Upungufu wa walimu shule za msingi unavyoathiri elimu Tanzania
- Ni pamoja na kushusha kiwango cha ufaulu na kupoteza vipawa muhimu.
- Serikali yatakiwa kuendelea kuajiri walimu zaidi.
- Jamii yashauriwa kuuona ualimu kama taaluma ya kuheshimika.
Dar es Salaam. Wakati watahiniwa zaidi ya milioni moja wa elimu ya msingi Tanzania Bara wakiwa wanasubiri hatma yao, baada ya kumaliza mitihani yao jana Septemba 14, 2023, utoshelevu wa walimu katika ngazi hiyo muhimu ya elimu kwa shule za Serikali umeendelea kuwa kitendawili
Kitabu cha hali ya uchumi cha mwaka 2022, kinabainisha kuwa mpaka Disemba mwaka 2022 kulikuwa na jumla ya wanafunzi milioni 10.8 katika shule za msingi za Serikali Tanzania, huku idadi ya walimu katika shule za Serikali ikiwa 173,276.
Hii ni sawa na kusema idadi ya wanafunzi waliopo ni mara 62 zaidi ya idadi ya walimu na hivyo kwa wastani mwalimu mmoja hufundisha darasa lenye wanafunzi 63 kwa wakati mmoja uwiano ambao uko juu ya kiwango kinachotakiwa cha wanafunzi 45 kwa darasa.
Aidha, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inataja Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma kuwa ndio wilaya ambayo mwalimu mmoja hufundisha darasa lenye wanafunzi wengi zaidi wanaofika 103.
Wilaya ya Muleba iliyopo mkoani Kagera ndiyo wilaya pekee iliyofanikiwa kufikia uwiano stahiki kwa wanafunzi 45 kufundishwa na mwalimu mmoja kwa darasa mwaka 2021.

Wakati idadi ya watahiniwa waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2022 ikiongezeka kwa asilimia 22 tofauti na mwaka 2021, idadi ya ufaulu wa jumla ilishuka kwa asilimia 2, ambapo asilimia 21 ya watahiniwa walifeli.
Hii ina maana ya kuwa katika watahiniwa 100, waliohitimu elimu ya msingi mwaka 2022, 20 kati yao walifeli.
Walimu hawatoshi
Pamoja na sababu nyingine zilizochochea ufaulu kuporomoka, huenda upungufu wa idadi ya walimu nchini ikawa ni miongoni mwa sababu hizo.
Nukta habari imezungumza na mdau wa elimu nchini Tanzania Richard Mabala, ambaye amebainisha kuwa upungufu wa walimu wa shule za msingi nchini unawafanya wanafunzi kutohudumiwa kwa muda muafaka.
“Mwalimu anahitaji muda wa kujiandaa na kuangalia kila mwanafunzi, kipindi cha dakika 40 hakitoshi kuhudumia wanafunzi zaidi ya 60 wala kutumia mbinu shirikishi za kujadili na kuchambua, sio rahisi kushirikiana hivyo ubora unashuka,” amesema Mabala ambaye pia ni Mkurugenzi mwenza wa taasisi ya azaki ya Haki Elimu.

Aidha, Mabala ameongeza kuwa uhaba wa walimu huwafanya wanafunzi wakariri kwa ajili ya mashindano ya mitihani ilihali mahitaji ya sasa duniani ni kuwa na watu mahiri wenye ubunifu, unyumbulifu, uchambuzi na fikra tunduizi.
Soma zaidi
-
Veronica Sarungi: TO anayeishi ndoto, taaluma ya ualimu
-
Miongozo mipya elimu maalum kuongeza ujumuishi Tanzania
Tunapoteza vipawa muhimu
Mkuu wa Idara ya Ualimu Chuo cha Agha Khan jijini Dar es Salaam, Veronica Sarungi ameiambia Nukta Habari kuwa wingi wa wanafunzi unamnyima mwalimu nafasi ya kukutana na mwanafunzi mmoja mmoja ili kumsaidia kwa ukaribu zaidi.
“Athari zake ni pamoja na mwanafunzi kupoteza uwezo na vipawa alivyojaliwa kwa kuwa hakuna mtu wa karibu kubaini na kuchochea ili ukue, hivyo kadri mwanafunzi anavyoendelea kukua ndio anapoteza uwezo wake ambao bado haujakomaa na taifa linapoteza nguvu kazi muhimu,” amesema Sarungi ambaye aliwahi kuwa mwanafunzi bora wa kitaifa kidato cha nne mwaka 1988.

Serikali iendelee kuajiri walimu
Pamoja na kwamba hivi karibuni Serikali imekuwa ikitangaza nafasi za ualimu, wadau wa elimu bado wanashauri idadi ya walimu inapaswa kuongezeka zaidi hususani katika shule za msingi za Serikali ambazo zinachukua wanafunzi wengi zaidi.
“Kwa mujibu wa Dk.Shivji kitu cha kwanza katika elimu ni walimu, kipaumbele kinachopaswa kuwekwa katika bajeti ni idadi ya walimu ili wawe wa kutosha, na wapewe ujuzi wa stadi za maisha kwa kuwa wanapaswa kufundisha umahiri wa fikra mpya, kwa kukaribisha mijadala, kupanua mawazo na sio kukariri,” anasema Mabala.
Walimu waheshimike
Hata hivyo, Sarungi anasisitiza kuwa, jamii inapaswa kwanza kubadili mtizamo ilionao kuhusu ualimu na kuitizama kama kazi ya kuheshimika, na sio fani inayokimbiliwa na watu masikini au walioshindwa kusomea taaluma nyingine.
“Tunaweza kutoa nishani kwa walimu, kutoa ufadhili wa masomo kwa walimu, na kuipa kipaumbele taaluma ya ualimu kama wanavyotizamwa madaktari, hiyo itawavutia watu wengi zaidi kuwa walimu,” amesisitiza Sarungi.
Latest
