Karibu nusu ya watu duniani wanaugua magonjwa ya kinywa
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Brazil wanaohudumu nchini Haiti wakifundisha watoto jinsi ya kutunza afya ya kinywa. (Picha | UN /Marco Dormino.
- Watu wana takriban bilioni 2.5 wameathiriwa na ugonjwa wa kuoza kwa meno.
- Watu 3 kati ya 4 walioathirika wanaishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati.
- Kuimarishwa kwa matibabu kunaweza kupunguza tatizo.
Dar es Salaam. Karibu nusu ya watu duniani wanaugua magonjwa ya kinywa ikiwemo kuoza meno huku kukosekana kwa huduma za afya za uhakika za ugonjwa ikitajwa kama sababu kuu, utafiti mpya umebaini.
Hiyo ni sawa na asilimia 45 au watu bilioni 3.5 wanaugua magonjwa ya kinywa, huku watu 3 kati ya 4 walioathirika wakiishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati.
Ripoti hiyo mpya ya hali ya afya ya kinywa duniani iliyotolewa jana Novemba 18 na Shirika la Afya Duniani (WHO) inatoa picha kamili ya mzigo wa magonjwa ya kinywa na takwimu kwa nchi 194.
WHO inasema visa vya kimataifa vya magonjwa ya kinywa vimeongezeka kwa bilioni 1 katika kipindi cha miaka 30 iliyopita ikiwa ni dalili ya wazi kuwa watu wengi hawana njia za kuzuia na kupata matibabu ya magonjwa ya kinywa.
“Afya ya kinywa kwa muda mrefu imekuwa ikipuuzwa katika afya ya kimataifa, lakini magonjwa mengi ya kinywa yanaweza kuzuiwa na kutibiwa kwa hatua za gharama nafuu zilizoainishwa katika ripoti hii,” imeeleza ripoti hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus amesema shirika hilo limejitolea kutoa mwongozo na usaidizi kwa nchi ili watu wote, popote wanapoishi wawe na maarifa na zana zinazohitajika kutunza meno na midomo yao, na kupata huduma za kinga na matunzo pale wanapohitaji.
Kwa mujibu wa WHO magonjwa ya kawaida ya kinywa ni kuoza kwa meno, ugonjwa ya fizi, kupoteza meno na saratani ya mdomo.
Ugonjwa maarufu zaidi duniani wa kinywa ni wa kuoza kwa meno ambao unaathiri takriban watu bilioni 2.5 na wengi hawatibiwi .
Ugonjwa mbaya wa fizi ndio sababu kuu ya kupoteza meno na unakadiriwa kuathiri watu bilioni 1 duniani kote huku takriban visa vipya 380,000 vya saratani ya kinywa hugunduliwa kila mwaka.
Ripoti hiyo ya WHO inasisitiza kuwa “kukosekana kwa usawa dhahiri katika upatikanaji wa huduma za afya ya kinywa, na mzigo mkubwa wa magonjwa ya kinywa ni hali zinazoathiri watu walio hatarini zaidi na wasio na uwezo.
“Watu wa kipato cha chini, watu wanaoishi na ulemavu, wazee wanaoishi peke yao au katika nyumba za utunzaji wa wazee, wale wanaoishi katika jamii za mbali na vijijini na watu kutoka kwenye vikundi vya wachache hubeba mzigo mkubwa wa magonjwa ya kinywa.”
WHO inasema mtindo huu wa kukosekana kwa usawa ni sawa na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama vile saratani, magonjwa ya moyo na mishipa, kisukari, na matatizo ya akili.
Sababu za hatari zinazoeneza magonjwa yasiyoambukiza kama vile unywaji wa sukari nyingi, aina zote za utumiaji wa tumbaku, na matumizi mabaya ya pombe yote huchangia tatizo la afya ya kinywa duniani kote.

Nini kinasababisha?
Ripoti hiyo mpya ya WHO inasema ni asilimia ndogo tu ya watu duniani wanahudumiwa na huduma muhimu za afya ya kinywa, na wale walio na uhitaji mkubwa mara nyingi wanapata huduma chache zaidi.
Vikwazo vikubwa vya kufikisha huduma za afya ya kinywa kwa wote ni pamoja na:
- Huduma ya afya ya kinywa zinahitaji gharama kubwa nje ya bima. Hii mara nyingi husababisha gharama na mzigo mkubwa wa kifedha kwa familia na jamii.
- Utoaji wa huduma za afya ya kinywa kwa kiasi kikubwa hutegemea watoa huduma waliobobea sana wanaotumia vifaa na nyenzo za hali ya juu, na huduma hizi hazijaunganishwa vyema na miundo ya afya ya msingi.
- Mifumo duni ya taarifa na ufuatiliaji, ikichanganywa na kipaumbele cha chini kwa utafiti wa afya ya kinywa ya umma ni vikwazo vikubwa vya kuunda mfumo na sera zenye ufanisi zaidi za afya ya kinywa.
Dk Bente Mikkelsen, Mkurugenzi wa WHO wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza amesema kuweka watu katika kitovu cha huduma za afya ya kinywa ni muhimu ikiwa tunataka kufikia malengo ya huduma ya afya kwa wote kwa watu binafsi na jamii ifikapo 2030.
“Ripoti hii ni sehemu ya kuanzia kwa kutoa taarifa za msingi ili kusaidia nchi kufuatilia maendeleo ya utekelezaji, huku pia ikitoa mrejesho kwa wakati unaofaa kwa watoa maamuzi katika ngazi ya kitaifa. Kwa pamoja, tunaweza kubadilisha hali ya sasa ya kutojali afya ya kinywa,” amesema Dk Mikkelsen.
Zinazohusiana:
- Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi
- Mambo yatakayokusaidia kupunguza hatari ya kupata saratani
- Fanya haya kulinda afya kazini
Jinsi ya kutunza afya ya kinywa
Upigaji wa mswaki kila siku na kuondoa taka au mabaki ya vyakula ni muhimu kwa kuwa husaidia katika kuondoa bakteria mdomoni. Iwapo taka hizo hazitatolewa, hurundikana na zinaweza kusababisha kuoza kwa meno na magonjwa ya fizi.
Muone daktari wa meno mara kwa mara kwa uchunguzi na matibabu ya mapema iwapo unahisi tatizo.
Latest
