Rais wa Tanzania aagiza kutolewa ajira za walimu 6,000
- Ni zile ambazo ziko wazi ka sababu mbalimbali ikiwemo vifo na kustaafu.
- Ajira hizo huenda zikapunguza ukame wa ajira kwa walimu.
Dar es Salaam. Wahitimu wa vyuo na vyuo vikuu waliohitimu fani ya ualimu ni miongoni mwa watu wa awali watakaonufaika na utendaji wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kiongozi huyo wa juu kuagiza kujazwa nafasi ya walimu zaidi 6,000.
Iwapo watendaji wa Serikali watatekeleza agizo hilo la Rais Samia kama lilivyoagizwa, kada hiyo sasa itapata angalau itaanza kupata matumaini mapya ya kupata ajira baada ya ukame wa muda mrefu.
Licha ya kuwa kila mwaka mamia ya walimu huhitimu kutoka katika vyuo na vyuo vikuu bado kasi ya nafasi ya ajira ilikuwa haiendani na kiwango cha fursa zilizopo.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya elimu wamesema ajira hizo zitasaidia kupunguza uhaba wa walimu shuleni na Serikali inatakiwa iweke nguvu kuajiri walimu wapya na kuwapeleka katika maeneo yenye upungufu mkubwa.
Katika hotuba yake Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuwaapisha makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na baadhi ya watendaji wakuu wa taasisi za umma, Rais Samia ameziagiza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais na Menejimenti ya Utumishi wa Umma kujaza nafasi 6,000 za walimu ambazo ziko wazi kwa sababu mbalimbali ikiwemo baadhi ya walimu kustaafu ili kuwawezesha wanafunzi kupata walimu wa kuwafundisha.
“Natambua kwamba kuna walimu karibu 6,000 na au zaidi ambao wameacha kazi, wamestaafu, wamefariki na sababu mbalimbali na kunahitajika warudishiwe, hawa siyo ajira mpya ni replacement (kujaza),”amesema Rais Samia leo Aprili 6, 2021.
Amesema suala hilo linatakiwa kufanyika haraka kwa sababu nafasi hizo ziko wazi na zinatakiwa kujazwa mara moja.
“Utumishi uko hapa pamoja na Tamisemi mko hapa naomba mkalitazame hilo, walimu 6,000 warudishwe haraka,” amesisitiza kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Ikiwa nafasi hizo zilizotajwa na Rais zikajazwa, zitasaidia kupunguza ukali wa maisha kwa wahitimu wa vyuo ambao wako mtaani na bado hawajapata ajira za ualimu.

Ajira zitatoa ahueni
Agizo la Rais Samia limepokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa elimu nchini huku wahitimu wa vyuo vikuu wakisema litawasaidia kupata ajira kwa sababu wamekaa nyumbani kwa muda mrefu.
Mhitimu wa fani ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Erick Msaki amesema tangazo hilo la Mama Samia limeamsha matumaini kwa sababu anaamini anaweza kuwa mmoja wa watu watakaojiriwa na Serikali.
“Nimesikiliza hotuba yake nimepata moyo wa kuajiriwa maana nimehitimu mwaka 2015 lakini mpaka leo sikuajiriwa,” amesema Erick ambaye alisomea fani ya ualimu katika sanaa.
Wachambuzi wa elimu Tanzania wamesema ajira hizo ikiwa zitatolewa zitasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa walimu ambalo limekuwa sugu katika shule mbalimbali nchini.
“Walimu 6,000 ni wengi itasaidia kupunguza uhaba lakini siyo kumaliza tatizo la walimu shuleni,” Mdau mashahuri wa elimu na mwandishi wa vitabu, Richard Mabala ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Amesema Serikali iwekeze katika kuajiri walimu wapya kila mwaka kulingana na mahitaji, ongezeko la wanafunzi na kuweka kipaumbele kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa.
“Ni mwanzo mzuri lakini wafanye tathmini ni wapi kuna upungufu mkubwa,” amesema Mabala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya shirika la elimu la HakiElimu na kuongeza kuwa kuajiri walimu wapya haitoshi bali kuwaboreshea maslahi yao ikiwemo mishahara, kupanda vyeo na mazingira mazuri ya kufundishia.
Zinazohusiana:
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari
- Kulikoni walimu kupungua shule za msingi za Serikali Tanzania?
- Hisabati, Kiingereza bado pasua kichwa mitihani darasa la Saba Tanzania
Mitaala ya elimu ipitiwe
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mitaala ya elimu kama inaweza kulivusha Taifa katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya teknolojia.
“Mimi naomba tujiangalieni, mitaala yetu tuiangalie sote sisi ni Watanzania tuone mtaala utakaotupeleka mbele Taifa letu. Tuna viwanda vingi, skilled labour (nguvukazi yenye ujuzi) hatuna. Kwa hiyo elimu mlitizame hilo,” ameagiza Mama Samia.
Pia ameitaka wizara hiyo inayosimamiwa na Profesa Joyce Ndalichako kuangalia uwezekano wa kutumia lugha ya Kiswahili katika masomo ili kukuza zaidi lugha hiyo na kutanua wigo wa ufundishaji wa somo la historia ya Tanzania.
“Sasa hivi, nchi za Kusini mwa Afrika na Afrika Mashariki, Kiswahili ni somo katika syllabus (mitaala) zao lakini siye wenye Kiswahili ni somo kwenye syllabus yetu. Sasa tunavyosema tunakuza Kiswahili sijui! Litazameni vizuri ni mawazo yangu. Msije mkasema Rais kasema,” amesema Rais.
Latest
