Ufahamu wa ugonjwa wa kula kupita kiasi unaoathiri maelfu kimya kimya
- Mara nyingi hali hizi huambatana na hofu au wasiwasi uliopitiliza kuhusu uzito na umbo la mwili.
Dar es Salaam. Chakula ni miongoni mwa hitaji muhimu la kiumbe hai chochote ikiwemo binadamu kikimsaidia kuimarisha ukuaji na kumpa ustawi wa mwili na akili.
Licha ya umuhimu wake katika maisha ya binadamu, kisipotumiwa kwa kiwango sahihi mtumiaji anaweza kuangukia kwenye changamoto ya ulaji ama ‘eating disorder’ inayoweza kudhoofisha mwili na kukaribisha magonjwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) changamoto ya ulaji ni tatizo la afya ya akili linalohusisha tabia zisizo za kawaida katika ulaji wa chakula, mara nyingi zikiambatana na hofu au wasiwasi mkubwa kuhusu uzito na mwonekano wa mwili.
Ugonjwa huo wa kula umegawanyika katika makundi mbalimbali ikiwemo ‘binge eating disorder’ na ‘bulimia nervosa’, ambayo yote yanahusisha ulaji kupita kiasi.
WHO inabainisha kuwa mwaka 2021 takribani watu milioni 16 duniani walikumbwa na moja ya hali hizo ikiwemo watoto na vijana milioni 3.4 .

Wataalamu wa afya waeleza chanzo
Daktari wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bombo mkoani Tanga, Dk Idi Mgaya, anafafanua kuwa chanzo cha tatizo hili si rahisi kubainika moja kwa moja.
“Ugonjwa wa kula kupita kiasi mara nyingi hauna chanzo kimoja cha moja kwa moja. Ni changamoto inayohusisha mwingiliano wa sababu za kibaiolojia, kisaikolojia na kijamii. Wakati mwingine unaweza kuchangiwa na vinasaba au mazingira,” amesema Dk Mgaya.
Dk Mgaya ameongeza kuwa wanao athirika zaidi ni vijana kuanzia umri wa miaka 18 ambao mara nyingi hukigeuza chakula kuwa njia ya kupata nafuu ya kihisia na furaha inayowapa ahueni ya kiakili.
WHO inabainisha kuwa licha ya ahueni hiyo wagonjwa hao hupitia msongo mkubwa wa mawazo na kuvurugika kwa utendaji wa kila siku, ikiwemo kushindwa kuzingatia masomo au kazi, pamoja na kuathirika kwa mahusiano ya kijamii.

Matibabu
Matibabu ya ugonjwa wa kula kupita kiasi mara nyingi huhusisha tiba ya kisaikolojia, hususan Cognitive Behavioral Therapy (CBT), inayolenga kubadili mitazamo na tabia zisizo sahihi.
Kutibu ugonjwa huu, kunahitaji kufanya kazi kwa ushirikiano na timu ya wataalamu wa afya na afya ya akili wenye utaalamu wa kutibu aina hii ya tatizo la ulaji.
Ingawa watalaamu hao hawajaainisha ni muda kiasi gani mtu anaweza kupona huenda ikawa ni miezi, mwaka au miaka kutegemea na hali ya mgonjwa.

“Tiba huanza pale mgonjwa anapojitambua kuwa ana tatizo. Kupitia CBT, tunamshirikisha mgonjwa katika kuchunguza tabia zake, kumpa majukumu maalum ya kubadili mtazamo na kumjengea uwezo wa kudhibiti hisia zake,” amesisitiza Dk Mgaya.
Wataalamu wanashauri kuwa jamii iongeze uelewa kuhusu matatizo ya afya ya akili ili kupunguza unyanyapaa na kuwahamasisha wahanga kutafuta msaada mapema.
Latest