916 zitajengwa katika maeneo yasiyofikika kirahisi kwanza.”
Latest
