‘Apps’ za elimu zinavyoweza kuwaelimisha watoto wadogo kabla ya kwenda shule

Rodgers George 0335Hrs   Septemba 15, 2018 Teknolojia
  • Baadhi ya wazazi wasema programu hizo zimefanya watoto wao wajue kuhesabu na kutaja herufi kabla ya kwenda chekechea.
  • Walimu wataka uangalizi wa kina kwa watoto wakati wa kutumia app hizo ili kupunguza uwezekano wa kutazama masuala yasiyofaa.
  • Japo ni jambo jema, madaktari waonya kuwa lazima uwekwe ukomo wa matumizi kwa watoto hao kwa kuwa kuna madhara ya kiafya na kiakili.

Tumezoea kutumia mitandao kwa burudani, elimu na mengineo mengi lakini je, tumewahi kujiuliza kama teknolojia hiyo inaweza kuwasaidia watoto wetu kielimu?

Kupitia michezo ya kwenye simu na kompyuta, mzazi anaweza kumfundisha mwanae kirahisi na kwa ufasaha ikiwa ni nyongeza ya elimu ambayo watoto hupata shuleni.

Teknolojia imetuleta karibu na programu za simu na kompyuta (app) kama “ABC kids”, “Learning numbers”, “Fruits learning” na “Color learning” ambazo zinaweza kumsaidia mzazi kumfundisha mwanaye kwa kutumia simu kabla hata ya kuanza shule ya awali.

Verediana Mwashi, mama wa watoto wawili, amekuwa akitumia simu yake kama shule kwa mwanaye mdogo Janelle. Akirudi jioni Janelle humuomba mama yake simu ili ajifunze herufi pamoja na tarakimu naye aemkuwa akimpatia kwa kuwa  anaona matokeo mazuri kwa mwanae.

“Janelle amekua akiniomba simu yangu punde tu ninapo fika nyumbani,” anasema Verediana.

“Mwanzo niliona ninamharibu lakini nilibadili mawazo pale nilipomuona anahesabu namba pamoja na kusema alfabeti kabla hata sijampeleka shule.”

Verediana anasema hata pale alipoamua kumwanzisha shule ya awali haikua ngumu kwake kuendana na mafunzo aliyopewa shuleni kwa sababu misingi mingi alikua nayo.

ABC Kids moja ya app zinazotumiwa kwa sasa kufundishia watoto wadogo. Wazazi wanapaswa kuzingatia umri wa maudhui yaliyopo kabla ya kuwapatia watoto kujifunza. Picha|ABC Kids.

Hata hivyo, anaeleza uwepo wa changamoto kwenye mafunzo hayo ya kidijitali ikiwemo ughali wa vifurushi vya intaneti hasa pale Janelle anapo hamia YouTube kujifunza. Mbali na masuala ya kifedha, pia inamhitaji awe naye karibu sana na mwanaye pale anapo tumia simu kujifunza ili kuzuia asifungue masuala yasiyomfaa.

“Saa zingine huwakuta na dada yake wameingia youtube wanajifunza na hiyo hunilia sana kifurushi cha internet lakini kama mzazi haina namna kwa maana mtoto anajifunza na siwezi mzuia japo nimemuwekea kiasi cha matumizi hayo” anasema Verediana.

Walimu wanaeleza kuwa matumizi ya teknolojia ya dijitali katika kufundishia watoto ni mazuri iwapo kutakuwa na usimamizi wa uhakika wa wazazi na walezi.


Inayohusiana: Wanafunzi wa kike shule za kata wapata fursa ya kujifunza programu za kompyuta


Mwalimu wa shule ya chekechea ya Geta Day Care, Elizabeth Urio anasema ni vyema mzazi au mlezi akimsaidia kwa upendo mtoto wake wakati wa kujifunza jambo litakalomfanya awe karibu naye kila wakati na kumuepusha na uwezekano wa kutazama vitu visivyofaa mtandaoni.

Ili kuwe na matokeo mazuri, Elizabeth anashauri ni vyema wazazi wakatumia app za masomo kwa kuzingatia umri wa watoto wao kwa kuwa kila programu huwa na maelezo na kigezo cha umri.

“Hata wenzetu wa nchi zilizoendelea wanatumia ‘tablet’ (kipakatishi) kufundishia watoto wao wawapo nyumbani. Hivyo ata kama sisi hatujafikia huko ni kheri kuanza kwa sababu ina manufaa,” anasema.

Syriacus Buguzi, daktari wa watoto, anaeleza kuwa mtoto anapokua karibu na vifaa kama simu na kompyuta inakua sio jambo zuri sana lakini hili hutegemeana na nini anachotazama kwa wakati huo.

“Kama mtoto anapata vitu vzuri vya kujifunza kutoka mitandaoni basi haina shida lakini wazazi wanatakiwa kuweka kiasi cha ukomo wa matumzi hayo,” anasema Dk Buguzi, ambaye pia ni mwanahabari wa masuala ya afya.

Related Post